Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ni miaka mitano ya joto la uchaguzi

11462 UCHAGUZI+PIC%255C TanzaniaWeb

Sun, 12 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Yanayoendelea katika Jimbo la Buyungu, Kigoma na katika kata mbalimbali nchini ni mwendelezo wa wapigakura kuchagua mbunge na madiwani kujaza nafasi ambazo ziko wazi.

Jambo hili hivi sasa linaelekea kuwa kawaida. Uchaguzi mdogo kila kukicha. Buyungu aliyekuwa mbunge, Kasuku Bilago alifariki dunia, kwingineko madiwani walijiuzulu na kuhama chama kutoka upinzani kwenda chama tawala na kuna wengine walifariki dunia.

Kutokana na hali hiyo, katika miaka mitatu ya mwanzo ya awamu ya tano, wapiga kura katika maeneo mbalimbali nchini wameendelea kusubiri zamu ya mwakilishi gani atatangaza kujivua ubunge au udiwani na kisha uchaguzi kurudiwa. Ni joto la uchaguzi mtindo mmoja, linazidi kupanda.

Baada ya mbunge kuachia jimbo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hupokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge kuitaarifu kuhusu nafasi husika kuwa wazi.

Hatua hii inafanyika kwa mujibu wa Katiba inayotamka kuwa, pamoja na sababu nyingine, mbunge na ataacha kiti chake ikiwa mbunge ataacha kuwa mwanachama wa chama alichokuwamo wakati alipochaguliwa au alipoteuliwa kuwa mbunge.

Mbali na sababu za kupoteza maisha kwa baadhi ya wawakilishi, suala la kujitoa katika vyama limechukua sura mpya na wiki iliyopita NEC imetangaza uchaguzi mdogo utakaofanyika Septemba 16 katika kata 21 na majimbo matatu ya Korogwe Vijijini, Tanga; Ukonga, Dar es Salaam na Monduli mkoani Arusha.

Wakati NEC ikitangaza ratiba hiyo, hivi sasa zinafanyika kampeni kwa ajili ya uchaguzi wa kata 77 na jimbo moja utakaofanyika kesho katika maeneo mbalimbali na si ajabu wengine wakaendelea kujiuzulu. Huu ni uchaguzi mdogo wa tano tangu kumalizika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015.

Kwa hali inavyoonekana, nchi itakuwa katika joto la uchaguzi katika kipindi chote cha miaka mitano tangu 2015 hadi mwaka 2020; ikizingatiwa kuwa mwakani kutakuwa na uchaguzi wa Serikali za mitaa na mwaka 2020 utakuwa ni Uchaguzi Mkuu.

Hatua ya kuendelea na uchaguzi karibu hii mbali na athari za kisiasa za malumbano na misuguano isiyoisha, inaweza kuathiri kwa kiwango gani shughuli za uzalishaji, utekelezaji wa mpango wa miaka mitano au Ilani ya CCM.

Mhadhiri wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Haji Semboja anataja athari za aina mbili zinazotokana na hali ya wananchi kupitia kwenye joto la uchaguzi katika kipindi hicho, akisema kuna athari zinazoonekana wazi na zile zisizoonekana.

“Sababu ambazo ni za moja kwa moja ni pamoja na Serikali kuingia gharama za fedha nyingi ambazo zingeweza kutumika kwa matumizi mengine, achilia mbali gharama ya muda unaotumika katika mchakato.

“Watu wanaoshiriki katika mchakato kuanzia CCM, Chadema na vyama vingine, walitakiwa kuwa kwenye shughuli nyingine za kiuchumi,” anasema.

Profesa Semboja anataja sababu nyingine zisizoonekana ni pamoja na hofu ya kuendelea kuingia kwenye gharama ya demokrasia kupitia utamaduni wa wanasiasa kuhamahama.

“Je, hali hii itakoma au itaendelea kujitokeza baada ya uchaguzi mkuu ujao. Kwa sababu ni haki yao kimsingi kuhama chama, je, vyama vya siasa vimejiandaa kimfumo kuhakikisha wanapata wagombea imara na wanaoaminika ili kuepuka gharama za demokrasia ya aina hii?” anahoji Profesa Semboja.

