Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

OPERESHENI ENTEBBE DAKIKA 90: Makomandoo wa Israel wafanya mazoezi ya mwisho kushambulia-5

74635 Opereshenipic

Sat, 7 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katika toleo lililopita tuliona jinsi Waisraeli walivyoanza kufanya mawasiliano na maofisa wa Serikali ya Kenya kuona uwezekano wa ndege zao za kivita kutua mjini Nairobi kwa ajili ya kujaza mafuta. Ofisa wa kwanza kabisa wa Serikali ya Kenya kufikiwa alikuwa mkuu wa polisi wa Nairobi, Lionel Byrn Davies na aliyekuwa kamanda wa Huduma Maalumu wa Jeshi la Anga la Uingereza nchini Kenya, Bruce McKenzie. Kwa kuwasiliana na maofisa wa Serikali ya Kenya, Israel walitaka kupata jibu la swali moja tu la msingi. Je, Kenya itaruhusu ndege za Israel kujaza mafuta mjini Nairobi? Waisraeli walifikia hatua hiyo kwa kuwa ndege kubwa za kijeshi ambazo wangetumia zingeweza kufika Entebbe bila kuongeza mafuta, lakini zisingeweza kurudi Israel bila kuongeza mafuta. Je, nini kiliendelea baada ya hapo? Sasa endelea.

Maofisa wa usalama wa Jeshi la Israel waliwasiliana pia na kamanda wa kikosi cha kukabiliana na fujo nchini Kenya (GSU), Geoffrey Karithii, ambaye alisema Rais wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta hangekuwa na tatizo. Walipomfikia mwanasheria mkuu wa Kenya, Charles Njojo walimshawishi naye akakubali na akasema atatoa hata ushauri wa kisheria kuhakikisha Israel haivunji sheria yoyote inayohusu masuala ya anga.

Raia mmoja wa Uganda ambaye alikuwa ni wakala wa shirika la ujasusi la Israel (Mossad) alituma taarifa za dakika za mwisho za hali ya ulinzi ya uwanja wa ndege wa Entebbe. Taarifa zilizowafikia majasusi wa Israel zilisema ulinzi katika uwanja huo ulikuwa umeongezwa kuliko ilivyokuwa kabla ya utekaji huo.

Wengine ambao walitumiwa na ujasusi wa Israel bila wao wenyewe kutambua ni pamoja na waandishi wa habari nchini Kenya. Miongoni mwao ni aliyekuwa mhariri mkuu wa gazeti la Daily Nation la Kenya, George Githii. Waliamtumia Githii kwa sababu kwa wakati huo alikuwa mshauri wa karibu sana wa Rais wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta.

Mapema Jumamosi ya Julai 3, 1976—siku moja kabla ya Entebbe kushambuliwa—jasusi mmoja wa Israel aliondoka Tel Aviv kuelekea Nairobi baada ya mazungumzo yake ya simu na baadhi ya maofisa wa serikali ya Kenya. Dakika chache kabla ya kuondoka Tel Aviv alimpigia meneja wa Shirika la Ndege la Israel (El Al) wa Nairobi na kumwagiza aandae kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kazi maalumu. Bila hata kuulizwa mtu wa El Al aliyekuwa Nairobi alitafuta umbali wa kutoka Nairobi hadi Entebbe. Aligundua kulikuwa na umbali wa maili 380.

Wakati hayo yakiendelea, mazoezi ya kuishambulia Uganda yalikuwa yanafanyika nchini Israel kiasi kwamba walianza kupeana matumaini makubwa ya kufika Uganda, kushambulia, kuokoa mateka na kuondoka nao—yote hayo yakiwa ni ndani ya saa moja tu.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
“Labda tutatumia dakika 55 tu,” alisema mnadhimu mkuu wa Jeshi la Israel, Luteni Jenerali Mordechai “Motta” Gur. Kulingana na kitabu ‘The Israeli Secret Services and the Struggle Against Terrorism’ cha Ami Pedahzur, timu nzima ya uvamizi wa Entebbe ilihakikisha kila kitu kimekamilika kabla ya kazi kuanza. Nia yao ilikuwa ni kuhakikisha kuwa wanawakomboa mateka ndani ya muda mfupi sana kadiri inavyowezekana.

Ingawa walikuwa wanapeana matumaini makubwa, bado Luteni Jenerali Gur hakuwa ameridhika vya kutosha. Alilazimika kuisoma jiografia ya Entebbe kwa makini zaidi kuliko awali. Alihakiki tena taarifa za kijasusi kutoka Entebbe zilizoonyesha hali ya ulinzi katika uwanja huo. Alihakiki pia kama wale mateka hawakuwa wamehamishiwa eneo jingine kuhifadhiwa. Baada ya hapo kungekuwa na makomandoo ambao kazi yao kubwa ni kuwahamisha mateka kwa haraka na kuwakimbiza kwenye ndege wakati kikosi kingine kikiimarisha ulinzi na wengine wakishambulia.

