Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

OPERESHENI ENTEBBE DAKIKA 90: Kumekucha, vikosi vya Israel vyaingia kazini-3

74323 OPERESHENI+PIC

Thu, 5 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mipango ya kuivamia Uganda na kuwakomboa mateka wa Ndege Flight 139 ikaanza kusukwa kwa makini ofisini kwa waziri wa Ulinzi wa Israel, Shimon Peres. Katika ramani waliangalia uwezekano wa kuruka kutoka Tel Aviv, waingie Uganda, wafanye shambulizi la kushtukiza na kisha warejee Tel Aviv. Kwa kufanya hivyo ndege ambazo wangetumia zisingeweza kusafiri umbali wa kilometa 8,000 bila kujaza mafuta, kwa hiyo jambo moja muhimu lilikuwa ni nchi ambayo ingewaruhusu watue, wajaze mafuta na kuondoka.

Katika ramani waliiona Djibout. Mara moja Peres alimpigia simu waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Yigal Allon na kumwambia azungumze na Serikali ya Ufaransa ili wazungumze na Djibout kuhusu ndege za Israel kujaza mafuta nchini humo.

Wakati Peres anazungumza na Allon, Jenerali Gur alikuwa kwenye simu nyingine akizungumza na makomandoo wa jeshi la Israel. Alitoa maelekezo kuwa kitengo maalumu cha makomandoo katika Uwanja wa Ndege wa Ben-Gurion Airport kiwekwe katika hali ya dharura na wawe tayari kwa lolote.

Wakiwa katika mipango hiyo huku wakiwa wamefungulia redio zao kunasa matangazo ya redio kutoka Uganda, mara ikasikika redio ya Uganda, Sauti ya Uganda. Mtangazaji alisikika akisema Uganda inaishutumu Ufaransa kwa kuikalia Djibout. Kana kwamba waandaaji wa taarifa hiyo walijua mipango ya Israel kuwatumia Wafaransa ili wakatue Djibout kujaza mafuta, sauti hiyo ikasema: “Djibout inakaliwa na Ufaransa na hiyo imekuwa ndiyo njia pekee kwa Israel kwenda Afrika na Mashariki ya Mbali,” ilitangaza redio hiyo.

Jioni ya Jumatatu, Juni 28, yaani siku moja baada ya ndege kutekwa, kikosi kazi kilianza maandalizi ya mpango wa kuivamia Uganda. Kikosi kilianza kupitia nyaraka mbalimbali. Muda mfupi baadaye kikosi kikagundua kuwa aliyeandaa mpango wa utekaji huo ni Dk Wadi Hadad aliyekuwa na umri wa miaka 46. Kabla ya hapo alikuwa ameshaandaa utekaji mbalimbali. Avery Plaw katika kitabu chake, ‘Targeting Terrorists: A License to Kill?’ ameandika kuwa huu utekaji wa Ndege 139, Dk Hadad aliupa jina la Operesheni Uganda.

Katika kulitekeleza hilo la Operesheni Uganda, Hadad alihamia Somalia kwa muda na kuwapanga watekaji wake, akawapa mafunzo na kisha wakaenda Athens. Miongoni mwa watekaji hao alikuwamo mwanamke mmoja wa Ujerumani na mwanamume mmoja pia wa Ujerumani aliyejulikana kwa jina la Wil-fried Bose na alijulikana zaidi kutokana na ushirika wake na aliyekuwa gaidi maarufu, ‘The Jackal’ Carlos Ramirez. Kiongozi wa timu ya watekaji hao ni Fayez Abdul-Rahim Jaber, aliyezaliwa Hebron, Palestina mwaka 1930 na ambaye kwa muda mrefu alikuwa mkazi wa Cairo aliyejihusisha sana na vikundi vya kigaidi.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Katika ukurasa wa 204 wa kitabu ‘Brothers in Blood: The International Terrorist Network’ mwandishi Ovid Demaris ameandika kuwa huyu Jaber aliandaa shambulio la bomu katika ndege ya shirika la ndege la Pan-Am mjini Rome, Italia Jumatatu ya Desemba 17, 1973 ambako watu 31 waliuawa.

