Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

OPERESHENI ENTEBBE DAKIKA 90: Uganda yatangaza kuanza kuua mateka wa Israel-4

74476 Opereshenipic

Sat, 7 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kabla kikosi kazi hakijaingia kazini, maofisa walipata kumbukumbu zilizoonyesha kuwa miezi mitano kabla ya utakeji huu haujafanyika, Rais Idi Amin wa Uganda alikuwa amewapatia magaidi wa Palestina makombora ya kutungua ndege yaliyotengenezwa Urusi. Kwa kuyatumia makombora hayo walikaribia kabisa kuitungua ndege ya Shirika la Israel (El Al) Jumapili ya Januari 18, 1976.

Lakini kabla ya kufyatua makombora yao walikamatwa na maofisa usalama wa Kenya. Gari lao lilipopekuliwa lilikutwa na bunduki za kivita, bastola na mabomu ya kutupwa kwa mkono.

Kwa mujibu wa kitabu ‘90 Minutes in Entebbe’, silaha zote hizi ziliingizwa Uganda, Serikali ya Idi Amin ikijua. Wawili miongoni mwa waliokamatwa walihusika katika shambulio la bomu katika ndege ya shirika la ndege la Israel (El Al) kwenye uwanja wa ndege wa Orly Airport mjini Paris Januari 1975. Desemba ya mwaka huo, watatu hao waliwasili Nairobi kama watalii wakiwa na visa walizopata katika ubalozi wa Uingereza mjini Beirut, Lebanon.

Januari 21 ‘wasamaria’ wawili, mwanamke na mwanamume wakiwa wanazungumza Kijerumani waliwasili Nairobi kuchunguza kilichowapata wenzao. Ilipobainika kuwa ni wagaidi, walikamatwa na kuhojiwa.

Walipopekuliwa, mwanamke alionekana kwenye tumbo lake pameandikwa maelekezo ya kuishambulia ndege ya El Al. Jumatatu ya Februari 3, 1975 Rais Jomo Kenyatta wa Kenya aliwakabidhi watu hao kwa siri wahojiwe na wanausalama wa Israel. Siri hiyo ilipofichuka baadaye, magaidi wakasema watalipiza kisasi kwa Wakenya mahali popote duniani kama hawatawaachia wenzao watano wanaoshikiliwa Kenya.

Mjini Tel Aviv, baada ya majadiliano marefu ya kikao chao cha jioni, Brigedia Jenerali Dan Shomron, ambaye baadaye alikuja kuwa kiongozi wa mpango mzima wa kuwakomboa mateka nchini Uganda, alisimama na kusema “vyovyote itakavyokuwa, na kwa gharama zozote, lazima twende Entebbe. Kama hatutakwenda itakuwa laana kwa vizazi vyote vijavyo. Tusipokwenda sasa basi wakati mwingine watakapoteka ndege zetu watataka wachukue hadi viongozi wetu, au watatutaka tuondoke Ukingo wa Magharibi.”

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Mpango wote wa kuivamia Entebbe ulianzishwa na Brigedia Jenerali Shomron. Kwa mujibu wa kitabu ‘Sun Tzu and the Art of Modern Warfare’ cha Mark McNeilly, Brigedia Jenerali Shomron alikuwa ni msimamizi mkuu wa mpango wote wa kuivamia Entebbe na kikosi kazi kiliundwa na Luteni Kanali Jonathan Netanyahu.

Wengi wa waliojumuishwa katika kikosi hicho ni makomandoo kutoka kitengo cha Seyeret Mat’kal cha Jeshi la Israel. Wakati baadhi ya wenzake wakimshangaa aliposema lazima waende Entebbe kuokoa mateka, Brigedia Jenerali Shomron naye aliwashangaa, akisema “Kama Serikali inataka—tunaweza kwenda popote duniani.”

Shomron alizaliwa Ijumaa ya Agosti 5, 1937 nchini Israel. Vita yake ya kwanza kupigana ilikuwa ni ile kampeni ya Israel dhidi ya wale iliowaita magaidi katika Sinai mwaka 1956 na nyingine ni ile iliyojulikana zaidi kama ‘vita iliyodumu kwa siku sita’ mwaka 1967.

Nchini Uganda watekaji waliweka Alhamisi ya Julai Mosi, 1976 kuwa ndiyo siku ya mwisho, kwamba ikiwa Israel haitawaachia magaidi waliowashikilia nchini Israel na katika nchi nyingine, basi mateka wote watauawa.

