Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Njia za kuimarisha uwezo wa mtoto wa kike

50934 Pic+njia

Mon, 8 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mara kadhaa tumezungumzia umuhimu wa wazazi na jamii kuwapa watoto nafasi sawa bila kujali jinsia. Leo tunawaletea mawazo tuliyopewa na waalimu wa shule mbili za sekondari wilayani Bunda na Kahama. Waalimu hawa wametushirikisha changamoto wanazopitia wanafunzi wao wa kike na wamependekeza njia za kuimarisha uwezo wa mtoto wa kike kujiamini na kujithamini.

Mwalimu Msemakweli alitueleza kuwa siku moja baada ya kuzungumza na wanafunzi wake kwa muda aliwauliza swali, “Nani maishani mwake anatamani angezaliwa mwanaume?” Cha kusikitisha ni kwamba kati ya wasichana 76 wa kidato cha kwanza, zaidi ya nusu walinyoosha mikono.

Sababu waliyotoa ni mwanamke kutothaminiwa katika jamii. Mmoja alieleza kuwa mara nyingi ameshuhudia baba, wajomba, na hata kaka zake wakiwapiga wake zao ‘hata kwa makosa madogo ya kawaida yanayofanywa na wanaume pia’. Mwingine alisema hapendi namna wavulana wanavyomfuata kumtongoza tena kwa vitisho “kana kwamba kuna walichochangia katika mwili wangu”.

Binti mmoja alieleza namna mama yake alivyotukanwa na kupigwa makofi na manesi wakati anajifungua. Aliumia sana na kuwaza kuwa hata yeye ni mwanamke hivyo haya yote yanamngojea. Laiti angelikuwa mwanaume, angeweza epuka hili. Sababu nyingine ni nafasi ndogo wanayopewa watoto wa kike kujisomea na kupigania ndoto zao kama ilivyo kwa watoto wa kiume.

Ipo dhana potofu, wengi huamini mtoto wa kike hawezi kufanya kitu cha muhimu ukilinganisha na wa kiume ambaye hupewa kipaumbele na fursa katika nyanja zote ikiwemo elimu.

Mwalimu Theresia anapendekeza yafuatayo ili kuwasaidia watoto wa kike kuimarisha uwezo wao na kujiamini.

Mosi, ni lazima suala la elimu lipewe kipaumbele kwa mtoto wa kike. Waalimu wanatakiwa kufanya bidii ili kuleta usawa kati ya wavulana na wasichana kwenye elimu. Kuwahamasisha kupenda elimu na kumpa moyo katika masomo yake ni moja ya mbinu za kumuimarisha mtoto wa kike, kwani itamfanya ajione yuko sawa na mtoto wa kiume.

Pili, elimu ya utambuzi ni muhimu. Mtoto wa kike anatakiwa kukumbushwa kuwa yeye ni sehemu ya jamii na hivyo kazi yake si kuzaa tu. “Nasema hivyo kwa sababu baadhi ya maeneo kama Kanda ya Ziwa mwanamke alikuwa hasomeshwi, kisha akikua kazi yake ni kuolewa na kuzaa watoto. Hii si sawa, mtoto wa kike anatakiwa aelimishwe anawajibika kuijenga jamii yake kwa namna nyingi si kuzaa pekee. Anatakiwa kutambua mchango wake kwa jamii upo kiuchumi na kadhalika,” aeleza Mwalimu Theresia.

Tatu, kampeni zinaweza kusaidia wanajamii kuondokana na dhana potofu ya kuwa mtoto wa kike hana thamani sawa na mtoto wa kiume. Asasi mbalimbali za kiserikali na zisizo za kiserikali kama vile FEMINA HIP, TAMWA, TGNP zinaweza kutoa elimu kwa jamii ya thamani ya watoto wote; wa kike na wa kiume. Vilevile, wazifahamishe jamii namna ya kuripoti matukio yanayohusu unyanyasaji wa mtoto wa kike.



Columnist: mwananchi.co.tz