Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ndoto za mafundi wasio na vyeti

10649 PIC+NDOTO TanzaniaWeb

Tue, 7 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ni karakana ndogo ya ukubwa wa kama futi 12 kwa 12. Ndani ya chumba kumejaa vyuma, vipande vya mabati, makopo ya rangi na vifaa vingine vya ufundi.

Ukitazama kwa haraka kama hujui kazi na thamani ya hivi vilivyomo ndani ya chumba hiki, unaweza kuona ni kama takataka. Nje ya karakana hii vinaonekana baadhi ya vitu viliyotengenezwa kwa vyuma hivyo.

Kitanda cha rangi nyeusi ya kuvutia ambacho kinaonyesha kipo tayari kwa ajili ya matumizi, madirisha, meza ya kujipambia na geti kubwa lililopakwa rangi tofauti na kuwekwa urembo. Hizi ni baadhi ya samani zilizopo nje ya karakana hii ndogo.

Vitu hivi ni matunda ya vyuma vilivyojaa ndani ambavyo kwa asiyejua kazi yake, anaweza kuvichukulia kama takataka kwake.

Hata hivyo, kwa Jeremia Thomas, vyuma hivyo ndivyo vinavyompa kipato cha kuendesha familia yake ya watu wanne.

Thomas anayeishi Tabata Kimanga mkoani Dar es Salaam, ni fundi wa kuchomelea samani za chuma, fani anayosema hakuisomea kokote zaidi ya kujifunza kupitia vitendo. Hana cheti, lakini ufundi huu ndio umuwekao mjini na kumudu maisha yake.

“Mwaka 2005 nilianza kazi hii ikiwa ni baada ya kumaliza darasa la saba mwaka 2004 na wazazi wangu kushindwa kumudu gharama za masomo,”anasema.

Anasema kwa kipindi hicho hata fedha ya kwenda kusomea ufundi chuoni hakuwa nayo, jambo ambalo lilimlazimu kujifunza kupitia vijana wenzake waliokuwa wakifanya kazi hiyo.

INAENDELEA UK 18

INATOKA UK 17

Anasema baada ya kukaa kwa muda katika karakana hiyo na kumudu mafunzo kikamilifu, aliamua kufungua kijiwe chake ili kuendeleza shughuli hiyo, huku akiwa na mashine moja ya kuchomelea aliyoinunua kwa Sh50,000.

Ufundi bila vyeti

Hadithi Thomas haitofautiani na ile ya Nasibu Mayazi ambaye pia ni fundi mchomeleaji wa samani za chuma kwa miaka 11. Anasema anafanya kazi hiyo lakini hana cheti chochote cha ufundi stadi.

Ufundi huu wa uchomeleaji na aina nyingine za uchumi, umekuwa kimbilio la vijana wengi wenye ndoto za kufanikiwa kimaisha. Ni vijana mahodari na mabingwa wa ufundi, lakini hawatambuliki na mifumo ya kielimu na kimafunzo nchini.

Mitaani, mijini na vijijini kumejaa mafundi makenika, maseremala, na mafundi wengine mbalimbali waliojiajiri katika sekta ya ufundi.

Nasibu anasema baada ya kumaliza darasa la saba 2004 na kukosa nafasi ya kuendelea na masomo, aliamua kutafuta kitu cha kumuingizia kipato kilicho nje ya elimu.

“Wakati nawaza kitu cha kufanya mwaka 2007, nilikuwa nashinda kwa rafiki yangu anayefanya kazi ya utengenezaji wa samani za ndani kwa kutumia chuma, nikawa kama msaidizi wake, huku nikimwangalia. Ulifika wakati namimi nikawa na uwezo wa kutengeneza kitu,’’ anasimulia alivyoanza ufundi.

Ufundi vyuma hauhitaji vyeti

Utafiti mdogo uliofanywa na gazeti hili, umebaini kuwa vijana wengi wanaojihusisha na utengenezaji wa samani mbalimbali kwa kutumia vyuma na mbao, mafundi magari na wengineo, hawana vyeti kutoka kutoka vyuo vya ufundi na wala hawatambuliki.