Baadaye Luteni Jenerali Gur alikaririwa na kitabu ‘Creative Thinking in Warfare’ cha Brigedia J Nazareth akisema: “Kilichonifurahisha ni kwamba hakuna hata mmoja kwenye timu ya uokozi aliyofikiri kuwa mkakati wetu utashindikana. Waliwahi kufanya operesheni nyingi za mfano wa uvamizi wa Entebbe. Walikuwa wamefunzwa na wameshapigana sana vitani kiasi kwamba kazi hii ni jambo la kawaida kwao. Hawakuwahi kupuuza magumu na hatari yoyote. Walikabiliana na hatari yoyote kwa weledi wa hali ya juu sana kama madaktari bingwa wanavyokutana na mgonjwa wa upasuaji. Mpasuaji anajua la kufanya anapofanya upasuaji, lakini anakuwa amejiandaa kwa lolote lisilotazamiwa linaloweza kutokea wakati wa kufanya upasuaji huo. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa wanaume hawa (makomandoo wa Israel).”

Luteni Jenerali Gur aliwaasa makomandoo hao waifanye kazi ya uvamizi wa Entebbe kwa namna ileile ambayo daktari bingwa anavyofanya upasuaji. Aliwaasa kuwa ikiwezekana waepuke kumwaga damu katika operesheni hiyo kwa kadiri wanavyoweza kuepuka na kwamba watilie maanani umuhimu wa operesheni hiyo.

Aliwaambia kuwa nia ya operesheni hiyo si tu kuwaokoa mateka bali pia ni kutuma ujumbe duniani kuwa Wayahudi wasitishwe au kunyanyaswa mahali popote walipo duniani na kwamba ujumbe huo uwe dhahiri kwa wote kwamba Wayahudi hawatakiwi kuwaogopa maadui zao.

Taarifa za kijasusi kutoka Shirika la Kijasusi la Uingereza, MI6 (Military Intelligence 6) zilizokusanywa na wapelelezi wao katika nchi za Afrika Mashariki zilizopatikana jioni Jumamosi ya Julai 3 zilidai kuwa Idi Amin alikuwa anarejea kutoka kwenye mkutano wa wakuu wa nchi huru za Afrika (OAU) uliokuwa unafanyika Mauritius na kwamba mateka wangeanza kuuawa mmoja mmoja kuanzia asubuhi ya siku inayofuata Jumapili ya Julai 4.

Taarifa hizo zilifanya ule uharaka wa kuivamia Uganda kupewa umuhimu mkubwa zaidi. Makomandoo walikadiria kuwa katika operesheni hiyo wanajeshi wa Israel wangeweza kuuawa kati ya 30 na 35. Hata hivyo, Luteni Jenerali Gur aliona kuwa ikiwa itatokea hivyo, ni heri zaidi kupoteza watu 35 kuliko Wayahudi 105 waliokuwa wanashikiliwa mateka mjini Entebbe.

“Usiri, kasi, na kushtukiza” ni maneno yaliyotumiwa zaidi mkuu wa operesheni hiyo ya kijeshi, Brigedia Jenerali Dan Shomron. Kwa njia hiyo, Jumamosi ilionekana kama siku ya kawaida sawasawa na Jumamosi nyingine zote.

Makomandoo ambao wangeifanya kazi hii walichaguliwa kutoka kwenye Brigedi ya Golani. Walichukuliwa pia wasichana wa jeshi la anga la Israel ambao kazi yao kubwa ingekuwa ni kuwatibu majeruhi ambao wangetokana na operesheni hiyo.

Luteni Kanali Yehonatan “Yonni” Netanyahu (wengine walimwita Yonatan Netanyahu) ambaye ni kaka yake Waziri Mkuu wa sasa wa Israel, Benjamin Netanyahu, alipewa jukumu la kuongoza kikosi cha makomandoo wa kushambulia.

Yonni aliwakusanya makomandoo wa kikosi chake na kuanza kuijadili Uganda kwa kina. Ingawa walishafanya mashambulizi mengi, hili la kuishambulia Uganda na kuwaokoa mateka lilikuwa jipya kwao.

Taarifa nyingine za kijasusi ziliendelea kumiminika mjini Tel Aviv. Mshauri wa kukabiliana na ugaidi, Meja Jenerali Rehavam Zeevi, alikuwa akihangaika kupata habari zozote kuhusu Uganda. Saa 8:30 mchana wa Jumamosi ya Julai 3, ikiwa ni saa moja kabla ya kuanza kwa operesheni ya kuivamia Uganda, Zeevi alimpigia simu Waziri Mkuu Rabin kuwa bado Idi Amin hajawasili Uganda kama ilivyokuwa imetarajiwa awali na kwamba angewasili baadaye siku hiyo na siku inayofuata mauaji ya mateka yangeanza.

Itaendelea kesho

Columnist: mwananchi.co.tz