Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ndege ya ATC ilivyotekwa kushinikiza Nyerere ajiuzulu-7

29508 Pic+ndege TanzaniaWeb

Fri, 30 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Baada ya maandalizi yote ya usalama na ndege kutua Uwanja wa Stansted, watekaji walianza kuzungumza na balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Anthony Nyaki.

Kama ilivyoelezwa awali, kwa kutumia umahiri wake wa kidiplomasia, Balozi Nyaki aliwazidi hoja watekaji ambao waliamua kumuomba awawezeshe kuongea na aliyekuwa waziri aliyehusika na tawala za mikoa, Oscar Kambona na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Peter Alexander Rupert Carington.

Lakini uzito wa hoja za Balozi Nyaki uliwafanya waone kimbilio pekee lilikuwa ni Kambona, ambaye alipoongea nao hakutaka kuonekana alihusika na utekaji huo na ndipo vijana hao watano walipojisalimisha.

Soma zaidi: Ndege ya ATC iliyotekwa kushinikiza Nyerere ajiuzulu (6)

Vijana walioteka ndege hiyo walikuwa Mussa Memba, aliyekuwa na umri wa miaka 25, Mohamed Ali Abdallah (26) na nduguye Abdallah Ali Abdallah (22), Mohamed Tahir Ahmed (21) na Yassin Memba (21).

Baadaye kulitokea taarifa mbili za kutegwa mabomu kwenye ndege mbili za ATC, ambazo zilionekana hazikuwa za kweli, na wala hazikuwa na uhusiano wowote na utekaji wa ndege aina ya Boeing 737 uliofanyika Februari 26, 1982.

Hata hivyo, kilichoonekana dhahiri ni kuwa matukio hayo mawili yalitokea katika muda usiozidi kipindi cha mwezi mmoja na yaliyofanana, yalihusu siasa.

Soma zaidi: Ndege ya ATC ilivyotekwa kushinikiza Nyerere ajiuzulu (5)

Ingawa maofisa wa Serikali waliendelea kusisitiza kuwa yalifanywa na wahuni, maofisa wa usalama pamoja na polisi waliwekwa katika hali ya tahadhari muda wote.

Madai ya kwamba vijana walioteka ndege hiyo walikuwa wahuni yaliendelezwa na baadhi ya vyombo vya habari vya ndani. Vyombo vya habari vya nje havikulichukulia jambo hilo kijuu-juu.

“Vijana hao walikuwa wakionekana wakizurura mjini Dar es Salaam bila kazi, na inawezekana walikuwa wavuta bangi,” liliandika gazeti la Uhuru toleo Na. 5835.

Gazeti hilo lilimkariri mtu mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe, akisema: “Vijana hawa walikuwa wakirandaranda hapa Kariakoo na jinsi walivyokuwa wakizungumza maneno ya ovyo, tuliwachukulia kuwa ni wavuta bangi.”

Mtu mwingine ambaye naye hakutaka jina lake litajwe gazetini, aliliambia gazeti hilo akisema: “Baadhi ya vijana hao walikuwa wakionekana mara kwa mara katika eneo la Magomeni ... lakini walitoweka wiki chache zilizopita.”

Ingawa mambo yalionekana kuwa kimya, upelelezi wa hali ya juu ulifanyika kutafuta ni kitu gani kilichokuwa nyuma ya mfululizo wa matukio yanayofanana katika kipindi kimoja.

Wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere alifikia uamuzi wa kutowarejesha nchini wale watekaji watano waliokuwa wanashikiliwa Uingereza ili washitakiwe na kuhukumiwa. Kama ilivyokuwa kawaida, mawazo yake aliyabeba mwenyewe kwa kuona kuwa ni busara wakasikika katika mahakama za nje ya Tanzania kuliko za Dar es Salaam.

Mwalimu Nyerere pia, kwa wakati huo, alianza kupatana na Waziri Mkuu wa Uingereza, Margaret Hilda Thatcher, kuliko wakati mwingine wowote uliotangulia na aliwahi kusema ni “kwa sababu ya utawala wake wa sheria”.

Kwa mujibu wa jarida la African Defence Journal, Rais Nyerere alimuomba balozi wa Uingereza mjini Dar es Salaam, Peter Moon kufikisha shukrani zake binafsi kwa Waingereza, hususan kwa Waziri Mkuu Thatcher, kwa kazi aliyoifanya ya kuwashughulikia ‘wahuni’ walioiteka ndege ya Tanzania.”

Kwa hakika huo utekaji wa aina yake ulikuwa ni wa tatu.

Kuhusika kwa Serikali ya Tanzania katika kuteka ndege kulianza mwaka 1972 wakati wakimbizi wa Uganda walioukimbia utawala wa Idi Amin, wakisaidiwa na Watanzania, walijaribu kumrejesha Dk Milton Obote madarakani.

Sehemu ya uvamizi huo, kwa mujibu wa jarida la Africa Contemporary Record ni kuchukua ndege iliyojaa ‘waasi’ ili itue Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe. Ili kufanya mpango huo uwezekane, maofisa wa Uwanja wa Dar es Salaam waliamriwa kufumba macho wakati rubani wa Uganda “akiiba” ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Mashariki kutoka uwanjani hapo.

Alhamisi ya Septemba 14, 1972, kwa mujibu wa ukurasa wa 47 wa kitabu cha Terrorism in Africa, ndege ya Shirika la Afrika Mashariki iliibwa usiku na rubani asiyejulikana kwenye Uwanja wa Dar es Salaam.

Baadaye ndege hiyo ilikutwa kwenye Uwanja wa Kilimanjaro ikiwa imepasuka matairi. Ndege hiyo ilitekwa kama ilivyokuwa imepangwa na watekaji hao, ikaondoka Dar es Salaam kuelekea Kilimanjaro ambako ingewabeba hao waliopangwa, lakini ikatua vibaya ikapasua matairi yake, na mpango wote ukaishia hapo.

Itaendelea kesho

Soma zaidi: Ndege ya ATC ilivyotekwa mwaka 1982 kushinikiza Nyerere ajiuzulu (4)



Columnist: mwananchi.co.tz