Hata hivyo, kukosa vyeti sio kikwazo kwao, japo baadhi wanakiri kuwa wamewahi kukosa kazi kutokana na kutokuwa na vyeti.

“Hizi kazi zetu bila kuwa na cheti au kuingia darasani ni ngumu kupata tenda kubwa zinazotangazwa na kampuni, taasisi au Serikali, anasema Nasibu.

Kwa upande wake, Thomas anasema baadhi ya wateja huamini zaidi watu walio na vyeti kuliko wasiokuwa navyo.

“Kuna wakati mtu anakunyima kazi kabisa kutokana na kukosa cheti. Hakuamini hata ukimuonyesha kazi zako nyingi ulizowahi kuzifanya kwa umahiri mkubwa, bado atakuona kama mjanja wa mjini,” anaeleza.

Hata hivyo, kwa Babuali Ahmad licha ya kuwa na cheti cha ufundi stadi kutoka chuo cha Veta Tanga, haoni umuhimu wa kuwa nacho kwa sababu hakuna aliyewahi kukiulizia tangu aanze kazi hiyo mwaka 2009.

Anaamini kuwa hata aliyejifunza mtaani anaweza kutengeneza samani nzuri zaidi ya fundi aliyekaa darasani.

“Haya mambo hayahitaji vyeti lakini utundu, ubunifu na namna ambavyo unavyoweza kucheza na mbao zako au vyuma, ili kuhakikisha unapata kitu bora na kinachoweza kumvutia mteja,” anasema Ahmad ambaye ni fundi seremala jijini Dar es Salaam.

Malengo yao

Vijana hawa wanasema kuwa wana ndoto za kufika mbali, ikiwamo kumiliki biashara na kutengeneza fursa za ajira kwa vijana wengine waliokosa fursa ya kuendelea na elimu.

Kwa mfano, Mayazi anasema mbali na uchomeleaji wa magari, endapo atapata fursa ya kujiendeleza kielimu, anapenda kusomea umeme wa magari.

“Ukiwa fundi wa magari ili upate wateja lazima uwe katika kampuni inayoaminika itakayohitaji uwe na elimu. Hii ni tofauti na utengenezaji wa samani za chuma kwani mteja anaweza kukuamini hata bila ya cheti,” anaeleza.

Kwa Thomas ndoto aliyonayo ni kwenda shule kuendeleza ujuzi wake…

“Elimu haina mwisho, hivi sasa naweza kufanya hivi kwa ufasaha lakini naamini nikikaa darasani ntafanya vizuri zaidi ya hapa.’’

Tunawasaidiaje?

Aliyekuwa Makamu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Idris Kikula anasema kinachotakiwa ni kuangalia namna ambayo vijana hao wanaweza kuongezewa ujuzi kutoka kwa wataalamu bila ya malipo ili waweze kuboresha utendaji kazi wao.

“Hawa ni sawa na wakulima wengine ambao hawajawahi kwenda kusomea kilimo lakini wanalima na wanapata mazao mengi kutokana na kusaidiwa kielimu, anasema na kuongeza:

“Uwezo wa wa vyuo vya Veta sio mpana kiasi hicho na sio wote wanaoweza kumudu gharama. Kama vijana wamejitengenezea kikundi ili wajiendeleze kinachoweza kuwasaidia ni kuwapatia mtaalamu awaelekeze hata kwa siku moja au mbili, ili waweze kufanya kitu bora zaidi ya hicho.’’

Kaimu Naibu Makamu wa Chuo cha Mzumbe Taaluma, Profesa George Shumbusho anasema Serikali inapaswa kuhakikisha malighafi wanazotumia kwenye shughuli zao zinapatikana kirahisi.

“Kufanya hivyo kutafanya waache kung’oa alama za barabarani, vyuma vya madaraja, hivyo Serikali ijenge viwanda vya chuma ili kurahisisha upatikanaji wake,” anasema Profesa Shumbuso.

Columnist: mwananchi.co.tz