Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ndege ya ATC ilivyotekwa kushinikiza Nyerere ajiuzulu-8

29787 Ndege+pic TanzaniaWeb

Mon, 3 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kama ilivyoelezwa katika toleo lililopita, utekaji wa ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATC) uliotokea Ijumaa ya Februari 26, 1982, kwa hakika ulikuwa ni wa tatu na wa aina yake lakini wa kwanza ambao Serikali ya Tanzania haikushiriki.

Matukio ya kutekwa kwa ndege nchini yalianza mwaka 1972 wakati wakimbizi wa Uganda walioukimbia utawala wa Idi Amin, wakisaidiwa na Watanzania, walijaribu kumrejesha Dk Milton Obote madarakani.

Sehemu ya uvamizi huo, kwa mujibu wa jarida la Africa Contemporary Record, ni kuchukua ndege iliyojaa ‘waasi’ ili itue kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe. Ili mpango huo uwezekane, maofisa wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam waliamriwa kufumba macho wakati rubani wa Uganda “akiiba” ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Mashariki kutoka uwanjani hapo.

Alhamisi ya Septemba 14, 1972, kwa mujibu wa ukurasa wa 47 wa kitabu cha Terrorism in Africa (Ugaidi Barani Afrika), ndege ya Shirika la Afrika Mashariki iliibwa usiku na rubani asiyejulikana kutoka Dar es Salaam

Baadaye ndege hiyo ilikutwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro ikiwa imepasuka matairi.

Mpango ulikuwa rubani huyo atue Uwanja wa Kilimanjaro kuwabeba waasi hao, lakini cha kushangaza alipokuwa akitua alisahau breki ya magurudumu ya ndege. Kwa sababu hiyo magurudumu hayo yakapasuka na mpango mzima nao ukaishia hapo. Wakati huo baadhi ya Waganda walioukimbia utawala wa Idi Amin walikuwa wakikutana mjini Moshi, Kilimanjaro kupanga mikakati ya kuuangusha utawala wa Amin. Kufikia mwaka 1979 zaidi ya vikundi 25 vya Waganda vilivyokuwa na lengo la kuikomboa nchi hiyo vilikuwa vimeshaundwa na vilikuwa vikikutana Moshi.

Hatimaye vikaibuka na kile kilichokuja kujulikana kama “Roho ya Moshi”. Utekaji wa ndege hiyo ulikuwa ni sehemu ya mikakati yao wakisaidiwa na Tanzania.

Utekaji wa pili ulifanywa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Na, jarida moja liliandika kuwa huenda huo ulikuwa ni utekaji wa kwanza wa kielektroniki kuwahi kutokea duniani.

Utekaji huo wa kielektroniki uliofanywa na JWTZ ulifanyika mwaka 1979 wakati vita ikiendelea kati ya Tanzania na Uganda. Wakati huo, ndege za mizigo za Libya zilikuwa zikifanya safari zake za usiku kumpelekea silaha Idi Amin. Mpango ulibuniwa jeshini kuziteka ndege hizo.

Usiku wa manane, wanajeshi wa JWTZ wakiwa Mwanza, walisubiri hadi walipoona kwenye rada ndege mojawapo ikielekea Entebbe, upande wa Uganda, karibu na Ziwa Victoria.

Waliwasiliana na rubani wa ndege hiyo na kujitambulisha kwake kwamba wao ni waongozaji wa ndege kwenye Uwanja wa Entebbe na kumuonya kuwa uwanja huo unashambuliwa vikali na wanajeshi na kwa hiyo isingefaa atue huko.

Wasiwasi mkubwa ulimpata rubani huyo kiasi kwamba alilazimika kuomba ushauri. Wanajeshi wa Tanzania wakamshauri kuwa uwanja wa ndege ulio karibu zaidi ni ule wa Mwanza na kwamba kwa sasa ni salama zaidi kutua.

Rubani alijaribu kuuliza maswali kadhaa alijibiwa kwa uangalifu. Majibu hayo, na jinsi yalivyotolewa, yalimridhisha rubani huyo. Kwa hiyo akaachana na uamuzi wake wa kwenda kutua Entebbe na akaamua kwenda Mwanza.

Mara baada ya ndege hiyo kutua Mwanza, ikazingirwa na wanajeshi wa Tanzania. Hata hivyo, walishangazwa kubaini kuwa ilikuwa ni ndege ya mizigo ya Shirika la Ubelgiji, Sabena, badala ya ndege ya Libya na iliyobeba silaha. Ndege hiyo ya Ubelgiji ilikuwa safarini kwenda Entebbe kubeba kahawa ili kuipeleka Djibout.

Kwa jinsi hali ilivyokuwa mbaya kutokana na kile kilichofanywa na Tanzania, Rais Julius Nyerere alilazimika kwenda ubalozi wa Ubelgiji kuomba radhi.

Tanzania na Uganda hawakuwa na uhusiano mzuri tangu Jumatatu ya Januari 25, 1971, siku ambayo Jenerali Idi Amin aliipindua serikali ya Dk Milton Obote. Tangu wakati huo kulikuwa na harakati nyingi kwa upande wa Tanzania zilizokuwa na lengo la kumrejesha Dk Obote madarakani.

Wakati hayo yaliposhindikana, huku uhusiano kati ya Tanzania na Uganda ukizidi kuzorota, mwaka 1978 Rais Julius Nyerere alitangaza vita dhidi ya “Nduli Idi Amin” baada ya majeshi ya Uganda kuvamia Kagera.

Alhamisi ya Novemba 2, 1978, Mwalimu Julius Nyerere alilitangazia Taifa kuhusu “uvamizi wa Idi Amin na uamuzi wa Tanzania wa kumpiga.” Akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwenye ukumbi wa mikutano wa Diamond Jubilee, Mwalimu Nyerere alielezea uamuzi huo wa Serikali.

“Nimewaombeni mkusanyike tena hapa (ili)niwaelezeni jambo ambalo kwa sasa wote mnalijua. Lakini naona si vibaya nikieleza. Nitajaribu kueleza kwa ufupi,” alisema Rais Nyerere.

“Huyu mtu ameivamia nchi yetu. Sasa hiyo ndiyo hali. Tufanye nini! Tunayo kazi moja tu. Watanzania sasa tunayo kazi moja tu—ni kumpiga.”

Itaendelea…



Columnist: mwananchi.co.tz