Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Okto-bar, Novem-bar, Desem-bar... mchumba hasomeshwi!

81766 Mchumbs+pic Okto-bar, Novem-bar, Desem-bar... mchumba hasomeshwi!

Sat, 26 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Sinza jioni. Niko kwenye baa moja maarufu wahudumu na wateja sura zao hazina ushirikiano wala mwingiliano na wikiendi. Ni kama vile wametekwa na kuhifadhiwa pale. Wanahudumia ili muda uende wakadange kwingine macho yao yanaonyesha kuwa pale ni kama anuani yao tu, lakini kipato wanapata nje ya hapo.

Kitu pekee kinachonipa mzuka ni mademu wanaingia na kutoka kwa wingi. Wamepigilia nguo rafiki na nafsi za wanaume kwenye kipindi hiki cha mvua za pepo la kisulisuli. Hizi mvua sijui zimetumwa na milima ya moto. Pepo la kisulisuli badala ya kuwapa dada zetu waume linaleta mvua ambayo ni faida kwa wamiliki wa nyumba za wageni na hoteli.

Mfukoni nilikuwa na kiasi fulani cha kunywa chupa moja na kusepa, pale baa nilikaa kupoteza muda ili mvua ikikatika niendelee na mishe zangu. Lakini kuna viumbe wa kike waliingia ghafla mpaka maini yalinicheza nikajipiga kifua changu na kujisemesha kuwa: “ Mimi ni nani hata nisiendelee kuwepo hapa?”

Nikamuita mhudumu na kuulizia kama kuna huduma ya pesa pale akajibu kuwa kaunta ipo huduma ya kutoa na kuweka kwa mitandao yote. Kwa jibu hili bila hiyana nikawashukuru mabeberu kwa ‘teknolojia’ hii. Nikainuka na kutoa kiasi ambacho kwa mkazi wa Ilula, angenunua shamba kubwa lenye nyanya, vitunguu na mbaazi ndani yake.

Mimi nilitoa ili lolote likitokea pesa yote iteketee ‘nikionaga’ mademu wazuri mimi sijui ‘najikutaga’ nani jamani. ‘Natamanigi’ hata kupaa hivi kila mtu anione sasa baada ya uhakika wa pesa za kiwanja kuwekwa mfukoni nikawa Samatta na Diamond ghafla ndani ya mwili mmoja. Kujiamini kama kote.

Kutoka neno “Dada naomba kinywaji” mpaka “We lete kinywaji hapa.” Kama pombe ndo husababisha kujiamini hivi, basi Wakenya wanakuwa wamelewa muda wote. Wale jamaa hawana neno “naomba’ wanaponunua kitu hii lugha ipo huku kwetu Vingunguti na Kimara, wao wana neno ‘lete’ tu. Bongo pesa yako bado mhudumu anataka uombe kinywaji.

Pia Soma

Advertisement
Hiki ni kipindi cha kujenga uhusiano mwema na baa hata wahenga walifanya kusudi kutunga majina ya miezi hii. Okto-bar, Novem-bar na Disem-bar. Hawakutaka kukufafanulia ili ujiongeze neno bar mwishoni kule la nini? Toka Januari wewe unahangaikia nini kama huna uwezo wa kujenga urafiki wa maeneo tengefu miezi hii?

Wakati kinywaji kikipita kooni narudisha kumbukumbu enzi za Mkapa dansa wa kike aliposukuma ndinga la milioni 18. Aisha Madinda (RIP). Dar ipo chini ya Mzee Makamba na Kamanda Tibaigana, pindi burudani ikiitwa burudani sigara Sh50 nauli Sh150 popote unapokwenda. Wacha leo nikakumbushie Twanga, tatizo sijui wanapiga wapi.

Kuna vitu haviwezi kujirudia kwenye maisha hata kama waliokifanya bado wapo. Twanga Pepeta inaweza kufanya kile ilichofanya mwanzoni mwa miaka ya 2000. Lakini wana hatuwezi kukutana tena pale Mango Garden kwenye wigo wa michongoma. Itabaki kuwa historia tu kama za kina Mkwawa na wenzake kina Kinjekitile.

Hata hulka na tabia za watu zimebadilika wakati ule ilikuwa lazima tukutane pale, na maeneo mengine ya burudani kama Ngwasuma na ‘klabu’. Leo hii tunaishia kwenye vibaa vya mitaani na kuchekeshana kwenye ‘vigrupu vya wasapu’. Huko ndiko unaweza kuopoa totozi kwa mwonekano wake wa picha au video.

Hata adabu na maisha ni kama imezaliwa upya yale majina ya ‘Pedeshee Hongahonga’ yaliyogeuka kama mashairi kwenye vinywa vya wanamuziki wa dansi. Yametoweka kama uso wa Konde Boy kwenye veranda za WCB wengi wao hata kuishi Sinza au Kinondoni kwao ni anasa.

Waliowahi kukimbia wengi wao wapo hapo Afrika Kusini na nchi jirani waliotia pamba masikioni wako katika kuta chakavu za Segerea pale, ni nyakati tu na kila nyakati na zama zake hata huku mtaani kama huna mizizi mirefu, huna tofauti na waliopo jela. Maisha yamekaza kuliko nati za reli ya SGR ndo maana tunaruka sarakasi kama bisi kwenye kikaango.

