Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

OPERESHENI ENTEBBE DAKIKA 90: Dora Bloch atolewa hospitali, auawa-15

76045 Operesheni+pic

Tue, 17 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Saa tisa usiku wa kuamkia Julai 4, 1976 wakati ndege nne za Jeshi la Anga la Israel (IAF) zikirejea Israel na mateka waliokombolewa kutoka Entebbe, huku zikiwa zimebakiza kiasi cha saa tatu kufika Israel, tena zikiwa juu ya anga la mahasimu wao ambako zingeweza kushambuliwa na ndege za Misri au Saudi Arabia, rubani mmoja wa ndege moja ya kijeshi alisikia Redio ya Mtandao wa Kijeshi wa Israel ikitangaza: “IDF (Jeshi la Israel) usiku huu limewaokoa mateka waliokuwa wanashikiliwa Entebbe.”

Wakikasirishwa na tangazo hilo, wanajeshi wa Israel waliokuwa katika ndege hizo angani walishangazwa na tangazo hilo wakaanza kuhojiana kwa nini litolewe kabla hata ndege hazijatua nyumbani Israel. Lakini hata hivyo taarifa za mashambulio ya Entebbe ya usiku huo yalikuwa yanaripotiwa pia na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na Shirika la Utangazaji la Ufaransa (AFP)

Ndege hizo zilipofika kwenye Rasi ya Sinai zililakiwa na ndege ya IAF aina ya ‘F-4 Phantoms’ ambayo ilizisindikiza. Ndege hizo zilitua kwenye uwanja wa ndege wa kijeshi karibu na Tel Aviv saa 3:30 asubuhi.

Mateka mmoja, Dora Bloch (75), ambaye alichukuliwa kwenye uwanja wa ndege wa Entebbe baada ya kukabwa na chakula alikuwa akitibiwa katika Wodi 6B ya Hospitali ya Mulago mjini Kampala.

Aliyekuwa akimtembelea hospitalini hapo ni aliyekuwa Waziri wa Afrya wa Uganda, Henry Kyemba. Miaka 11 baadaye, 1987, Kyemba aliiambia Tume ya Haki za Binadamu nchini Uganda kwamba Dora Bloch aliburutwa kutoka kitanda cha hospitali kwa amri ya Rais wa Uganda, Idi Amin.

Baada ya Kyemba kuondoka, huku nyuma muda wa saa 12 jioni ofisa Mwingereza kutoka Ubalozi wa Uingereza mjini Kampala, Peter Chandley, alimtembelea Dora. Walipoonana, Dora alimwomba Chadley amtafutie chakula kwa sababu alikuwa na njaa. Chandley aliondoka hospitalini hapo kwenda nyumbani kwake kumwandalia chakula alichoombwa. Lakini mara tu baada ya kuondoka, nyuma askari wa siri wa Idi Amin wakaingia hospitalini hapo.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Wanaume wawili waliokuwa wamevaa nguo za kiraia, wakiwa wamebeba bastola walifika hospitalini hapo na kumchukua mama huyo kutoka kitandani alipokuwa amelazwa na kumburuza huku akipiga kelele za kuomba msaada.

Wagonjwa, wafanyakazi wa hospitali na wageni waliotembelea wagonjwa hospitalini hapo walikusanyika kwenye mlango wa wodi hiyo kuangalia kilichokuwa kinatokea. Wakiwa katika hali ya hofu waliwatazama wanaume hao wawili wakimburuta mwanamke huyo, huku akilia kwa sauti kubwa ya kuomba msaada.

Kulingana na Henry Kyemba, kila aliyeona kilichokuwa kinatendeka alijua kuwa Dora Bloch alikuwa anapelekwa kuuawa, lakini hawakuweza kufanya lolote. Walitambua wazi kuwa kuingilia hali hiyo ni kujitafutia kifo na isitoshe, hili halikuwa tukio la kwanza mjini Kampala. Ilikuwa ni kawaida ya kila siku.

“Tukio hilo halikuchukua zaidi ya dakika tano tangu limeanza hadi limemalizika. Ilikuwa ni saa tatu asubuhi,” anaandika Kyemba katika kitabu chake, ‘A State of Blood: The Inside Story of Idi Amin.’ Hospitalini hapo aliacha mkongojo wake aliokuwa akiutumia kutembelea, viatu, mkoba na nguo.

Walimtupa kwenye gari aina ya ‘Peugeot 504 ambalo lilikuwa ni mojawapo ya magari mawili yaliyofika hospitalini hapo yakiwa na namba za usajili za kikosi cha usalama cha Serikali ya Uganda. Polisi aliyekuwa akimlinda hospitalini hapo naye aliuawa.

