Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ndege ya ATC iliyotekwa kushinikiza Nyerere ajiuzulu (6)

29322 Ndege+pic TanzaniaWeb

Thu, 29 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katika viwanja vya ndege vya Nairobi na Jeddah, Saudi Arabia ndege hiyo iliruhusiwa kutua, kujaza mafuta na kuondoka.

Kabla ya ndege hiyo kupelekwa Uingereza na kuamriwa kutua Uwanja wa Ndege wa Stansted badala ya Heathrow, ilikuwa imeweka kituo chake cha tatu jijini Athens, Ugiriki.

Baada ya kujaza mafuta kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mfalme Abdulaziz mjini Jeddah, kituo cha tatu kilikuwa Athens. Pamoja na maombi mengi ya Serikali ya Tanzania ya kutaka ndege hiyo izuiwe kuondoka, maofisa wa Ugiriki walitangaza mapema kabisa, hata kabla Boeing 737 haijatua, kwamba ingeruhusiwa tu kujaza mafuta na kuondoka mara moja bila kuikawiza.

Ikiwa imetua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Athens, aliletwa daktari mmoja ambaye aliingia kwenye ndege hiyo kwa kusudi la kutibu jeraha la risasi alilopata Oscar Mwamaja, rubani msaidizi wa Kepteni Deo Mazula. Daktari huyo alipoingia ndani, mmoja wa watekaji alimuuliza: “Mapinduzi hayajaanza huko Dar es Salaam au bado?”

Hata hivyo, pamoja na kwamba hawakuelewana vizuri katika lugha, daktari huyo hakuweza kumjibu kwa sababu alishangaa kuulizwa maswali yanayohusu siasa za Tanzania. Mtekaji huyo alidhani kuwa Watanzania ni watu ambao walikuwa wameudhika sana kiasi kwamba tukio moja kama hilo la kuteka ndege lingeweza kusababisha maasi ya jumla.

Baada ya kutibu jeraha la Mwamaja, daktari huyo alishuka kisha akawaambia maofisa wa uwanja hapo kuwa ndani ya ndege hakuona kielelezo chochote kilichoashiria kwamba kuna mtu mwingine aliyejeruhiwa—iwe kwa risasi au kwa silaha nyingine yoyote—isipokuwa rubani Mwamaja.

Kabla ya kuondoka Athens, watekaji walimwachia mtu mmoja aliyedaiwa kuwa alikuwa ni dereva wa lori mwenye asili ya Kisomali na kasisi mmoja wa Ubelgiji. Waliwaachia wawili hao kwa kile walichodai kuwa wao “si raia wa Tanzania”. Kisha wakaomba wapatiwe ramani ya anga lote la Ulaya.

Wakati mmoja, watekaji hao aliwaambia abiria kuwa wangewapeleka “kwa Kanali Gaddafi (Libya)”. Lakini ndege ilipoondoka Athens, watekaji walianza kuzungumza habari za Oscar Kambona (54) ambaye kwa wakati huo alikuwa akiishi uhamishoni Uingereza.

Kambona aliwahi kuwa waziri katika Serikali ya Tanzania kabla ya kukimbia nchi mwaka 1967 baada ya kushindwa kuelewana na Rais Nyerere katika siasa za Ujamaa na Kujitegemea.

Wakisukumwa na hamu ya kukutana na Oscar Kambona na ‘kuratibu’ mpango wa kumuandaa arejee Tanzania kuchukua nafasi ya urais badala ya Mwalimu Nyerere, watekaji hao waliiamuru ndege ipelekwe London, Uingereza.

Tangu mapema kabisa Serikali ya Uingereza ilikuwa imepata taarifa za kutekwa kwa ndege hiyo, lakini haikujua kuwa ingepelekwa huko. Kwa hiyo baada ya maofisa kujua kuwa ndege hiyo sasa ilikuwa ikielekea Uingereza, serikali ilielekeza itue Uwanja wa Stansted, nje kidogo ya jiji la London.

Kamati ya watu 35 ya maofisa wa Uingereza ya kushughulikia tatizo kama hilo la utekaji iliingia kazini mara moja kufanya kazi yake. Kamati hiyo ilifanya kikao chake cha dharura na cha haraka kilichokuwa chini ya uenyekiti wa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza, William Stephen Ian Whitelaw, na kuwajumuisha maofisa kadhaa wa usalama, mkuu wa polisi wa Jimbo la Essex, Peter Simpson akiwa miongoni mwao. Uwanja huo uko jimbo la Essex.

Uwanjani zilikuwapo ndege kadhaa na magari ya kubeba wagonjwa yakiwa na maofisa wa afya waliokuwa tayari kwa lolote. Yaliegeshwa kando ya eneo ambalo ndege ya Tanzania ingetua, huku vinasa sauti vikiwa vimewekwa mahali maalumu.

Askari wa kikosi cha watu wapatao 80 waliokakamaa na waliovalia kofia maalumu na nguo zisizopenya risasi, walijificha uwanjani hapo wakiwa na kazi ya kutazama na kusubiri kitakachotokea.

Hawa walikuwa ni askari wa kikosi maalumu cha huduma za anga chenye makao yake makuu katika mji wa Hereford. Walikuwa na silaha mbalimbali, zikiwamo SMG (sub-machine guns) na mabomu ya kutupwa kwa mkono.

Mara baada ya ndege kutua, magari matano yakiwa yamesheheni polisi yalifika na kuizingira ndege hiyo. Muda mfupi baadaye taa zote za Uwanja wa Ndege wa Stansted zilizimwa. Magari ya kuzima moto nayo yaliletwa kuizingira ndege hiyo.

Dakika chache baadaye alitumwa ‘mwanasaikolojia’ mmoja kwenda kuzungumza na watekaji hao. Mwanasaikolojia huyo ambaye alitambulika kwa jina moja tu la Mike, alikuwa akizungumza kama mtu wa kati baina ya watekaji na maofisa wa Serikali ya Uingereza. kazi yake kubwa ilikuwa ni kuwachunguza, kuwashawishi na kuwalainisha.

Magari yote yaliyokuwa yameegeshwa karibu na eneo la ndege hiyo, yaliondolewa kwa tahadhari dhidi ya lolote lisilotazamiwa. Ilionekana kana kwamba hata watekaji walikuwa wamejiandaa kwa hali hiyo.

Wakati hali ya Uwanja wa Stansted ikiwa ni ya wasiwasi baada ya kuonekana kuwa watekaji hawaambiliki, balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Anthony Balthazar Nyaki alionyesha kuwa anao uwezo wa kukabiliana na watekaji hao. Lakini alichelewa sana kufika uwanjani hapo.

Ndege ya ATC ilivyotekwa kushinikiza Nyerere ajiuzulu (5)

Itaendelea kesho



Columnist: mwananchi.co.tz