Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

OPERESHENI ENTEBBE DAKIKA 90: Ndege iliyobeba raia wa Israel yatekwa anga la Ugiriki na kupelekwa Uganda-1

73972 Opereshen+pic

Tue, 3 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Saa 12:45 asubuhi ya Jumapili Juni 27, 1976 ndege ya Shirika la Ndege ya Singapore 763 ilitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Athens, Ugiriki, ikitokea Bahrain kupitia Kuwait.

Miongoni mwa abiria watano walioshuka kwenye ndege hiyo, wanne walielekea eneo ambalo abiria wa ndege ya Shirika la Ndege ya Ufaransa, Flight 139, wangeondokea kwenda Paris, Ufaransa.

Saa 2:59 asubuhi hiyo, ndege ya Shirika la Ndege ya Ufaransa, Flight 139 ikirushwa na Kapteni Michel Bacos ilipaa kutoka Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion mjini Tel Aviv katika kile kilichopangwa kuwa ingekuwa ni safari ya kwenda Ufaransa kupitia Athens.

Wakati ndege hiyo Flight 139, ikitua Athens, abiria 58 waliokuwa wakiisubiri walikuwa katika hatua za mwisho za kukamilisha taratibu za uwanjani hapo.

Kwa mujibu wa Louis Williams katika kitabu chake, ‘The Israel Defense Forces: A People’s Army’, miongoni mwa abiria hao alikuwa msichana mmoja mwenye umri wa miaka 25 mwenye hati ya kusafiria ya Ecuardor. Jina lake ni Ortega na nyuma yake kwa mbali kidogo alikuwa kijana aliyekuwa na hati ya kusafiria ya Peru iliyoonyesha jina lake ni Garcia. Nyuma zaidi walikuwako wanaume wengine wawili waliokuwa na hati za kusafiria za Bahrain na Kuwait.

Flight 139 ilitua katika Uwanja wa Athens saa 5:30 asubuhi kuwabeba abiria hao 58. Wote wanne walipanda Flight 139. Saa 6:20 mchana ndege ikawa imepaa tena angani kuelekea Paris, Ufaransa, ikiwa na jumla ya abiria 246.

Pia Soma

Advertisement   ?
Baadaye, baada ya uchunguzi wa kina, ilikuja kujulikana kuwa jina halisi la mwanamke huyo ni Gabriele Kjoche-Tiedemann, ambaye aliwahi kushiriki kuwateka mawaziri wa nchi zinazochimba mafuta (Opec) katika makao yao makuu mjini Vienna, Austria katika tukio la Jumapili ya Desemba 21, 1975.

Gabriele aliwahi kuishi na aliyedaiwa kuwa ni gaidi maarufu zaidi aliyeitwa Carlos ‘The Jackal’ na mshirika wake katika hii ndege ya Ufaransa ni mwanachama wa kikundi cha kigaidi kilichojulikana kama Baader-Meinhof.

Mmoja wa Waarabu wawili waliokuwa na Ortega na Garcia baadaye walikuja kutambuliwa kama mwanzilishi na mpango mikakati wa kikundi cha Harakati za Ukombozi wa Palestina (PFLP).

Dakika nane tu baada ya kupaa angani, Ortega na Garcia na washirika wao wa Kiarabu wakaanza kile ambacho baadaye kimekuja kubaki katika vitabu vya historia duniani. Dakika nane tangu ndege kupaa, Ortega alikimbia kwa kasi kutoka kiti alichokaa hadi mbele huku akipiga kelele za kuwaamuru abiria waweke mikono kichwani. Dakika mbili baadaye mwanamama huyo Ortega akawaambia abiria kuwa wameiteka ndege hiyo na kwamba waliohusika na utekaji huo ni kundi la “Che Guevara” na kikundi cha “Gaza Unit” cha Harakati za Ukombozi wa Palestina.

Mawasiliano na ndege hiyo yalipotea muda mfupi baada ya kupaa angani kuelekea Ufaransa. Kitendo cha mawasiliano kupotea kilianzisha operesheni ya juma nzima lililoanza siku hiyo ya kutoweka kwa ndege hiyo-Jumapili ya Juni 27 hadi Jumapili ya Julai 4, 1967-iliyowahusisha makomandoo wa Jeshi la Israel (IDF). Operesheni hiyo iliitwa Thunderbolt na iliendeshwa kwa usiri mkubwa hadi pale ilipofanikiwa.

