Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ndoa inakupa unachotafuta, sio unachotaka

28740 Pic+ndoa TanzaniaWeb

Mon, 26 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Upo kazini, unapokea meseji kutoka kwa mwanamke ambaye unashirikiana naye kumzunguka mke wako—kwa lugha nyepesi mchepuko – inasomeka; ‘Mjinga wangu amesafiri. Unaweza kuja leo’.

Na wewe ni kama mwanasiasa aliyeona kamera za waandishi, hutaki kupitwa. Baada ya kuisoma tu na kumuhakikishia kuwa utakwenda, unamtumia meseji mkeo kumjulisha mambo mawili – kwanza kwamba unaweza kurudi nyumbani usiku sana kwa sababu kuna kazi ya dharura mnatakiwa muimalizie, na pili ni kama itashindikana basi utarejea hata asubuhi – naye anajibu sawa mume wangu, bila chembe ya mashaka juu yako.

Unatoka kazini unakwenda nyumbani kwa mdhambi mwenzio. Anakwambia leo tuna nafasi kama yote, huyu bwege kasafiri, lakini pia nilimuaga kwamba na mimi nitakwenda Bagamoyo kwa mama kwa hiyo huko alipo hana wasiwasi; unachekelea, unaona umelamba dume.

Mara punde mnasikia hodi mlangoni, mwenzio uliyejifungia naye ndani anakuhakikishia kwamba huyo anayegonga mlango ni mwenye mali, kwa hiyo ili kuokoa ndoa yake na roho yako – mnakubaliana kwamba akufiche uvunguni mwa kitanda, akupe na funguo moja ya mlango, abaki na moja, amfungulie mumewe.

Halafu kwa sababu yeye aliaga kuwa atakwenda Bagamoyo, aende aache wewe ukiwa uvunguni – huku akikuhakikishia kuwa kwa kufanya hivyo, kutamfanya mume wake atoke nyumbani, kwa sababu hawezi kukaa peke yake – kwa hiyo wewe utatoka na kuondoka kiulaini kama kwako.

Kwa akili zako unakubali – unaingia uvunguni. Mdhambi mwenzio anafungua mlango, mume wake anaingia. Unasikia kila kinachoendelea ukiwa uvunguni. Unasikia mwanamke anaaga, anajiandaa, anaondoka, wewe ukiwa bado uko uvunguni na ujui ni saa ngapi utatoka.

Sasa badala ya mambo kwenda kama ulivyotaka, yaani mwenye nyumba atoke kwa sababu mkewe ametoka, yanakwenda kinyume, unasikia mwenye nyumba anapiga simu kana kwamba kuna mtu wanakubaliana aje pale ndani – na kweli, baada ya dakika chache anakuja mwanamke ambaye unagundua kuwa ni mchepuko wa mwanaume.

Na anapoingia unasikia mwanaume akimwambia, hili jinga limekwenda kwa mama yake Bagamoyo, litarudi kesho.

Kisha dakika chache tu baadaye hodi inasikika mlangoni. Ukiwa chini ya uvungu unasikia mazungumzo ya mume na mchepuko wake yakithibitisha kwamba huyo anayekuja ni mchepuko wake – hivyo mume wake naye ana kibarua cha kumficha muasherati mwenzake.

Haraka wanapata wazo la kwamba mwanamke aingie uvunguni, kisha watafuta upenyo wa kumtoa baadae – bila kujua kama wewe umetulia uvunguni, wanalipitisha wazo lao.

Mwanamke anaingizwa uvunguni, ile kuingia anakukuta na wewe, anajikausha baada ya kuelewa kinachoendelea, lakini baada ya kuingia kabisa na kutulia – unagundua kuwa huyu ndiye yule mwanamke uliyemuaga kuwa utachelewa kurudi nyumbani au utalala kabisa huko huko– yaani mkeo.

Hadithi ya kufanana na hivi ikija kukutokea ndiyo utaelewa kwa nini wauza kahawa wanatembea na vyombo vya moto lakini hawana leseni.



Columnist: mwananchi.co.tz