Katika ukurasa wa 102 wa kitabu chake, ‘The Story of Mohamed Amin’, mwandishi Brian Tetley aliandika mahojiano kati ya aliyekuwa mpiga picha maarufu, Mohamed Amin na aliyekuwa mfungwa wa Uganda, John Sekabira, ambaye kwa mara ya kwanza kabisa alitoa habari za mauaji hayo kwa mwandishi wa Shirika la Habari la Ufaransa, John Edlin. Sekabira alidai yeye alikuwa mmoja wa walioamriwa kuuzika mwili wa Dora Bloch. Alielezea habari za lori kubwa la Jeshi la Uganda likiwa limejaa miili ya watu waliouawa. Lori hilo lilifika kwenye gereza ambalo yeye Sekabira alikuwa amefungwa.

Sekabira alimwambia Mohamed Amin kuwa lori hilo lilikuwa na kiasi cha maiti 200. Alisema: “Baada ya shambulio la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe walikuja na miili mingi ya wana-anga na wanajeshi wa majini. Ndipo siku moja mapema asubuhi walikuja wakatuambia tuandae makaburi mawili. Tuliyaandaa. Kisha jioni saa 11 walileta miili miwili, mmoja ni wa polisi ukiwa kwenye sare yake ya polisi na mwingine ni wa mwanamke mkongwe, mwanamke wa Kizungu.”

Alipoulizwa kama anadhani huyo mwanamke wa Kizungu alikuwa ndiye Dora Bloch, Sekabira alisema, “Hicho ndicho ninachofikiri ... nilipowauliza watu nao waliniambia ndivyo wanavyofikiri. Na ofisa magereza aliyeshuhudia polisi huyo akipigwa risasi alituambia huo ni mwili wa mwanamke wa Israel. Tulimuuliza (ofisa magereza) kwa nini polisi huyo aliuawa, akatujibu kuwa wakati wanausalama walipokuja na kumnyang’anya redio (ya mawasiliano) hospitalini alikokuwa anatibiwa (Dora), polisi huyo aliwataka wajitambulishe. Badala ya kujitambulisha walimuua kwa kumpiga risasi, wakaukokota mwili wake hadi kwenye gari aina ya ‘Jeep’. Waliwaleta pamoja na bado walikuwa wanapumua.”

Alipoulizwa ni majeraha gani aliyokuwa nayo Dora Bloch, Sekabira alijibu: “[Dora] alipigwa risasi ya kichwani na yule polisi alikuwa amepigwa risasi tatu.”

Siku tatu baadaye mpiga-picha wa ‘Visnews’, ambalo ni shirika la habari lenye makao yake mjini London, Uingereza, alikutana na aliyewahi kuwa mpishi wa Idi Amin aliyeitwa Moses Aloga. Kwa mujibu wa kitabu hicho, Aloga alikuwa mpishi wa Amin kwa miaka minne mfululizo ambaye naye alielezea ukatili wa Idi Amin na jinsi alivyokuwa akihifadhi viungo vya wanadamu katika majokofu yake.

Kwa mujibu wa kitabu ‘From Jerusalem to the Lion of Judah and Beyond,’ watu wawili waliomuua Dora Bloch baadaye walikuja kugundulika kuwa ni Meja Farouk Minawa ambaye alikuwa mkuu wa Polisi wa Siri wa Amin (State Research Bureau—SRB) na Kapteni Nasur Ondoga, ambaye alikuwa ni mkuu wa Itifaki wa Serikali ya Idi Amin.

Mwili huo ulizikwa kwenye shamba la miwa umbali wa kilometa 30 mashariki mwa Kampala. Mpiga-picha wa kujitegemea, Jimmy Parma, ambaye alifanikiwa kupiga picha mwili huo, aliuawa na SRB.

Mjukuu wa Dora aliyeitwa Ofer Bloch aliliambia hivi gazeti la ‘The Times of Israel’,: “Wakati Idi Amin alikuwa madarakani, hatukujaribu hata kufuata mabaki yake.”

Hata hivyo, miaka mitatu baada ya uvamizi wa Entebbe Idi Amin aliondolewa madarakani. Na hapo ndipo Jeshi la Israel lilipotuma ujumbe pamoja na mtaalamu wa magonjwa, kutambua mabaki yake, na kuyapeleka Yerusalemu kwa ajili ya mazishi ya kitaifa.

Columnist: mwananchi.co.tz