Kutoweka kwa ndege hiyo kuliingiza kazini Idara ya Ujasusi ya Israel. Kupotea kwa Myahudi yeyote ni jambo linalopewa umuhimu mkubwa sana kwa wao. Vitengo katika ujasusi wa Israel vilipoanza kufanya kazi, walipokea ujumbe mmoja uliosema:

“‘Ndege 139’ yenye idadi kubwa ya abiria ambao ni raia wa Israel ni ama imeanguka au imetekwa.” Ujumbe wa pili ukasema: “Ndege iliyopotea ni ndege ya Shirika la Ndege la Ufaransa, ambayo imetoka Uwanja wa Ndege wa Ben-Gurion (karibu na Tel Aviv) muda mfupi kabla ya saa tisa alasiri ...”

Ujumbe huo ulipelekwa kwenye Bunge la Israel ambalo lilikuwa katika kikao chake cha Jumapili. Waziri wa Usafiri ambaye alikuwa mchumi, Gad Yaakobi (41), aliupokea ujumbe huo na kuupeleka kwa waziri mkuu wake, Yitzhak Rabin. Muda ulikuwa ni saa 7:30 mchana, ikiwa ni dakika chache tu baada ya Ndege 139 kupoteza mawasiliano baada ya kupaa kutoka Athens.

Rabin, ambaye alikuwa jenerali mstaafu wa jeshi la Israel alimwambia Yaakobi: “Kama ndege itakuwa imetekwa, hakikisha unashughulikia habari zote zinazoihusu.” Hapo Gad Yaakobi akagundua mara moja kuwa amekabidhiwa jukumu la kushughulikia suala la kupotea kwa ndege hiyo—iwe ni kwa utekaji au kuanguka.

Baada ya dakika chache, taarifa zaidi kuhusu ndege hiyo zikaanza kumiminika. Ingawa huo ulikuwa ni muda wa kupata chakula cha mchana, njaa waliyokuwa nayo maofisa wa Serikali ya Israel ilitoweka. Badala ya kwenda kupata mlo, walianza kukusanya habari zozote kuhusu ndege hiyo.

“Airbus (ndege) iliyopotea imeondoka hapa (Tel Aviv) na abiria 245 na wafanyakazi 12,” waliripoti maofisa usalama wa Uwanja wa Ndege wa Ben-Gurion mjini Tel Aviv ambao walikuwa wakipitia mafaili yote yanayohusu safari ya ndege hiyo.

“Tunaamini kulikuwa na Waisraeli 83—lakini labda walikuwako wengi zaidi kwa sababu baadhi ya abiria wana uraia katika nchi nyingine ... idadi isiyojulikana ya Waarabu wanaaminika kuwa walihamishiwa kutoka Shirika la Ndege la Singapore ambayo iliingia Athens muda mfupi kabla ya ndege Flight 139 (kutua na kupaa)…” anaandika Brigadier J. Nazareth katika kitabu chake, ‘Creative Thinking in Warfare’.

Timu ya kushughulikia tatizo hilo ikaundwa saa 9:30 alasiri—ikiwa ni saa mbili kabla ya taarifa za kijasusi kuanza kumiminika na robo saa tu kabla ya kuvunjika kwa kikao cha bunge la nchi hiyo. Waliojumuishwa katika timu hiyo ni pamoja na waziri mkuu na mawaziri wengine watano wa baraza lake. Miongoni mwao alikuwamo pia mnadhimu mkuu wa IDF, Luteni Jenerali Mordechai “Motta” Gur, ambaye alikuwa akisifiwa sana kama “mwanajeshi mahiri”.

Kila mjumbe wa timu hii alikuwa na wataalamu wake waliobobea katika nyanja mbalimbali za kigaidi, kijeshi, kisiasa, kidiplomasia na kijamii. Walikutana kwa haraka kwa ajili hiyo. Kwao hili la kupotea kwa ndege yenye Wayahudi lilikuwa jambo la udharura wa hali ya juu sana. Hadi muda huu hakuna hata mmoja wao aliyekuwa amejua kama ndege ilikuwa imetekwa au ilikuwa imepata ajali.

“Nina wasiwasi ndege imetekwa,” Waziri Mkuu Rabin alimwambia mshauri wa kisayansi wa ulinzi wa Israel, Dk Yehezkel Dror (baadaye alikuja kuwa profesa). “Tukabiliane na ukweli halisi wa jambo hili.”

Wakati wakijadiliana hilo, ndege 139 ilikuwa bado angani ikielekea kusini badala ya kaskazini kuelekea Paris kama ilivyokuwa imepangwa.

Fuatilia nini kilitokea kesho

Columnist: mwananchi.co.tz