Katika toleo la jana tuliona jinsi ndege ya timu ya kushughulikia kupotea kwa ndege yenye Wayahudi ilivyoundwa. Mara baada ya kufahamika kuwa ndege iliyokuwa na Wayahudi ndani yake imepoteza mawasiliano, habari za kijasusi kuhusu ndege hiyo zilianza kumiminika robo saa tu kabla ya kuvunjika kwa kikao cha Bunge la nchi hiyo kilichokuwa kikiendelea siku hiyo. Waliojumuishwa katika timu hiyo ni waziri mkuu na mawaziri wengine watano wa baraza lake. Miongoni mwao alikuwamo pia Mnadhimu Mkuu wa IDF, Luteni Jenerali Mordechai “Motta” Gur, ambaye alikuwa akisifiwa sana kama mwanajeshi mahiri. Kila mjumbe wa timu hii alikuwa na wataalamu wake waliobobea katika nyanja mbalimbali za kigaidi, kijeshi, kisiasa, kidiplomasia na kijamii. Walikutana kwa haraka kwa ajili hiyo. Kwao hili la kupotea kwa ndege yenye Wayahudi lilikuwa jambo la udharura wa hali ya juu sana. Sasa endelea…
Wakati ndege hiyo ikielekea Paris, Rais wa Ufaransa, Valery Giscard d’Estaing, alikuwa kwenye ndege nyingine kwenda kukutana na Rais Gerald Rudolph Ford wa Marekani katika mkutano uliofanyika Puerto Rico. Pamoja naye walikuwamo mawaziri waandamizi wa serikali ya Ufaransa.Waliokuwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Charles de Gaulle mjini Paris wakisubiri kuwapokea wageni wao waliokuwa kwenye Ndege Flight 139 waliona mabadiliko ya muda wa kuwasili kwa ndege hiyo. Badala ya muda kusomeka saa 7:35 mchana, ilibadilishwa na kusomeka ‘IMECHELEWA’.
Baadaye kidogo sauti ikasikika: “Attention!” kisha likatolewa tangazo lililoihusu ndege hiyo, “Shirika la Ndege la Ufaransa linaomba radhi kuchelewa kwa ndege yake, Flight 139. Wote wanaoingojea ndege hiyo tafadhali mnaombwa kufika ofisi kuu ya shirika kwa maelezo zaidi...”
Wakati ule ule ambao ndege hiyo ilikuwa imepangwa kutua katika jiji la Paris ndio wakati huo huo ambao ilikuwa katika hatua zake za mwisho za kutua katika Uwanja wa Ndege wa Benghazi, Libya. Hii ilizua hofu mbaya zaidi.
Wakati ndege hiyo ikitua Libya, nchini Israel tayari ilikuwa ni jioni. Kikosi kazi cha kushughulika na hali za dharura kilikuwa katika pilikapilika za kushughulikia upotevu wa ndege hiyo. Kufikia wakati huo, ukweli fulani kuhusu tukio hilo ulikuwa umeanza kuibuka. Sasa ilikuwa imejulikana kuwa ndege imetekwa na ilikuwa inaelekea Libya. Hii ilikuwa ni vita mpya dhidi ya Israel iliyoanzishwa na kikundi cha Harakati za Kuikomboa Palestina (PFLP), ambacho kiongozi wake alikuwa ni Dk Wadi Hadad.
Habari zinazohusiana na hii
Kwa mujibu wa kitabu ‘The Israeli Secret Services and the Struggle Against Terrorism’ cha Ami Pedahzur, Dk Hadad alikuwa anasimamia kikosi cha wapiganaji wenye msimamo mkali. Majasusi wa Israel waliamini kuwa Dk Hadad aliondoka Lebanon na kwenda eneo fulani la Afrika kutoa mafunzo ya kigaidi kwa vijana chipukizi.Dk Hadad alihusishwa pia na kutekwa kwa ndege ya Ubelgiji Mei 1972 iliyoruka kutoka uwanja wa ndege wa Ben-Gurion Airport jijini Tel Aviv, lakini ikarejeshwa uwanjani hapo na makomandoo wa jeshi la Israel waliojifanya kuwa ni mafundi wa ndege. Katika tukio hilo waliwaua Waarabu wawili waliokuwa na silaha lakini abiria 97 wa ndege hiyo waliokolewa.
Taarifa za mwanzo kabisa za watekaji wa ndege hiyo zilitoka katika Jiji la London usiku wa Jumapili ya Juni 27-siku ile ya kutekwa kwa ndege hiyo. Taarifa hizo za kijasusi zilidokeza kuwa Wajerumani wawili ndio walikuwa wakisimamia utekaji huo na kwamba watekaji walikuwa wanatumia “mpango ulioandaliwa vyema na kwa uangalifu” na kwamba Ndege Flight 139 ingepelekwa katika nchi ambayo ni “rafiki kwa magaidi”.