Usiku wa manane wa Jumatatu ya Juni 28 kuamkia Jumanne ya Juni 29, 1976, Rais wa Uganda, Idi Amin na mlinzi wake walionekana katika picha ya pamoja na wanamgambo wa Palestina waliokuwa wamevaa sare za kijeshi. Redio ya Uganda ilimtangaza Idi Amin kama “msuluhishi” kati ya watekaji na taifa la Israel.

Kwa mujibu wa mwandishi Ovid Demaris, usiku huo waziri mkuu wa Israel hakuwa na amani moyoni. Swali kuu alilokuwa anajiuliza ni “kwa nini Israel?” Ukweli mchungu kuhusu utekaji huo waliupata kutoka kwa yule dada wa Uingereza aliyeachiwa huru katika uwanja wa ndege wa Benghazi, Libya. Dada huyo, Patricia Heyman, aliwaeleza Scotland Yard kuhusu “kutengwa” kulikokuwa kunafanyika. Mateka Wayahuhdi walikuwa wanatengwa na mateka wengine, hususan Wajerumani. Na walikuwa wakitengwa kwa kunyooshewa bastola ndani ya ndege.

Taarifa kutoka Uganda zilizokuwa zikivifikia vitengo vya usalama vya Israel, zilisema Rais Amin alikuwa akiwatembelea mateka hao na kuwaambia kuwa anawalinda.

Majasusi wa Israel walianza kumchezea Idi Amin. Komandoo mmoja alijifanya ni muuza duka katika kitongoji kimoja cha Jiji la Tel Aviv. Akiwa katika kitongoji hicho alipiga simu mjini Kampala, Uganda.

Nia ilikuwa ni kumpata Idi Amin ili aongee naye, ammwagie sifa na kumpongeza kwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) na kwamba kwenye mkutano wa OAU uliopangwa kufanyika Mauritius wakati huo yeye (Amin) angeonekana ‘nyota wa mchezo’.

Idi Amin alikuwa mwenyekiti wa OAU tangu Jumatatu ya Julai 28, 1975 hadi Ijumaa ya Julai 2, 1976. ‘Muuza duka’ huyo alikuwa ni Kanali Baruch Bar-Lev, “Borka,” ambaye alikuwa ni mkuu wa misheni ya Jeshi la Israel nchini Uganda.

Wakati akiwa Uganda, Borka alikuwa rafiki kipenzi sana wa Idi Amin na walifahamiana sana, pia huyo Borka ndiye aliyefanya mipango na kumsaidia Idi Amin kumpindua aliyekuwa Rais wa Uganda, Milton Obote, Januari 25, 1971.

Borka alianza kumpigia Idi Amin simu za mfululizo wakati kikosi kazi cha kuivamia Entebbe kikijipanga.

Maofisa wa Israel walikuwa wakifanya kazi kwa kasi wakijua kuwa kuna abiria kiasi cha 250 na wafanyakazi 12 wa ndege iliyotekwa ambao wangeweza kufikwa na lolote nchini Uganda kwa kuwa walijua Amin ni mtu hatari.

Ilipofika Jumanne, Juni 29, redio Uganda, Sauti ya Uganda, ilitangaza kuwa watekaji wamedai kuachiwa kwa Wapalestina 53 waliotuhumiwa kwa ugaidi.

Ilidaiwa kuwa 40 miongoni mwa hao walikuwa wanashikiliwa nchini Israel, sita (6) Ujerumani Magharibi, watano nchini Kenya, mmoja Uswisi na mwingine mmoja nchini Ufaransa.

Wakati matangazo hayo yakiendelea, kikosi kazi cha Israel kikapata habari kuwa mateka 47 wasio Wayahudi wameachiwa huru. Hatua hii iliwafanya Waisrael kuungana zaidi kwenye jambo hilo kuliko mwanzo kwa sababu sasa walikuwa na uhakika kuwa waliolengwa ni Wayahudi.

Baada ya abiria 47 kuachiwa na watekaji na kuwasili jijini Paris, Ufaransa usiku wa Jumatano ya Juni 30, walitoa taarifa za hatari waliyoiona Entebbe.

Awali ilionekana kana kwamba Rais Idi Amin alikuwa msuluhishi lakini maelezo ya hao abiria walioachiwa yalionyesha picha tofauti. Habari hizi zilipofika Israeli ndipo ilipoonekana kuwa Idi Amin alikuwa akishirikiana na watekaji.

Itaendelea kesho….

Columnist: mwananchi.co.tz