Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Paul Makonda wa mwaka 2017 na yule wa 2018

16271 MAKONDA+PIC TanzaniaWeb

Sun, 9 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwaka 2017, Rais John Magufuli alichora mstari wa imani yake kuhusu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda. Kwamba ni kiongozi kijana mchapakazi, anayechukiwa na watu kwa sababu ya uhodari wake kazini. Na katika hilo alibeba lawama nyingi kumkingia kifua.

Mwaka 2018, Rais Magufuli amechora mstari wa tofauti kuhusu imani yake kwa Makonda, kwamba ni kiongozi asiyeaminika, vilevile ni mtumiaji mbaya wa madaraka aliyompa. JPM amefika mbali zaidi kwa kumtuhumu Makonda kushirikiana na wafanyabiashara ili kukwepa kodi.

Mabadiliko ya imani hiyo ya Rais Magufuli kwa Makonda ni kipimo kwa Makonda mwenyewe kutambua kuwa mwaka jana alikuwa mwenye kuaminika mno lakini sasa imani hiyo imepungua.

Inawezekana Rais Magufuli akambakisha Makonda kwenye nafasi yake ya ukuu wa mkoa wa Dar es Salaam, kwa matarajio kuwa atajirekebisha. Hata hivyo, haiondoi ukweli kwamba Makonda inabidi awajibike mithili ya mtu afanyae kazi chini ya uangalizi.

Hivi sasa Makonda anatakiwa ama kujenga imani mpya kwa Rais Magufuli au kuirejesha ile ya zamani iliyotoweka. Hapo inabidi yeye mwenyewe ajiulize; nini kilitokea mwaka jana mpaka JMP akawa haambiwi kitu kuhusu yeye na kipi kinajiri sasa hivi hadi kumpambanua katika sura tofauti?

Muhimu zaidi ni kutambua kuwa nafasi yake ni ya kuteuliwa. Hakuna sheria inayombana Rais kumwondoa au kumbakisha, kama ambavyo hakubanwa katika kumteua na kumwacha mpaka leo. Hivyo, kwa vile nafasi yake ni uteuzi, ulinzi wake kazini ni mapenzi ya aliyemteua.

Ajiulize pia jinsi mwaka 2016, Makonda akiwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Rais Magufuli alivyommwagia sifa na kuhoji: “Huyu kijana anavyofanya kazi vizuri, akipanda cheo mtaona anapendelewa?” Kweli alimpandisha cheo. Kuna ulazima wa kujiuliza; imani hiyo imetoweka vipi hadi kumuibua JPM mwenye kauli kali kuhusu makontena?

Tuanze na mwaka 2018

Mgogoro wa kodi kuhusu makontena yaliyoingizwa nchini chini ya jina la Makonda ndiyo yamechokonoa mtazamo mpya kuhusu yeye. Kwa mujibu wa nyaraka za kiofisi, Makonda aliomba msamaha wa kodi kwa makontena hayo kwa sababu yana samani za walimu.

Maelezo ya Makonda ni kuwa samani hizo za kiofisi kwa ajili ya walimu wa shule za Dar es Salaam, zimetolewa msaada na Watanzania wanaoishi nje ya nchi (diaspora). Makonda aliiomba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuruhusu makontena hayo kupita bila kulipiwa kodi kwa vile ni misaada kwa walimu.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango alimjibu Makonda kuwa makontena bandarini hayakuwa na sifa za kusamehewa kodi kwa sababu mosi, aliyetumiwa ni mtu binafsi (Paul Makonda) na siyo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Pili, sheria ya kodi haitoi mwanya wowote wa makontena hayo kupata msamaha wa kodi.

Majibu hayo ndiyo ambayo yaliibua mvutano kati ya Makonda na Mpango. Ikatokea hali ya kutunishiana misuli kuoneshana nani zaidi. Mpango aliahidi kuwa yupo tayari kujiuzulu lakini makontena ya Makonda lazima yalipiwe kodi au yapigwe mnada kufidia kodi. Makonda yeye alitangaza laana kwa Mpango mpaka atakayenunua.

Mvutano huo ndiyo ambao ulimuibua Rais Magufuli, aliyezungumza na taifa kupitia uongozi wa Halmashauri ya Chato. Kauli za Rais Magufuli ndizo ambazo zimedhihirisha imani yake mpya kwa Makonda. Alisema, makontena lazima yalipiwe kodi na akataka viongozi wa wananchi kuwa mfano bora wa kutumikia watu, kwani utumishi bora ndiyo sadaka.