Hivi sasa ukimtokea demu akikataa unashukuru unaona kabisa umeepushwa na pepo la kisulisuli, kwa sababu akikubali ni majanga. Enzi za Mkwere walikuwa wasumbufu kwenye ‘apointimenti’ kwa sababu walikuwa na madanga mengi, leo hii sisi ndo tatizo hatuna kitu na zile pesa za kuchezea ndo ziko Segerea na Afrika Kusini.

Kila mtu anataka kuwa Mswati, sihamasishi ngono bali pesa bila totozi ni kama kinywa bila meno. Kama kijana cha msingi tengeneza pesa nyingi uzeeke kama mzee Mengi (RIP). Kwani maisha ni nini? Ni furaha na kupata unachotaka gonga ‘chiazi’ kisha muite ‘weita’ ili alete kama tulivyo apeleke na meza ya tatu yenye totozi tupu.

Kama huna kitu maisha haya utakoma dawa ya mademu ni kuwapiga sana fiksi. Kujituma faragha na zaidi ni kuwa na keshi acha kupoteza muda gym kusaka six packs. Wazee wanapeleka pesa zao Uswisi sisi kama sisi pesa zinaishia kwenye mitungi na mikasi. Mpe maskini kilevi ili asahau shida zake hili andiko kila mnywaji analijua na hulitumia vyema.

Hakuna asiyejua kuhonga tunazidiana tu mipunga. Pale mkwanja unapoongezeka na matumizi hupanda. Honga mpaka mama mkwe akuote kwa niaba ya mwanae acha kupoteza muda kwa mashairi mengi kama Andanenga wewe mpe pesa. Kisha mpe pesa. Muongezee pesa na usiulizie matumizi yake. Ni jukumu lake achague kukuita ‘bebi’ au ‘switi’.

Pesa ndo kila kitu. Wapo wanaoishi kwa pesa za unga bila kuuza wala kusafirisha. Askari, mahakimu, wanasiasa, madaktari, wanamichezo na viongozi wa dini ambao si waaminifu hata kwa nafsi zao. Wanaishi na kutajirika kwa pesa za unga kwa sababu biashara ya unga ina mtandao mpana kuliko CIA wala Al-Qaeda ya Osama. Ni zaidi ya mtandao wa Kanisa Katoliki kuna sehemu unga unauzwa hata Biblia hawaijui. Wauza unga si watu wa mchezo, pesa ya biashara hiyo inatembea kwenye mikono mingi kuliko pesa ya sadaka na ni ngumu sana kuidhibiti. Ngumu sana kuvunja mtandao wa wauza unga pamoja na awamu hii kutolea macho suala hili lakini vita haijaisha. Ili biashara ya dawa za kulevya ife Serikali za dunia nzima zikubaliane kwa pamoja kutotumia pesa kama msingi wa uchumi kwa mataifa na watu binafsi. Pesa isipokuwepo na biashara ya unga itakufa. Tukiendelea kuiabudu mpaka kwenye vibaraza vya nyumba zetu za ibada, biashara ya unga itaendelea kutawala dunia.

Wengi huponzwa na tamaa ya vitu vikubwa zaidi ya uwezo wao. Waathirika ni vijana kwa tamaa zao hupelekea kuwa wahanga wa unga. Kwa kubwia, jela au kwa kuuawa, cha msingi kijana usithubutu kujilinganisha na wengine hili jambo huwatesa wengi sana.

Maisha ya wengi sivyo kama uyaonavyo huenda ukawa na uafadhali mkubwa sana kuliko unaowatamani.

Sasa hata tukija kwenye suala la uhusiano hali ni ile ile tu labda watu wanatofautiana uafadhali. Lakini mauzauza yapo kila sehemu ‘my friend’ jifunze kujikubali na kuikubali hali yako. Jiulize kama wewe dada unatamani kuwa Vanessa Mdee na kaka unatamani kuwa Juma Jux sasa nani atatamani kuwa wewe? Tulia ‘dogo’ na ujikubali.

Ikiwa wewe mwenyewe unajisaliti na kujikana, nani atakayeiona thamani yako? Mtu anapata mfadhaiko kila akimuona jirani yake amepiga hatua fulani kiasi kwamba anashindwa kushughulika na maisha yake. Hakuna ujanja wa kijanja kama kujikubali kama mjanja.

Muda ulivyozidi kwenda totozi zilizidi kuongezeka baa. Sina kumbukumbu nzuri nikashangaa ghafla meza imepambwa na nyuso za kike. Tamu kuliko yale ‘mafilta’ ya insta hawa walikuwa mbele yangu siyo wa mitandaoni, mimi nani hata nishindwe kutumia nao pesa niliyoihangaika kwa jasho langu?

Nikaanza kuzungusha pombe kama kawaida. Watoto wakaendelea kulewa huku wakipiga stori za mjini mara Zari kahama kwenye nyumba ya Dai ‘Sauzi’, Hamisa kamnunulia mamaake gari. Wema baada ya kuzawadiwa gari na Aunty, naye kampa duka la urembo. Mara Wasafi Fm wamesajili watangazaji kama Manchester City.

Ukitaka kujua habari za mjini wakusanye warembo kisha wape pombe utaingia mwaka mpya ukiwa unajua kila kitu na kila mtu kupitia mtungi. Anayekueleza naye kaelezwa kwenye maeneo ya pombe.

Twendeni kulewa na upepo wa kisulisuli. Unacheka mimi kutumia pesa na warembo, sisi tutakucheka wakati ukijutia kwa kusomesha mchumba.

Columnist: mwananchi.co.tz