Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Njia rahisi ya kufanikiwa ndoto zako baada ya vyeti

46200 Pic+ndoto Njia rahisi ya kufanikiwa ndoto zako baada ya vyeti

Tue, 12 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Unafikiria kuwa mkurugenzi, kupandishwa cheo au kuwa ofisa mtendaji wa kampuni? Pengine unadhani umri na uzoefu wako mdogo ni kikwazo? Hapana siyo kweli.

Berthasia Ladislaus (33), ni binti msomi anayeweza kuwa shahidi katika hoja hiyo. Mei mwaka huu atatimiza mwaka mmoja tangu alipoteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kimataifa la watu wenye ualbino la Under The Same Sun (UTSS), akipokea mikoba ya Vicky Ntetema.

Berthasia anasema kutunukiwa vyeti vya shahada ya uzamili au uzamivu tena kwa ufaulu wa kiwango cha juu bado siyo kigezo cha mwisho kukufikisha katika mafanikio ya ndoto ulizonazo.

Katika maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Duniani, gazeti hili limefanya mahojiano na Berthasia kufahamua misingi iliyochagiza kufikia mafanikio ya kukabidhiwa jukumu la kuondoa aibu ya Tanzania katika matukio ya ukatili na unyanyapaa wa watu wenye ualbino kupitia UTSS akiwa na umri mdogo.

Berthasia: Uaminifu ni kitu cha muhimu sana katika kufikia mafanikio. Vijana wengi wa kike wanaotoka vyuoni ni ‘potential’ (wana ubora), wana ndoto kubwa katikati ya fursa nyingi ila changamoto zinazoweza kukwamisha baadhi yao kufikia ndoto zao, ni ‘altitude’ (mitazamo). Mwingine anakuwa na mtazamo wa kulalamika tu, kutoshirikiana na wengine ofisini, anataka kuonekana anajua kila kitu.

Hiyo siyo nzuri, ukitaka kufanikiwa unapaswa kushirikiana na wengine. Binti anatakiwa kujua kwamba, anahitaji kujifunza kuanzia kwa wateja na wafanyakazi wengine, lakini wengi wanakosa moyo wa uvumilivu, wanatakiwa kuwa ‘mentored’ (kupewa uangalizi) ili kujenga uvumilivu kutoka kwa watu wote walioko juu yao, chini au walio nao katika daraja moja.

Elimu ni sawa inahitajika sana, lakini jambo lingine ni ushirikiano. Hata kama unajua kitu unahitaji kusikiliza kwa mtu mwingine na hayo yote yanatakiwa kwenda sawa na bidii ya kazi.

Kwa upande wa mabinti waliosoma kozi za ukaguzi wa ndani, wanatakiwa kuhakikisha wanatambulika kisheria na bodi zinazohusika. Kufanya mitihani ya bodi, inamjengea mtu kujua sheria na taratibu za utekelezaji wa majukumu ya taaluma hiyo.

Mwandishi: Pengine unadhani ni kigezo gani kimetumika katika uteuzi wako?

Berthasia: Mkaguzi wa ndani siyo mahesabu tu, huangalia zaidi malengo ya shirika, vipaumbele vya shirika na malengo ya kila idara na uwezekano wa kufanikisha, anaangalia ripoti zinazotolewa zina ukweli gani.

Sehemu yoyote, mkaguzi mkuu wa ndani, anakuwa sawa na Mkurugenzi Mtendaji. Wote huripoti kwa ofisa mtendaji mkuu au kwa bodi.

Kwa hiyo ni rahisi kwa mkaguzi mkuu wa ndani kuelewa mwelekeo wa shirika unakwendaje, ndiyo maana inakuwa rahisi mkuu wa ‘internal audit’ (ukaguzi wa ndani) kuwa mkurugenzi kwa sababu utendaji wote anaupitia na kuufahamu. Kwa hiyo nadhani ndiyo kigezo kilichoangaliwa zaidi.

Hata hivyo, kikubwa zaidi mimi nimejengewa mazingira ya kujiamini tangu nikiwa nyumbani, watoto wa kike tulikuwa wawili tu kati ya watoto wanane. Tulijengewa uwezo wa kujiamini na wazazi kujiona wote ni sawa. Wanaume walitutia moyo. Kwenye vikao tulipewa nafasi za uongozi labda kujadili mirathi, kuzungumza hata kutoa maelekezo, ilinisaidia.

Mwandishi: Katika ofisi zote ulizofanya kazi, ilikusaidiaje kuongeza uwezo na umahiri katika nafasi za uongozi?

Berthasia: Kuanzia hatua ya mafunzo kwa vitendo, kazi ya kujitolea, kupata uzoefu NHC na Pwc, ilinisaidia kupata fursa ya kukagua makampuni mengi ya Serikali na binafsi zikiwemo NGOs, nilijifunza mifumo ya usimamizi na mahesabu ya mashirika mbalimbali.

Pia, niliona changamoto ya uwepo wa wanawake wachache mno katika uongozi, wachache hao walinivutia, nikawatumia kama wakufunzi na walezi wangu, nilipoingia UTSS nilifanya kazi ya kukagua na kushauri juu ya idara zote za shirika.

Mwandishi: Ulianza na jambo gani zito UTSS katika vita dhidi ya ukatili na unyanyapaa wa watu wenye ualbino?

Berthasia: Kwanza kabisa ifahamike kwamba, ndoto ya UTSS ni kuhakikisha watu wenye ualbino wanapata haki stahiki katika jamii, hivyo kuona siku za unyanyapaa zinafifia.

Ili wapate haki hizo inabidi tuone wakishirikishwa katika kuchagua na kuchaguliwa kuwa viongozi, kuongoza nafasi mbalimba za uongozi wa juu, katika ajira na nyanja mbalimbali zinazoendana na uwezo wao, wanapata elimu bora. Hilo ndilo lengo langu la kwanza.

Kwa kutekeleza hayo nategemea zaidi shirika, tunajikita katika kutoa elimu kote ambako tunaona kuna upungufu wa elimu kwa jamii. Mwaka huu tunajiandaa kuanza na waandishi wa habari kwa sababu wao ndiyo sehemu ya kwanza ya walimu wa jamii yetu.

Columnist: mwananchi.co.tz