Kauli kadhaa zilionesha jinsi imani ya Rais Magufuli ilivyopungua kwa Makonda. Mojawapo ni ile Rais Magufuli aliyomtuhumu kuwa pengine alikuwa na mazungumzo na wafanyabiashara kuhusu makontena hayo. Hapo ilionesha kuwa Rais Magufuli ana hisia au taarifa kwamba Makonda anafanya udanganyifu kuhusu makontena ili yapite bila kulipiwa kodi.

Kauli nyingine ngumu ya Rais Magufuli kwa Makonda ni ile aliyosema kuwa samani zilizopo ndani ya makontena hayo zingeweza kugawiwa shule chache kisha nyingine zingeuzwa. Kutafsiri hiyo ni kwamba imani ya Rais kwa Makonda imeshuka kiasi cha kumwona ni mdanganyifu, anayekula njama ya kuinyima Serikali mapato.

Rais Magufuli pia alisema kulikuwa na uwezekano wa walimu walikuwa wanatumika ili kufanikisha kupitisha makontena hayo bandarini. Akahoji mbona shule ambazo misaada hiyo inapelekwa hazitajwi? Alionya pia wafanyakazi wa umma wasitumiwe kwa masilahi ya watu binafsi. JPM alihoji: “Kwani walimu walikwambia wanataka makochi, sofa?”

Weka hoja zote za Rais Magufuli kwenye kapu moja, jawabu la jumla ni kuwa Makonda wa mwaka 2018 haaminiki. Inawezekana amekuwa na matukio mfululizo ambayo yamepunguza imani ya JPM au hili suala la makontena limempa ukweli anaouamini zaidi, kwa hiyo ameamua kumshughulikia waziwazi.

Makonda wa mwaka 2017

Machi 17, mwaka jana, Makonda alituhumiwa kuvamia kituo cha runinga cha Clouds TV, akiwa na askari wenye bunduki na kulazimisha kurushwa hewani kwa maudhui yaliyokataliwa na uongozi wa kipindi cha Shilawadu, vilevile menejimenti ya televisheni hiyo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Vipindi na Utafiti, Clouds Media Group (CMG), Ruge Mutahaba maudhui ambayo Makonda alitaka yarushwe yalimhusu Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima. Alipoona maudhui hayo hayaendi hewani, ndipo akavamia kituo.

Kitendo hicho cha Makonda kiliibua sauti ya pamoja ya jumuiya ya wanahabari na wananchi kwa jumla. Kamati ya Bunge, Baraza la Habari Tanzania (MCT), Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo chini ya aliyekuwa waziri wake, Nape Nnauye walionesha mshikamano.

Sauti kubwa iliyopazwa ni ile iliyojaa shinikizo kutaka Makonda ajiuzulu au afukuzwe kazi. Nape aliunda kamati ya uchunguzi wa sakata hilo, akitaka ihoji pande zote mbili ili kupata ukweli. Kwa hali iliyokuwepo, ilionekana nafasi ya Makonda kubaki Mkuu wa Mkoa Dar ni finyu mno.

Makonda alituhumiwa kuvamia Clouds TV Ijumaa usiku, hivyo habari za uvamizi zilianza kusambaa mwishoni mwa wiki. Jumatatu (Machi 20, mwaka jana) asubuhi, ndiyo CMG walitoa tamko lao kupitia kwa Ruge, vilevile wadau wa habari akiwamo Nape, waliitembelea CMG siku hiyohiyo asubuhi. Ilikuwa asubuhi yenye joto la mshikamano wa jumuiya ya wanahabari dhidi ya Makonda.

Ikatokea kwamba siku hiyo, Machi 20, ndiyo ambayo Rais Magufuli alikuwa anazindua ujenzi wa barabara ya juu kwenye makutano ya Ubungo, maarufu kama Ubungo Mataa. Makonda pia alikuwepo. Na Rais Magufuli alijua shinikizo lililokuwepo. Alimwambia Makonda afanye kazi na akataka watu wasimpangie mtu wa kufanya naye kazi.

