Wakati Fainali za Kombe la Dunia 2018 zilizomalizika jana zilipokuwa zikipigwa nchini Russia niliona dalili za timu za Afrika kutolewa mapema katika fainali hizo na nikaandika uchambuzi niliouita ‘Makosa ya uwanjani yanavyoigharimu Afrika Kombe la Dunia’.
Niliona jinsi wachezaji wa Afrika wanavyocheza kwa nguvu, huku wakishindwa kutumia akili inayotakiwa.
Soka linahitaji akili ya juu uwanjani, soka linahitaji nidhamu, shauku, uamuzi, heshima na unyenyekevu.
Niliona baadhi ya wachezaji wa Afrika wanavyoshindwa kuzichezea timu zao za taifa kwa shauku, heshima na unyenyekevu.
Niliona pia, makosa katika safu ya ulinzi, ubunifu katika kiungo na ujanja katika pasi za mwisho, pia niliona timu za Afrika zikishindwa kuzuia mbinu za pasi za mwisho, mipira ya kona na hata mipira ya adhabu na kuwafanya washindwe kuwa bora mbele ya timu za Ulaya na Amerika Kusini.
Suala lingine nililoliona ni wachezaji wa Afrika kukosa umakini muda wote uwanjani, wakifanya vizuri kidogo baada ya muda mfupi baadhi ya wachezaji katika timu wanapoteza umakini hivyo timu pinzani kutumia mwanya huo kupata ushindi.
Kubwa zaidi nililoliona ni wachezaji wa Afrika kufanya makosa mengi katika mechi.
Sawa soka ni mchezo wa makosa, lakini makosa yaliyofanywa na wachezaji wa timu za Afrika katika Fainali za Kombe la Dunia 2018 ndiyo yaliyozigharimu timu zote tano za Afrika na hivyo kutolewa katika hatua ya makundi katika Fainali za Kombe la Dunia 2018!.
Ndiyo, kuna mambo mengi ya kujifunza kutokana na Fainali za Kombe la Dunia 2018, lakini yapo matano ambayo ninaona ni ya muhimu zaidi hasa kwa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.
Moja ni kuwekeza kwa wachezaji wenye kiwango cha juu, tuwe nao kwa muda mrefu, tusikubali kuwapoteza mapema. Kwa mfano katika fainali hizi za Kombe la Dunia zilizomalizika tumeona kuna timu zilikuwa na wachezaji waliozichezea timu hizo kwa zaidi ya miaka mitano mfululizo.
Baadhi yao ni (Andres Iniesta, Sergio Ramos, Gerald Pique, Sergio Busquets-Hispania), (Chicharito, Dos Santos, Guillermo Ochoa, Rafael Marquez-Mexico), (Edson Cavani, Luis Suarez, Godin- Uruguay), Brazil (Fernandinho, Paulinho, Neymar, Tiago Silva, Marcelo) na Ujerumani (Manuel Neuer, Jerome Boateng, Mat Hummels, Mesut Ozil na Sam Khedira).
Pili, ni kwamba wachezaji wa timu ya Taifa wanatakiwa kuwa na stamina na kutumia akili zaidi uwanjani.
Soka la kimataifa linahitaji zaidi ya kipaji.
Soka la kimataifa linataka wachezaji wanaofikiri na kufanya maamuzi katika muundo wa pamoja (Wachezaji walioiva kiujuzi).
Tatu, kocha wa timu ya taifa anatakiwa awe kocha wa kimataifa; makocha ambao walipata mafanikio katika klabu walizozichezea katika kiwango cha kimataifa. Kigezo cha kuwa kocha wa ligi yetu ya nyumbani hakitoshi!
Soka la kimataifa linahitaji upeo wa juu.
Nne, ni kwamba hata kama nafasi za timu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia zitaongezwa na kuwa 50 bado itatuchukua miaka 50 zaidi kuweza kufuzu kushiriki fainali hizo kwa sababu Tanzania tupo miaka mingi nyuma katika soka.
Tano, ni kwamba mchezo wa soka ni mkubwa kuliko uwanja wa mpira!, soka ni biashara kubwa, soka ni utalii, soka ni fedha za kigeni, soka ni ajira na miundombinu.
Swali la kujiuliza, Je, tumejifunza nini katika Fainali za Kombe la Dunia2018?
Wakati mwingine naweza kujijibu kuwa imekuwa kawaida, tuliangalia fainali kishabiki na mapenzi kwa baadhi ya timu lakini hakuna tulichojifunza iwe kwa wachezaji na hata wadau wengine.
Itapendeza kama kile kilichojiri Russia walau robo yake inafanyiwa kazi.