“Ngoja niwape story ya kweli, mwaka 1999 au 2000, (Thabo) Mbeki atakumbuka vizuri, tulikutana Tokyo (Japan) kwenye G-7 tukawaona hawa wababe kwa dakika 15-20 wakatuuliza mipango yenu kwa Afrika ni nini?”
Kauli hiyo ilitolewa na rais mstaafu wa Nigeria, Olusegun Obasanjo baada ya kubanwa kwa swali na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema wakati wa mjadala kwenye Jukwaa la Sita la Viongozi kuhusu utunzaji wa mazingira na usimamizi mzuri wa rasilimali.
Mjema alimtaka Obasanjo kueleza nini alifanya alipokuwa Rais baada ya kutoa kauli za kulaumu viongozi wengine kushindwa kusimamia yale wanayokubaliana.
Obasanjo anasema kuna wakati walitaka kuweka msimamo wa pamoja, lakini wakajikuta wachache baada ya baadhi yao kujiondoa.
Alisema walikwenda katika mkutano huo wa viongozi wa mataifa tajiri duniani kwa ajili ya kuzungumzia masuala ya maendeleo.
Obasanjo anasema wakiwa huko walipata nafasi ya kukutana na viongozi hao wa mataifa tajiri (G-7) kwa kati ya dakika 15 hadi 20, lakini wakawauliza mipango yao kwa Afrika ni nini, lakini hawakuwa na majibu kwa kuwa hawakuwa na mipango ya pamoja kama bara moja.
Pia Soma
- Ziara ya Dk Bashiru Dar yaondoka na katibu, diwani wa Chadema
- Watano wauawa kwa risasi Marekani
- Papa Francis akwama kwenye lifti, awaomba radhi waumini
Obasanjo anasema kauli ya wababe wale iliwafanya waweke juhudi za kuwa na mikakati ya pamoja. Waliwatuma wasaidizi wao waliokutana nchini Afrika Kusini na ndiko Nepad ikazaliwa.
Anasema baada ya kuwa na Nepad ambayo ndiyo mkakati wa pamoja wa viongozi wa Afrika, mwaka 2002 walikwenda nchini Canada kulikokuwa na mkutano mwingine wa kundi la mataifa nane tajiri, maarufu kwa jina la G-8.
Obasanjo anasema walipofika Canada na kuwasilisha mpango wao wa Nepad, mataifa hayo yalikubali kuwaunga mkono kwa kuwa programu hiyo ilianzishwa na Waafrika wenyewe.
Anasema viongozi wa Afrika walipokutana kwenye mkutano wa Nepad mwaka 2010, waligundua wababe hao hawakuwa na haja ya kuwasaidia kwa kuwa walikuwa wameachana nao na hakukuwa na mawasiliano.
Hata hivyo, Mbeki alichangia hoja hiyo ya Obasanjo kwa kumkumbusha kwamba katika kundi hilo la marais watano pia alikuwapo Benjamin Mkapa ambaye ni Rais wa Awamu ya Tatu wa Tanzania aliyemaliza utawala wake mwaka 2005.
Mbeki anasema katika kundi lao la marais watano walihakikisha wanashirikiana ili kuweka msukumo wa pamoja katika maendeleo ya Afrika.
Anasema katika kundi lao walianza kujadili changamoto zinazoikabili Afrika na walipokutana Addis Ababa nchini Ethiopia walijadili na kuona uwezo upo lakini hawajaweza kukaa pamoja.
Mbeki anaongeza kuwa kuna wakati viongozi wanakuwa wanahitaji kupewa moyo na wananchi, mfano kama wananchi wataamua kuandamana kupinga ubabe wa mataifa makubwa kutawapa nguvu viongozi wao wa Afrika.
Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa alichangia hoja hiyo kwa kusema kuwa lazima viongozi wawe na umoja, ushirikiano na kuvutia wananchi katika umoja wao kama viongozi.
Hata hivyo, Mwenyekiti na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Infotech Investiment Group Limited, Ali Mfuruki alipigilia msumari wa moto kwa kusema wakati alipokwenda makao makuu ya Umoja wa Afrika yaliyopo Addis Ababa nchini Ethiopia waliambiwa kuwa kuna maazimio zaidi 1,400 yaliyopitishwa na viongozi wa Afrika hayajafanyiwa kazi tangu yalipopitishwa miaka mingi imepita.
Mfuruki anasema pia walielezwa ofisi nyingi za taasisi za kimataifa zipo Addis Ababa kwa kuwa wajua hapo ni makao makuu na viongozi wote wa Afrika wanakutana hapo lakini viongozi hao hawazitumii.