Machi 22, mwaka jana, yaani siku mbili baada ya Rais Magufuli kutoa tamko hilo la kumkingia kifua Makonda, kamati iliyoundwa na Nape iliwasilisha ripoti yake ambayo moja kwa moja ilimtia hatiani Makonda kuvamia Clouds TV na kuwatisha watangazaji pamoja na waandaaji wa kipindi cha Shilawadu. Taarifa hiyo ya kamati iliwekwa wazi kwa vyombo vya habari.

Asubuhi Machi 23, mwaka jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, alitoa taarifa kwa vyombo habari kwamba Rais Magufuli alikuwa amemteua Dk Harrison Mwakyembe kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Kabla ya uteuzi huo Mwakyembe alikuwa Waziri wa Sheria na Katiba. Profesa Palamagamba Kabudi aliteuliwa kuwa Waziri Sheria na Katiba.

Maana yake Nape aliondolewa kazini bila maelezo yoyote. Hata hivyo, kwa kujiongeza tu, kila kitu kilikuwa wazi kwamba sababu ya kuondolewa ni kwenda kinyume na maagizo ya Rais Magufuli. Alisema Makonda aachwe afanye kazi, yeye akaruhusu kamati yake isome ripoti yenye kumtuhumu au kuthibitisha kuwa kweli alivamia Clouds TV.

Kumbukumbu zaidi kimatukio

Hata baada ya Nape kuondolewa uwaziri, mshikamano wa jumuiya ya wanahabari uliendelea dhidi ya Makonda. TEF walitoa taarifa kutaka Makonda asipewe ushirikiano wowote wa kihabari. Hata hivyo, vipo vyombo vya habari vilivyokuwa vikitoa habari hasi za mkuu huyo wa mkoa wa Dar.

Hilo lilimkera Rais Magufuli na katika moja ya mikutano yake, Ikulu, alihoji kama wamemfungia kwa nini wawe wanatoa habari zake zenye sura hasi? Hili lilionesha wazi kwamba JPM hakutaka kuona Makonda anashughulikiwa na vyombo vya habari wakati yeye alikuwepo. Aliitoa onyo.

Kulikuwa na kelele zilizoshika kasi kuhusu namna ambavyo Makonda alivyoanzisha na kushughulikia operesheni ya kukamata watuhumiwa wa biashara ya dawa za kulevya na wauzaji. Alilaumiwa kwamba alikuwa akivunja sheria na alishusha heshima ya watu wengi. Nape alikuwa mmoja wa waliotoa hoja hiyo. Rais Magufuli alimkingia kifua na kumtaka aendelee na kazi.

Ukifuatilia matokeo ya jumla, namna Rais Magufuli alivyojenga imani kubwa kwa Makonda. Akimpandisha cheo kutoka kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni hadi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, na namna alivyomtetea na kumkingia kifua hasa sakata la uvamizi wa Clouds TV, kisha msimamo mpya kuhusu makontena bandarini, ni kipimo kwamba imani imeshuka kwa kiasi kikubwa.

Makonda anatakiwa kutazama anakosea wapi. Hakuna kiongozi ambaye angependa kuonekana kila siku anamlinda msaidizi wake anayefanya makosa. Zaidi, si sawa hata kama unapendwa na kiongozi wako ndiyo uoneshe tambo na vishindo. Ukimya na uchapaji kazi kwa kufuata utaratibu ni hulka mzuri sana, lakini zaidi ni ulinzi wa nafasi yako kazini.

Kitendo cha Makonda kutoka na kumrudi Waziri Mpango kwa maneno makali ilikuwa kuonesha kwamba yeye ndiye yeye. Mpango ndiye waziri anayesimamia hazina, uchumi na bajeti ya nchi, si mtu wa kubeza. Hivyo basi, pamoja na tuhuma ambazo JPM amezitoa dhidi ya Makonda na makontena yake, muhimu ni Makonda mwenyewe kuelewa kuwa kukosa utulivu na mikogo mingi ni sababu ya kumfikisha alipo.

Sasa anatakiwa kufanya kazi chini ya kiongozi ambaye ameonyesha dalili za kutomwamini. Akiweza awatafute wataalamu wa saikolojia ili wamsaidie jinsi kumudu mazingira ya kufanya kazi katika mazingira hayo, vilevile kujenga imani mpya au kuifufua upya ya zamani iliyosinyaa. Vinginevyo ajiuzulu. Wakati huohuo haieleweki Rais Magufuli anawaza nini.

Columnist: mwananchi.co.tz