Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Polisi, DPP wasipigie ramli makosa ya jinai

72490 Liquman

Thu, 22 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mahakama Kuu nchini Singapore imeweka ilani kuhusu mchakato wa haki katika makosa ya jinai. Imeandikwa kuwa utoaji haki katika makosa ya jinai unaundwa na kanuni mbili – ukuu wa utawala wa sheria na ulinzi wa umma.

Kwenye Katiba ya Tanzania, miongoni mwa mambo mengi yaliyoandikwa kama mwongozo kwa maisha ya Watanzania, masuala matatu yamezingatiwa kwa uzito mkubwa – ukuu wa utawala wa sheria, ukuu wa Bunge, mgawanyo wa mamlaka ya mihimili ya dola.

Pamoja na mgongano wa tafsiri, wanazuoni wa sheria wanakubaliana kuwa ukuu wa utawala wa sheria una matawi mawili – udhibiti wa mamlaka ya Serikali na usawa mbele ya sheria.

Kwa kuangalia suala la Singapore; mchakato wa haki katika makosa ya jinai, kanuni yake ya kwanza si utawala wa sheria, bali ukuu wa utawala wa sheria. Pili ni kuulinda umma. Ulinzi wa umma una maana ya kumlinda mwananchi.

Ulinzi wa mwananchi hao unazingatiwa katika mambo matatu; uhuru wake usidhulumiwe wala kubughudhiwa; usiwe kero kwa uhuru wa wengine na mamlaka za nchi ziheshimu uhuru wa mtu.

Tawi la uhuru wa mtu kuwa kero kwa uhuru wa wengine ndilo linalotoa mwanya kwa mamlaka za nchi kuingilia uhuru wa mtu. Hufanya hivyo kwa ajili ya kuulinda umma.

Pia Soma

Watu wenye kutenda makosa mbalimbali ya jinai, tafsiri yake ni kuwa wanatumia uhuru wao vibaya, hivyo kugeuka kero kwa wenzao. Sasa, kwa vile umma lazima ulindwe, inabidi anayebughudhi uhuru wa wenzake achukuliwe hatua ili raia mwema abaki salama.

Katika uchukuaji hatua, upo uwezekano wa mamlaka kutumika vibaya, hivyo hata wasio na makosa kuadhibiwa.

Kwa kutambua hilo, ndio maana imeelekezwa katika ukuu wa utawala wa sheria kuwa Serikali lazima nayo idhibitiwe.

Sasa basi, sheria zipo ili watu walio huru waheshimu uhuru wa wenzao. Kadhalika, sheria zimewekwa kwa minajili ya kudhibiti mamlaka zisionee watu, kubughudhi au kudhulumu uhuru wao – ili watu wafurahie uhuru wao.

DPP anapigia ramli?

Imekuwa kawaida kusikia habari kutoka mahakamani kuwa mshtakiwa kaachiwa huru kwa sababu Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) hana nia ya kuendelea na shauri husika.

Mara nyingi utasikia mshtakiwa baada ya kuachiwa huru anakamatwa tena na kusomewa mashtaka mengine tofauti na yale ya awali. Unajiuliza; ofisi ya DPP huwa inaandaa mashtaka au inapigia ramli?

Mashtaka hayatakiwi kuwa kitu cha kubahatisha. Maana yanagusa uhuru wa watu. Kumweka mtu mahabusu kwa sababu ya tuhuma za uhalifu fulani, kisha baadaye kumwachia kwa kuwa DPP hana nia ya kuendelea kumshtaki, ni kipimo kuwa ofisi hiyo inatenda kazi kwa kubahatisha kama kupiga rami.

Majibu ya ramli yamekuwa hayaaminiki maana ni yenye kubahatisha pia hujaa uchonganishi kwa jamii inayoamini ushirikina.

Ofisi ya DPP kumshtaki mtu, tena kwa kesi nzito isiyo na dhamana, halafu baada ya miezi ikamwachia kwa kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka, halafu mtuhumiwa aliyeachiwa anakamatwa tena na kubadilishiwa mashtaka. Huko si kubahatisha?

Swali; mtu anakamatwa na kufunguliwa mashtaka baada ya kuchunguzwa na kubainika ana makosa, au anakamatwa kwanza kisha ndio makosa yake yanatafutwa?

Mtuhumiwa kukamatwa, kuachiwa huru na kukamatwa tena ni kipimo kuwa Ofisi ya DPP, haijiandai kwa mashtaka. Inatafuta makosa baada ya kukamata mtu.

Wakishaona mashtaka yanadunda au yana upungufu, Ofisi ya DPP inatangaza kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi. Mtuhumiwa akiachiwa anakamatwa tena, ili mashtaka mapya yaandaliwe.

Matendo ya namna hiyo, yanaonesha jinsi uhuru wa watu usivyoheshimika. Ofisi ya DPP inasema haina nia ya kuendelea na shauri, halafu haiombi radhi kwa kuisumbua mahakama wala mshtakiwa. Haisemi ni kwa namna gani itamfidia mshtakiwa kwa usumbufu au kwa kumfanya akae mahabusu kwa makosa ambayo DPP anaona hayana uzani.

Tunaambiwa kuwa alama ya ukuu wa utawala wa sheria ni mamlaka za Serikali kudhibitiwa. Tunaona pia kuwa Ofisi ya DPP inaweza kutenda haya bila udhibiti wowote.

Tunaambiwa pia kuwa udhibiti wa mamlaka za nchi lengo lake ni kumlinda mwananchi. Je, wananchi wanaokamatwa kuwekwa ndani miaka, wakaachiwa a kukamatwa tena wanalindwaje?

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe wamepata kutoa hoja bungeni wakiituhumu Ofisi ya DPP kutumika kuwafungulia watu makosa ya kuwakomoa, kisha hufanya makubaliano pembeni.

Tuseme Ofisi ya DPP inasingiziwa. Lakini kitendo cha kufungulia watu mashtaka na kuwachia, kisha kuwashtaki kwa makosa mengine tofauti tafsiri yake ni nini?

Polisi na maofisa wa Takukuru ambao hukamata, Ofisi ya DPP inayoandaa mashitaka, kwa pamoja lazima waongozwe na tahadhari kuwa wanayemkamata na kumshtaki, ni mtu huru ambaye uhuru wake unalindwa katika nchi huru. Lazima wawe na uhakika na mashtaka yao. Wasipige ramli.

Columnist: mwananchi.co.tz