Anasema licha ya kuwapo ofisi hizo, viongozi wengi huwa hawahudhurii mikutano na badala yake huishia kutuma wawakilishi, lakini inapotokea mikutano nje ya Afrika huko viongozi huudhuria wenyewe bila kutuma wawakilishi.
Mfuruki anasema kutokana na hali hiyo hata watumishi walioko katika ofisi hizo hawana maslahi mazuri na wakati mwingine husotea hata pensheni zao.
Anasema kutokana na hali hiyo ndio maana wafanyakazi wengine wamekuwa wakitafuta safari kwa ajili ya kupata posho ili kuendesha maisha yao.
Mfuruki anasema kutokana na utamaduni wa viongozi wa Afrika wa kutohudhuria mikutano ya maamuzi katika umoja wao ndio maana nchi zilizoendelea kila mmoja anataka kuitawala Afrika anavyotaka.
Alitoa mfano namna mataifa hayo yanavyojitapa kila mmoja kutaka kuisaidia Afrika, lakini kwa malengo yao. Na ndio maana viongozi wengi wa Afrika wanakimbilia kuhudhuria mikutano ya nje ya Afrika. Mfano, hivi sasa huko Yakohoma nchini Japan kuna mkutano unoitwa TICAD unaohusisha ushirikiano wa maendelo kati ya Japan na nchi za Afrika.
Pia, kuna ushirikiano wa kibiashara wa Afrika na Marekani unaoitwa AGOA na kuna ushirikiano mwingine wa kibiashara kati ya China na Afrika unaojulikana kama Sino-Africa.
Mfuruki alisema kutokana na hali hiyo Afrika imekuwa kama binti mrembo ambaye kila kijana anamtamani. Na kwamba kama Afrika itaendelea na njia hiyo haitafika popote.
Mwendeshaji wa mjadala wa jukwaa hilo, Julie Gichuru alirushwa swali kwa Rais mstafu wa Madagascar, Hery Rajaonavimampianina kwamba huyu binti mrembo anayegombaniwa na mataifa tajiri nini kifanyike ili Afrika ijinasue?
Julie alitumia ubeti wa wimbo wa Bob Marley kwamba ‘jikwamue mwenyewe kutoka katika fikra za kitumwa’ akimaanisha ni wakati kwa Afrika kujikomboa kutoka kwa wakoloni kwa kuondokana na fikra tegemezi.
Julie alimuomba kiongozi huyo wa zamani wa Madagascar kutoa maoni yake kuhusiana na namna Afrika invyogombewa na mataifa tajiri.
Mstaafu huyo anasema jambo la muhimu ni kuweka mtazamo kwamba Afrika ni tajiri na kwamba matatizo yote waliyozungumza hayawezi kutatuliwa na mtu mmoja mmoja ni lazima kuyafanya kwa pamoja kupitia Umoja wa Afrika.
Kwa upande wake Rais John Magufuli anasema yapo matatizo kadhaa yanayoifanya Afrika ishindwe kuendela miongoni mwa matatizo hayo ni masalia ya fikra za kikoloni kwa kushindwa kutafsiri vizuri dhana ya uhuru.
Anasema lengo ni kurejesha rasilimali, kuzisimamia na kuziendeleza. “Lakini, sisi bado tunaamini wakoloni ndio wanaweza.”
Anasema rasilimali nyingi za Afrika zimekuwa zikichukuliwa na wakoloni kama malighafi na wanazirejesha zikiwa bidhaa kamili kwa ajili ya kuziuza tena kwa gharama kubwa.
Anasema kwa kushindwa kusimamia vizuri rasilimali kumeifanya Afrika iendelee kudanganywa kwamba msingi wa maendeleo ni fedha.
Rais Magufuli anasema pia tatizo lingine ni ukosefu wa ubunifu na kutokuwa na viwanda, kwa maana ni lazima ijikite katika kukuza ubunifu ili kuwa na viwanda vyenye kuzalisha bidhaa kamili badala ya kuuza malighafi.
Anasema pia Afrika limekuwa ni bara lenye migogoro na hali tete ya kisiasa, kiasi kwamba maliasili iliyopo imekuwa ikiporwa na wageni. Anaongeza kuwa tatizo lingine ni mikataba mibovu waliyoingia na mabeberu kiasi cha kuifanya iedelee kunyonywa na kuwa masikini zaidi. Na kwamba ili kuondokana na hali hiyo ni lazima Afrika isimamie vizuri na kuitumia kwa ajili ya maendeleo rasilimali zake.