Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ndege iliyotekwa mwaka 1982 kushinikiza Nyerere ajiuzulu-3

28869 Ndege+pic TanzaniaWeb

Mon, 26 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ikiwa kwenye uwanja huo wa ndege jijini Nairobi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Dk Robert Ouko alijadiliana na watekaji hao. Tanzania ilimteua waziri wake wa Mawasiliano na Uchukuzi, John Samuel Malecela, kushughulikia utekaji huo.

Akiwa jijini Nairobi, Waziri Malecela aliwaambia waandishi wa habari kuwa watekaji hao walimtaka Mwalimu Nyerere ajiuzulu, lakini aliporejea Dar es Salaam alisema watekaji hao hawakutoa madai yoyote.

Akiwa kama kiongozi wa kushughulikia utekaji huo, Waziri Malecela alitoa taarifa hizo hizo kwa Mwalimu Nyerere: “Watekaji hawakutoa madai yoyote.”

Kwa kuwaamini maofisa wake, Mwalimu Nyerere aliamini pia hata kile walichomwambia kuhusiana na utekaji huo.

Maofisa wa Serikali ya Tanzania waliopiga kambi nyumbani kwa Mwalimu Nyerere, kulingana na taarifa walizokuwa wakipokea, walianza kuchukulia kuwa utekaji huo haukuwa na shabaha zozote za kisiasa. Kwa kuwa baadhi yao hawakujua kisa halisi cha kutekwa kwa ndege hiyo, walibuni vya kwao.

Walianza kuambizana wenyewe kwa wenyewe, na wakamwambia na Mwalimu Nyerere pia, kwamba ‘inawezekana’ watekaji hao walikuwa wameiba kiasi kikubwa cha dhahabu na almasi ambazo walitaka kuzitoa nchini.

Waliamini pia kwamba walitumia utekajij huo kuvusha mali hizo na kwamba familia ya Kiarabu iliyotaka kwenda Dubai kwa kupitia Mombasa ilikuwa ni sehemu ya utekaji huo.

Namna jambo hilo lilivyoshughulikiwa lilizua maswali mengi sana nchini Kenya. Kama ilivyoelezwa awali, Dk Robert Ouko alijiingiza katika mjadala wa utekaji huo kwa sababu ndiyo kwanza tu alikuwa ametua uwanjani hapo akitokea kwenye mkutano mjini Addis Ababa na si kwamba alifika uwanjani hapo rasmi kwa sababu ya tukio hilo.

Ilikuwa ni sadfa tu kwamba Dk Ouko alitua uwanjani hapo wakati uleule ambao ndege ya Tanzania iliyotekwa nayo ilikuwa imetua.

Hata hivyo, utekaji huo haukutokea wakati mzuri kwa sababu mgogoro kati ya Kenya na Tanzania kuhusu kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ulikuwa haujapoa.

Mgogoro kati ya Kenya na Tanzania ambao ulioanza taratibu kuanzia mwaka 1974, ulifikia kilele chake mwaka 1977 wakati nchi zote mbili—Tanzania na Kenya—zilipogoma kutoa michango yake ya uanachama wa jumuiya hiyo. Kwa kukosa bajeti yake ya mwaka wa fedha wa 1977-1978, jumuiya hiyo ikafa rasmi Ijumaa ya Julai Mosi, 1977.

Machungu aliyokuwa nayo Mwalimu Nyerere yaliyotokana na kuanguka kwa jumuiya hiyo bado alikuwa nayo. Kitendo cha Kenya kuiruhusu ndege hiyo kuondoka mjini Nairobi kiliongeza idadi ya maswali yaliyoulizwa na hata kutonesha kidonda cha machungu aliyokuwa nayo Mwalimu Nyerere kuhusu jumuiya hiyo. Hata hivyo, Serikali ya Kenya haikujiingiza kwa undani katika kulizungumzia suala hilo.

Wakati sasa watu wakitafakari kilichotokea, ndege ya ‘Kilimanjaro’ ilikuwa ikiambaaambaa angani kuelekea Jeddah, Saudi Arabia. Ilipopata habari, Serikali ya Saudi Arabia iliinyima ndege hiyo ruhusa ya kutua na kwa kuonyesha haikuwa inatania iliufunga uwanja wake.

Lakini, Kepteni Deo Mazula alipowasiliana na wasimamizi wa uwanja huo na kuwaambia kuwa ndege yake imeshasafiri umbali wa kiasi cha maili 1,600 tangu alipoondoka Nairobi na kwamba haikuwa na mafuta zaidi ambayo yangeiwezesha kuendelea na safari nyingine, Serikali ya Saudi Arabia wakaufyata. Wakairuhusu ndege hiyo itue.

Ndege ilitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mfalme Abdulaziz mjini Jeddah. Ruhusa ya kutua kwa ndege hiyo ilikuwa ni kwa ajili ya kujaza mafuta tu. Walinyimwa hata ruhusa ya kufungua mlango wa ndege hiyo.

Wakati huu hali ya hewa katika ndege hiyo ilikuwa imeanza kurejea katika hali yake ya kawaida. Viyoyozi vilikuwa vimeshaanza kufanya tena kazi na watekaji walijaribu kusemezana na watekwaji huku wakiwaambia shabaha yao ya kuiteka ndege hiyo.

Hata hivyo, ujumbe waliokuwa wakijaribu kuutoa haukueleweka sawasawa kwa abiria wa ndege hiyo. Watekaji walijitambulisha kuwa wao ni wanachama wa ‘Harakati za Kidemokrasia za Vijana wa Tanzania.’

Waliwaeleza abiria hao kuwa walitaka Rais Julius Nyerere ajiuzulu kwa sababu “...Watanzania wanaishi katika hali ya shida na hawana chakula.”

Mwisho wa mazungumzo yao waliwaambia abiria kuwa wamekusudia kuipeleka ndege hiyo nchini Marekani. Wakati wakisema hayo, watekaji hao walikumbuka kuwa kuna abiria mmoja alitoa bastola yake walipokuwa Uwanja wa Ndege wa Mwanza na kuikabidhi chumba cha marubani.

Ni utaratibu katika viwanja vya ndege vya Tanzania kwa abiria yeyote kuitoa silaha yake na kuikabidhi kwa wafanyakazi wa ndege hadi mwisho wa safari.

Walipokumbuka hilo, mmoja wa watekaji hao alimfuata Kepteni Mazula na kumtaka awapatie bastola hiyo. Mmoja wao, Mussa Memba alipoipokea alionekana kubabaika kidogo kana kwamba hakuwa na ujuzi wowote wa namna ya kuitumia silaha hiyo.

Alipokuwa amejikunja upande mmoja wa chumba cha rubani akiishika shika bastola hiyo, pengine akiishangaa au kuichunguza, ghafla risasi ilifyatuka. Risasi iliyofyatuka iliuparaza mgongo wa Oscar Mwamaja, rubani msaidizi wa Kepteni Mazula na kumjeruhi.

Baada ya kujaza mafuta kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mfalme Abdulaziz mjini Jeddah, kituo cha tatu kilikuwa ni Athens, Ugiriki. Pamoja na maombi mengi ya Serikali ya Tanzania ya kutaka ndege hiyo ishikiliwe ili isiondoke, maofisa wa Serikali ya Ugiriki walitangaza mapema kabisa, hata kabla Boeing 737 haijatua, kwamba ingeruhusiwa tu kujaza mafuta na kuondoka mara moja bila kuikawiza.

Watekaji: Tunataka Nyerere ajiuzulu - 2

 

Itaendelea kesho…



Columnist: mwananchi.co.tz