Mkurugenzi wa Sera wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), Hussein Kamote pia anaona athari za kiuchumi katika mchakato huo, akisema wanaoathirika zaidi ni wazalishaji katika eneo la uchaguzi unakofanyika.

“Lakini, kuathirika kwa shughuli za kiuzalishaji kunategemeana na majira, kwa mfano kama watu wamefikia hatua ya kuvuna inawezekana isiwe taabu sana kama uchaguzi ungefanyika kipindi cha kulima na kupanda. Bado kwa vyovyote vile kuna athari iwe mashambani au viwandani, imekuwa kama ushabiki wa mpira na unafanya watu kufikiria uchaguzi tu, kwa hiyo haipendezi sana kufanyika kila wakati,” anasema Kamote.

Chaguzi nyingine

Jumapili ya Oktoba 25, 2015, Watanzania walielekea vituoni kuwachagua viongozi kwa miaka mitano ijayo baada ya kushiriki kampeni za uchaguzi huo. Kwa upande wa Zanzibar uchaguzi ulifutwa na kuitishwa upya Machi 20, 2016.

Novemba 26, 2017, vyama vya siasa vikaingia tena katika uchaguzi mdogo uliofanyika katika kata 43 ili kuwapata wawakilishi baada ya wengi wao kujivua uanachama Chadema na kuhamia CCM au kufariki dunia.

Januari 14, mwaka huu uchaguzi mwingine ukaitishwa na CCM ikapata ushindi katika uchaguzi mdogo wa majimbo ya Songea Mjini, Singida Kaskazini na Longido. NEC ilitangaza kufanyika kwa uchaguzi huo baada ya wawakilishi wake kuhama vyama na mbunge wa Songea mjini Leonidas Gama kufariki dunia.

Mwezi uliofuata, Februari 17, mwaka huu NEC iliendesha uchaguzi mwingine katika majimbo ya Kinondoni (Dar es Salaam) baada ya mbunge wake, Maulid Mtulia aliyekuwa CUF kuhamia CCM na Siha mkoani Kilimanjaro ambako mbunge wake Dk Godwin Mollel aliyekuwa mbunge kupitia Chadema kuamua kukihama chama hicho kikuu cha upinzani na kuhamia CCM. Katika uchaguzi huo ambao CCM ilishinda majimbo yote ya Siha na Kinondoni, kampeni zilichukua nafasi kubwa katika mitandao ya kijamii.

Pia, kesho unafanyika uchaguzi mdogo katika kata 77 na jimbo moja la Buyungu unaotokana na sababu mbalimbali zaidi ikiwa ni kuhama vyama kutoka upinzani kujiunga na CCM. Uchaguzi huo mdogo ni wanne.

Tume hiyo imetangaza tena uchaguzi mdogo wa marudio ikiwa ni mara ya tano utakaofanyika Septemba 15 mwaka huu katika kata 21 na majimbo matatu ya Korogwe Vijijini, Ukonga na Monduli. Uchaguzi huo unafanyika baada ya wabunge wawili wa Ukonga na Monduli wote wa Chadema kujiuzulu na kuhamia CCM, wakati jimbo la Korogwe Vijijini mbunge wake Stephen Ngonyani ‘Majimarefu’ alifariki dunia.

Kwa mujibu wa Katiba, Tanzania huingia kwenye chaguzi mara mbili endapo hakutatokea changamoto ya mbunge au diwani kufukuzwa uanachama, kuhama chama au kufariki dunia. Lakini safari hii mambo ni tofauti.

Tatizo linaanzia wapi?

Kujitokeza kwa idadi nyingi ya chaguzi katika kipindi cha awamu ya tano, kumeibua dhana mbili tofauti zilizoitenganisha jamii katika mitazamo. Kundi moja linaamini hatua ya wanasiasa kuhama vyama inaweza kuwa ni kiwango kikubwa cha ukuaji wa demokrasia hapa nchini ambayo haikuwahi kutokea katika vipindi vya uongozi wa chama hicho.

