Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Nimeyasikia ya Cannavaro nikamkumbuka Esther Chabruma

11738 Ibra+Bakari TanzaniaWeb

Mon, 13 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hakuna asiyefahamu hali halisi ya sasa wanayopitia Yanga kwamba haikuwahi kutokea lakini kwa jinsi na mazingira, wanabakia kuyazoea.

Baada ya kuondoka mwenyekiti wa klabu hiyo , Yusuf Manji mapema mwaka jana, Yanga imekuwa ikiyumba, Yanga haijatulia hata mara moja.

Manji aliiweka Yanga mabegani, aliisaidia, aliionyeshea njia na mwisho wa siku aliipa mafanikio ambayo Yanga itayakumbuka katika historia ya klabu hiyo.

Lakini kuna kitu kimoja hapa. Kuyumba kwa Yanga ni kama ngoma iliyoanza, na wachezaji nao wakaingia jumla na kuanza kuicheza.

Pamoja na matatizo waliyokuwa nayo, wachezaji wa Yanga hawakupaswa kuicheza ngoma ile ambayo sasa imewafikisha pabaya.

Kuna timu ya Gor Mahia ya Kenya, wana matatizo kama Yanga, lakini angalia wachezaji wake, wanacheza kwa kujtuma wakijua kuwa mbele kuna mafanikio na kweli wameyapata na sasa wanasubiri mamilioni ya CAF kwa kufuzu kuvuka hatua ya makundi.

Hata juzijuzi nilisoma habari moja ya Bakari Malima, beki wa zamani wa Yanga ambaye pia aliwahi kuichezea Simba aliweka wazi kuwa tatizo ni kwa wachezaji wenyewe hawakutaka kujiongeza na hilo limetokana na baadhi ya wanachama, wakishirikiana na viongozi wasiokuwa na mtazamo wa maendeleo na timu na pengine kushawishi mambo yanayoigharimu timu.

Jembe Ulaya aliwashambulia moja kwa moja akisema kuwa wachezaji wa Yanga wamejimaliza wenyewe, hakuna mtu wa kuwalaumu na wasipokuwa makini watazidi kujiongezea matatizo mengi kwa sababu wanachotakiwa wao ni kucheza mpira.

Tuyaache. Hayo yalikuwa ya kushtua tu, lakini hapa hoja yangu ni kuhusu hili la beki wa timu hiyo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, ambaye ametangaza kustaafu soka Yanga.

Cannavaro amestaafu soka na jana alikuwa akiagwa na timu moja ya Mawezi Market ya Daraja la Kwanza.

Nilipoisikia Mawenzi nikamkumbuka mchezaji wa Twiga Stars, Esther Chabruma. Huyu aliagwa kishujaa, ilialikwa timu ya Malawi akacheza kidogo, akavua jezi na kuaga mashabiki.

Chabruma alikuwa kipenzi cha mashabiki kwa aina ya soka yake kiasi cha kumbatiza jina la ‘Lunyamila’.

Nikamkumbuka mchezaji mwingine, Sunday Juma wa Simba, aliagwa kishujaa, alikuwepo Mecky Maxime, Shaaban Nditi walipoachana na timu ya taifa, nikamkumbuka Fred Mbuna waliagwa kishujaa na timu walizocheza nazo zilikuwa zinaeleweka, siwadharau Mawezi Market, lakini si kwa Cannavaro kuagiwa huko vichochoroni.

Mchezaji ameitumikia Yanga muda mrefu, alikuwa nahodha wake na pia kwa timu ya Taifa Stars na Zanzibar Stars kwa wakati mmoja, leo hii anaagwa kwa namna hiyo. Hapa kiukweli Yanga hawakumtendea haki.

Cannavaro ameichezea Yanga kwa nidhamu, alikuwa akipambana kwa nguvu zote, aliumizwa sana Yanga ikifungwa, alikuwa kiongozi bora uwanjani, hakutaka kuona vitendo vya kihuni kupiga waamuzi vikifanyika na kuipa Yanga ubingwa zaidi ya mara tano. Sioni wapi Yanga wamepatia kumuaga Cannavaro kwa staili hiyo.

Nilitaraji ialikwe hata AFC Leopards ya Kenya, hata AS Vita ya Congo au hata kuandaa mechi ya Simba na Yanga au na Azam angalau madaraja yanafanana.

Labda isemwe hii ya Morogoro ni uwakilishi wa mikoani bado ya Dar inakuja, hapo nitaelewa, lakini kwa hili, hawakumtendea haki.

Columnist: mwananchi.co.tz