Katika jiji la Tel Aviv, ndugu, jamaa na marafiki wa mateka waliposikia ikifika Alhamisi ndugu zao waliotekwa wangeuawa, walilazimika kwenda ofisini kwa Waziri Mkuu Rabin kumlilia atekeleze madai ya watekaji kwa ajili ya usalama wa ndugu zao. Ili kuendelea kuwazubaisha watekaji, Serikali ya Israel wakasema wanaanzisha mazungumzo kati yake na watekaji ili wafikie muafaka wa namna bora zaidi ya kushughulikia jambo hilo. Hata hivyo walijua kuwa Rais Idi Amin, kwa vile alikuwa ni mwenyekiti wa OAU, angeondoka nchini kwake kwenda kwenye mkutano wa Nchi Huru za Afrika (OAU) uliopangwa kufanyika Mauritius.

Idi Amin alikuwa akiwatembelea mateka hao mara kwa mara na kuzungumza nao. Wakati mwingine aliwaambia wasiwe na wasiwasi kwa sababu watakuwa salama ikiwa tu serikali yao yaani Israel itakubaliana na matakwa ya watekaji.

Kwa kujua kuwa Idi Amin alikuwa akishirikiana na watekaji, Waziri wa Ulinzi wa Israel, Shimon Peres, akaanza kuona ulazima wa kutumia nguvu za kijeshi. Akajikuta anakubaliana na Brigedia Jenerali Dan Shomron kwamba ni lazima Uganda ivamiwe kijeshi kuokoa mateka wa Kiyahudi.

“Kama Israel haitaivamia Uganda,” akasema Peres, “Nina wasiwasi janga kubwa sana litaikumba nchi hii. Na tunapojadili maisha ya waliotekwa nyara na hatari iliyoko kwa maisha yao, nataka mjue kuwa nawaona wao kama wanajeshi wa Israel wakiwa vitani.”

Kwa Israel kuivamia Uganda kulihitaji pia idhini ya bunge la Israel. Lakini taarifa kutoka Uganda zikasema kuwa siku iliyofuata mateka wangeanza kuuawa na kwamba wangeanza na mateka mmoja baada ya mwingine.

Taarifa nyingine zilizofikia meza za kijasusi za Israel zilisema Rais Idi Amin angeondoka Jumamosi ya Julai 3 kwenda kuhudhuria mkutano wa OAU uliopangwa kufanyika Mauritius.

Maandalizi ya kuivamia Uganda kijeshi yalianza na yakapata kasi zaidi usiku wa Ijumaa, yaani usiku mmoja kabla ya uvamizi wa kijeshi. Kwa kuwa Waisraeli ndio waliokuwa wakilipatia mafunzo jeshi la anga la Uganda, hawakupata shida kukusanya taarifa za kijasusi zilizohusu uwezo wa jeshi la Idi Amin na ulinzi wake. Walijua idadi ya ndege walizokuwa nazo pamoja na silaha nyingine mbalimbali.

Waisraeli walijua pia kwamba kiasi cha wanajeshi 21,000 waliokuwa wamepata mafunzo ya kijeshi kikamilifu, nusu yao walifikiriwa kuwa walikuwa wako katikati ya Entebbe na Kampala na kwamba uwanja wa ndege wa Entebbe ulikuwa unalindwa na wanajeshi waliokuwa wakitumia zana za kijeshi zilizotengenezwa Urusi vikiwamo vifaru.

Habari zaidi za kijasusi kuhusu uwanja wa ndege wa Entebbe zilipatikana katika dakika za mwisho za maandalizi ya uvamizi.

Kuanzia hapa, mawasiliano muhimu yalifanywa kati ya ofisa usalama wa Israel na Lionel Byrn Davies, mkuu wa polisi wa Nairobi, na aliyekuwa kamanda wa Huduma Maalumu wa Jeshi la Anga la Uingereza nchini Kenya, Bruce McKenzie.

Kwa kuwasiliana na maofisa wa Serikali ya Kenya, Israel walitaka kupata jawabu la swali moja tu la msingi. Je, Kenya itaruhusu ndege za Israel kujaza mafuta mjini Nairobi?

Ndege kubwa za kijeshi ambazo wangetumia zingeweza kufika Entebbe bila kuongeza mafuta, lakini zisingeweza kurudi Israel bila kuongeza mafuta. Kulikuwa na pendekezo la kujaza mafuta kwenye ndege hizo zikiwa angani, lakini lilikataliwa kwa sababu lilionekana kuwa ni hatari zaidi ikizingatiwa ndege zingepita juu ya anga za maadui wa Israel. Je, nini kiliendelea baada ya hapo?

Usikose kesho kujua nini kitaendelea.

Columnist: mwananchi.co.tz