Mbali na kundi la wawakilishi wanaofariki dunia, wanasiasa wanaohama vyama wamekuwa wakieleza sababu za kuchoshwa na vyama wanavyotoka huku na kufurahishwa na vyama wanavyokwenda.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Samwel Ruhuza anatofautiana na dhana hiyo akisema ni demokrasia feki inayotengenezwa na kundi moja la watu wenye mlengo wa CCM.

Anasema gharama ya kuingia kwenye chaguzi hizo ni hofu ya CCM kupoteza nguvu katika maeneo mengi yenye ngome za upinzani.

“NEC imewahi kutoa taarifa za gharama ya kuingia kwenye uchaguzi, kwa jimbo moja inatumia karibu Sh2 bilioni, kwa kata moja inatumia karibu Sh100 milioni, kwa sasa tunazo kata ngapi zilizofanya uchaguzi? Halafu uchaguzi wa marudio CCM inamsimamisha mgombea yuleyule aliyejiuzulu? Kuna ulazima gani wa uchaguzi hapo? anahoji Ruhuza.

Ruhuza anapendekeza kwamba, Bunge lijadili marekebisho madogo ya Katiba kuepusha gharama ya kuingia kwenye uchaguzi wa marudio kwa mbunge au mwakilishi anapohama, kufariki dunia au vinginevyo.

“Mgombea anasimamishwa na chama, kwa hiyo wapiga kura hawamchagui mgombea anayejinadi ila chama kilichomsimamisha, kama ndiyo hivyo kwa nini mwakilishi akiondoka, chama kisiteue mwakilishi aliyeshinda nafasi ya pili katika kura za maoni? Kwa nini isifanyike kama utaratibu wa viti maalumu?

Katibu wa CCM wa Mkoa wa Mara, Innocent Nanzaba anatofautiana na mtazamo wa Ruhuza akisema chama kinachoongoza jimbo kutangaza mwakilishi mwingine bila kurudia uchaguzi si demokrasia tuliyokubaliana.

“Siungi mkono, huwezi kupitisha mtu aliyeshinda nafasi ya pili, watu wanabadilika kwa hiyo mchujo unahitajika. Anayehoji gharama zinazotumika haelewi maana ya demokrasia. Ndiyo makubaliano ya kitaifa, tuko kwenye mfumo wa vyama vingi, wanasiasa wanaamua wakati wowote watumike wapi,” anasema Nanzaba.

Vurugu, kesi za kisiasa

Katika chaguzi hizo, tayari kuna athari ya kesi, migogoro na vifo vimejitokeza. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji anasema uchaguzi huo umeongeza majeraha zaidi ndani ya chama hicho kwa kuathiri maisha ya vijana ambao wengi wao ni wafuasi wa chama hicho.

Akitoa mfano wa kesi zilizofunguliwa mahakamani dhidi ya wafuasi na viongozi wa chama hicho ni pamoja na uchaguzi wa udiwani Kata ya Sofi, wilayani Malinyi, baada ya msimamizi kutangaza matokeo ambayo yalibishaniwa na vijana kuibua vurugu hatua iliyosababisha kukamatwa na kufunguliwa kesi mahakamani.

Tukio hilo lilitokea katika kipindi cha uchaguzi wa marudio katika jimbo la Kinondoni.

“Pia, kuna vijana waliokamatwa kwa kosa la maandamano, sijui mikusanyiko na kesi yao iko Mahakama ya Kisutu. Pia, kuna kesi ya viongozi wa juu wa chama kwa tuhuma za kufanya maandamano yasiyokuwa na kibali wakati wa kuelekea uchaguzi wa marudio jimbo la Kinondoni,” anasema.

Aidha, Februari 15, mwaka huu, Katibu wa chama hicho Kata ya Hananasif, Daniel John alipatikana katika ufukwe Coco. Hayo yote ni matukio yanayoambana na chaguzi ndogo na endapo hazitaisha, hakuna ajuaye nini kitatokea kesho.

Columnist: mwananchi.co.tz