Licha ya sekta ya kilimo kuajiri zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania, bado kilimo chenyewe ni cha kujikimu, yaani ni kwa ajili ya chakula cha kaya na kupata fedha za matumizi madogo. Bado sehemu kubwa ya kilimo cha Tanzania hakijawa cha kibiashara.
Kilimo kuwa cha kibiashara haimaanishi kwamba mkulima awe ni mkubwa kwa kuwa na eneo kubwa na mazao mengi, bali inawezekana kuwa na shamba dogo linaloingiza faida.
Watu wengi wamekuwa wakitamani kuingia kwenye kilimo cha biashyara kwa kupata maelezo kwenye mitandao ya jamii, magazeti na vyanzo vingine wakisoma na kusikiliza simulizi zenye mafanikio ya wakulima wengine.
Lakini wanapoingia kwenye kilimo wanajikuta wanapata hasara. Hiyo ni kutokana na kutofanya utafiti wa kutosha kuhusu kilimo.
Yapo mambo ya kuzingatia kabla mkulima hajaingia kwenye kilimo cha biashara. Mambo haya yanahitaji muda wa kufanya utafiti ili kujiridhisha vya kutosha, vinginevyo unaweza kutumbukiza mtaji wako na kuishia kulisika bure.
Jambo la kwanza la kufikiria ni masoko ya zao unalolima.
Wataalamu wa kilimo biashara wanashauri kufanya utafiti ikiwa pamoja na kuuliza kwenye masoko ya mitaani na kwa wafanya biashara na kwa kuangalia mwenendo wa bidhaa zinazouzwa au kukubalika kwa walaji na bei zilivyo. Katika kuangalia mwenendo wa bei, kuna mazao yenye bei elekezi zinazotolewa na Serikali na hasa mazao ya biashara kama vile korosho, pamba, kahawa na chai.
Lakini mazao ya chakula (perishable) mara nyingi hutegemea upatikanaji wake. Hivyo mkulima anapaswa kuangalia ni wakati gani bei hushuka na kupanda.
Ni hatari kibiashara kwa wakulima kuvuna mazao kwa wakati mmoja, japo hutokea kwenye misimu ya mvua, kwani hapo bei hushuka na mkulima anaweza asipate faida. Lakini mkulima anaweza kutafuta mbinu ya kuhifadhi mazao hadi wakati yanapopungua sokoni.
Jambo la pili ni hali ya hewa ambapo mkulima anapaswa kutambua hali ya hewa kama vile vipindi vya jua kali, upepo, mvua za masika na mvua za vuli. Kuna mazao yanakubali wakati wa mvua nyingi na mengine hayataki mvua nyingi, mengine kwenye baridi kali, mengine kwenye joto kali. Ni vizuri pia kufuatilia taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), kila mara.