Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ndege ya ATC ilivyotekwa mwaka 1982 kushinikiza Nyerere ajiuzulu (4)

29007 Ndege+pic TanzaniaWeb

Tue, 27 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Baada ya Serikali ya Uingereza kupata habari kuwa ndege iliyotekwa ya Shirika la Tanzania (ATC) ingewasili Uwanja wa Stansted, waliuzingira kukabiliana na watekaji. Mara baada ya ndege kutua, magari matano yakiwa yamesheheni polisi yalifika na kuizingira ndege hiyo. Muda mfupi baadaye taa zote za uwanjani zilizimwa na magari ya kuzima moto yakaizingira ndege hiyo.

Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Anthony Balthazar Nyaki alifika uwanjani hapo, ingawa alichelewa.

Vijana walioteka ndege hiyo ni Mussa Memba (25), Mohamed Ali Abdallah (26) na nduguye Abdallah Ali Abdallah (22), Mohamed Tahir Ahmed (21) na Yassin Memba (21).

Balozi Nyaki alikuwa ameteuliwa mwaka uliopita (1981) kuwa balozi wa Tanzania nchini Uingereza kuchukua nafasi ya Amon James Nsekela aliyeishikilia nafasi hiyo kuanzia mwaka 1974.

Baadaye kidogo Balozi Nyaki alijitokeza kukabiliana na watekaji. Huu ukawa ni mchezo wa ama kuelewana au kutoelewana kati ya mwanadiplomasia na watekaji nyara waliotaka Rais wa nchi yao ajiuzulu.

Balozi Nyaki aliwasili Stansted saa 1:33 usiku (saa za Afrika Mashariki) ikiwa ni muda wa saa tano baada ya ndege hiyo kutua. Hata hivyo hakuonekana kuwa na wasiwasi.

Katika hali ya haraka kidogo na kumkasirikia balozi, watekaji walitaka kujua sababu za Balozi Nyaki kuchelewa kufika uwanjani hapo wakati ujumbe wao wa kumtaka afike uwanjani ulitumwa saa kadhaa zilizokuwa zimepita. Kwa kuwa walichukulia kuwa wamedharauliwa, hasira zao zilipanda hata zaidi.

Kwa utulivu, Balozi Nyaki aliwaelewesha kuwa yeye kama mtu aliyepata heshima ya kuwa mwakilishi wa Serikali ya Tanzania nchini Uingereza, angeweza tu kufanya kazi kwa kutegemea mawasiliano anayopewa na mwenyeji wake—yaani Serikali ya Uingereza. Aliwaambia kuwa angekwenda uwanjani hapo ikiwa tu angehitajika kufanya hivyo, na wala si kujiendea tu kwa matakwa yake yeye mwenyewe.

“Kambona yuko wapi?” walimuuliza.

“Sijui aliko,” aliwajibu.

“Inawezekanaje hujui?” waliuliza.

“Waingereza waliompa hifadhi ndio wanajua aliko,” alijibu kwa utulivu.

Waliposisitiza kwamba Kambona aletwe ili waweze kuonana naye, halafu wapatiwe maji, chakula na mafuta kwa ajili ya ndege. Kwa utaratibu kabisa Balozi Nyaki aliwajibu kwamba “mambo yote hayo mnayoyataka yako nje ya uwezo wangu”.

Lakini hayo yote—maji, chakula na mafuta ya ndege—yalikuwa ni matakwa madogo. Kuonana na Kambona na kupewa maji, chakula na mafuta kwa ajili ya ndege yao yalikuwa ni madai madogo. Hadi wakati huo, watekaji hawakuwa wametoa dai lao kubwa zaidi; Nyerere ajiuzulu.

Hatimaye likaja lile dai kubwa kuliko yote waliyokuwa nayo. Hilo ndilo lilikuwa shabaha yao. Ni lile dai ambalo wanasiasa wa Tanzania hawakutaka lijulikane. Dai hilo lilikuwa jambo zito kwa balozi yeyote—hasa kwa balozi wa Tanzania.

“Ni lazima Rais Julius Nyerere ajiuzulu,” walisema watekaji hao.

Balozi Nyaki hakuwa na haraka ya kuuliza wala kujibu maswali yao. Huenda tayari alikuwa amekwishapata fununu ya madai yao. Kwa hiyo hakuonekana kushtuka sana dai hilo lilipotajwa. Walipoona anakawia kuwajibu, walirudia dai lao: “Tunataka Nyerere ajiuzulu.”

“Mko wangapi ambao mnadai jambo hili?” aliwauliza.

“Elfu tatu (3,000),” walijibu.

“Watu elfu tatu?” alihoji Balozi Nyaki. “Yaani watu 3,000 mnataka ajiuzulu mtu aliyechaguliwa na mamilioni ya watu?”

Mjadala huo ulielemea upande wa Balozi Nyaki. Balozi alijua kwa hakika kuwa hatimaye angekuwa mshindi wa mjadala huo. Kwa hiyo hakufanya haraka. Aliwasubiri waulize maswali zaidi ili naye apate wasaa wa kujibu yote ambayo wangeuliza. Alijua kuwa kama hangewasikiliza na kujibu maswali yao, wao pia hawangemsikiliza na kujibu maswali yake.

Kwa kutumia uzoefu wake wa kidiplomasia, alitambua kuwa alihitaji nafasi ya kutosha ya kuwauliza maswali, lakini ili watekaji hao wampe nafasi hiyo, ilikuwa ni lazima kwanza yeye aanze kwa kuwapa nafasi hiyo.

Baada ya mjadala kuendelea kwa kitambo fulani, watekaji walilainika na kuonekana kuwa wamekosa hoja za kumjibu Balozi Nyaki. Mmoja wao akasikika akinung’unika: “Ah! Nyie ndio wakubwa bwana!”

Pamoja na kuzidiwa na hoja za Balozi Nyaki, watekaji hao hawakutaka kujisalimisha. Badala yake walimwomba Balozi Nyaki awasaidie waweze kukutana na Oscar Kambona, ambaye aliwahi kuwa waziri wa tawala za mikoa wa Tanzania na pia Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Peter Alexander Rupert Carington.

Balozi Nyaki, kwa kutumia uwezo ule ule wa kidiplomasia, aliwajibu kuwa ili kutekeleza hilo atalazimika kwanza kuomba ushauri kabla hajafikiria kulitekeleza. Walipotaka kujua itamchukua muda gani kuomba ushauri hadi kulitekeleza, Balozi Nyaki aliwajibu: “Sijui.”

Hata hivyo, hawakujisalimisha. Mwanadamu pekee ambaye sasa walitaka kumwona kuliko mwingine yeyote duniani alikuwa Kambona. Pamoja na kwamba walikuwa na njaa na kiu, ilionekana kana kwamba Kambona alikuwa muhimu kwao kwa wakati huo kuliko mahitaji hayo.

Ilihisiwa kwamba mtu aliyekuwa nyuma ya mambo yote hayo ni Kambona. Hata hivyo, Kambona alijitokeza mwishoni mwa mambo yote yaliyotendeka kwenye Uwanja wa Ndege wa Stansted.

Itaendelea kesho



Columnist: mwananchi.co.tz