Kitabu ‘No Waiting for the Messiah’ cha Morton Mayer Berman kinasema kuwa kidokezo muhimu sana kilitoka kwa msichana mmoja wa Kiingereza, Patricia Heyman, mwenye umri wa miaka 30, ambaye alisema aliwashawishi watekaji wake wamwachilie Benghazi kwa sababu alikuwa na ujauzito na alikuwa katika hatari ya kujifungua.
Katika ukurasa wa 77 wa kitabu ‘Terrorism in Africa’ cha Martha Crenshaw, Pat Heyman alikuwa na hati ya kusafiria ya Uingereza, lakini nyumbani kwake ilikuwa ni eneo la Petach Tikva, Israel. Hakusema chochote hadi alipopakiwa kwenye ndege ya kawaida ya Shirika la Ndege la Libya ambayo alisafiri nayo kwenda London, Uingereza.
Akiwa London ndipo wapelelezi wa Scotland Yard walipoanza kumhoji kwa saa tano. Alihojiwa na wataalamu mbalimbali wa ujasusi. Taarifa za awali zilizotolewa na mwanadada huyo zilidakwa na Serikali ya Israel.
Taarifa ambazo majasusi wa Uingereza walizipata kutoka kwa Pat Heyman walilishirikisha Shirika la Kijasusi la Israel (Mossad). Taarifa iliyotumwa kwa ujasusi wa Israel ilisema: “Dakika tano baada ya kuondoka Athens, Ndege 139 ilitekwa na mwanamke wa Ujerumani, mwanamume wa Ujerumani na watu wengine watatu walioonekana kama ni Waarabu, hiyo ni kwa mujibu wa taarifa za mateka mmoja aliyeachiwa na watekaji ... (watekaji) wote wanaonekana kuwa na silaha. Mabomu, ambayo ni dhahiri yanaonekana kama makopo, yaliwekwa kwenye milango ya ndege. (Uwanja wa ndege wa) Benghazi unaonekana kama ni kituo tu lakini ndege itaendelea na safari nyingine. Inaelekea ndege itapelekwa Afrika ya Kati.”
Usiku wa manane wa kuamkia Jumatatu ya Juni 28, Waziri wa Ulinzi wa Israel, Shimon Peres aliondoka kwenye uwanja wa ndege wa Tel Aviv na kuelekea ofisini kwake ghorofa ya pili ya jengo la makao makuu ya Jeshi la Israel.
Peres, ambaye alizaliwa Poland Alhamisi ya Agosti 2, 1923, alikuwa amepelekwa Palestina akiwa na umri wa miaka 11 kama mtoto aliyechaguliwa kuiwakilisha familia ya Wayahudi katika harakati za kuanzisha taifa la kuwalinda Wayahudi. Peres aliteuliwa kuwa waziri wa wizara hiyo nyeti siku 24 kabla ya utekaji huo, Juni 3, 1976.
Akiwa ofisini kwake akapata habari kuwa Ndege 139 ilikuwa imeshatua katika Uwanja wa Ndege wa Entebbe nchini Uganda. Peres alijua mambo fulani kuhusu Uganda na rais wake, Idi Amin kwa sababu kwa miaka kadhaa Israel ilikuwa ikimpatia misaada na mafunzo kwa Jeshi la Uganda, hususan jeshi la anga. Lakini kulikuwa na jambo la kushangaza zaidi. Mwaka 1903 Uganda ilipendekezwa kuwa taifa la Wayahudi na kwa sababu hiyo Uganda ingekuwa ni mbadala wa Palestina.
Akiwa ofisini kwake alianza kujadiliana na mnadhimu Mkuu wa IDF, Luteni Jenerali Mordechai Gur na washauri wa masuala ya kijasusi huku akitandaza ramani ya dunia mezani kwake na picha kadhaa.
Katika kujadiliana, Gur alimwambia Peres kuwa “kuna umbali wa zaidi ya kilomita 4,000” kati ya Israel na Uganda na kwamba katikati ya nchi hizo mbili kuna nchi nyingine hasimu wa taifa la Israel. Wakiwa katika mjadala, ofisa mwingine wa ujasusi aliingia na kuungana nao. “Magaidi wanaungwa mkono na Rais Amin,” alisema ofisa huyo.
“Una hakika?” Peres aliuliza.
“Ndiyo,” alijibu. “Sauti ya Uganda (redio) inatangaza madai yanayotolewa na watekaji, na redio inaishambulia Ufaransa na Israel. Magaidi hawa tayari wana chama chao nchini Uganda. Inaonekana mwendesha mipango wao huwa anasafiri kati ya Uganda na Somalia.”
Itaendelea kesho