Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ndege ilivyotekwa mwaka 1982 kushinikiza Nyerere ajiuzulu

28578 Ndge+pic TanzaniaWeb

Sun, 25 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kutokana na hali ya kisiasa iliyokuwa ikiendelea nchini tangu Tanganyika ilipojipatia Uhuru Jumamosi ya Desemba 9, 1961, wako Watanzania ingawa wachache ambao hawakuridhishwa na uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kiasi kwamba wako waliodiriki hata kuteka ndege ya abiria ya Tanzania kwa lengo la kuishinikiza Serikali kukubaliana na madai yao.

Miongoni mwao ni vijana watano walioteka ndege aina ya Boeing 737 ya Shirika la Tanzania (ATC) aina, Boeing 737 ikiwa mjini Mwanza.

Huo ulikuwa ni utekaji wa kwanza wa aina yake tangu ATC lilipoanzishwa Ijumaa ya Machi 11, 1977 baada ya kuvunjika kwa Shirika la Ndege la Afrika Mashariki (EAA) Januari 1977 na kisha kufa rasmi Jumanne ya Februari 1, 1977.

Utakaji wa ndege hiyo ulikuja siku moja baada ya kutekwa kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kuwait, Alhamisi ya Februari 25, 1982. Ndege hiyo ilitekwa katika ardhi ya Beirut, Lebanon ikirejea kutoka Libya. Ilikuwa na abiria 150.

Pamoja na kwamba utekaji wa kwanza wa ndege katika anga la Tanzania ulifanyika mwaka 1972 na mwingine ukafanyika mwaka 1979, huu wa Februari 1982 ulikuwa wa kipekee kabisa na—ingawa ulikuwa ni utekaji uliohusiana na siasa—Serikali ya Tanzania haikutaka ijulikane hivyo.

Ilivyokuwa

Saa 11:00 jioni ya Ijumaa ya Februari 26, 1982, baada ya kuagana na ndugu, jamaa na marafiki, abiria kutoka Uwanja wa Ndege wa Mwanza waliingia katika ndege ya ATC iliyokuwa na jina la Kilimajaro ubavuni mwake.

Kwa wasafiri wengi, Uwanja wa Ndege wa Mwanza haukuwa na sifa nzuri kutokana na kukosa usalama kiasi cha baadhi ya marubani kuutaja kama “kituo cha basi”.

Kulikuwa na makundi ya kawaida ya watu uwanjani hapo kama ilivyokuwa siku zote kwa wasafiri wa Mwanza—Dar es Salaam. Wengi wao walikuwa ni wale wenye asili ya India, Waarabu na wazawa wachache. Pamoja na kwamba mambo yote yaliyonekana kuwa ya kawaida, kulitokea jambo dogo ambalo liliifanya safari ya ndege hiyo isiwe ya kawaida.

Boeing 737 ilipaa angani saa 11:20 ikielekea Dar es Salaam na ilitarajiwa kuwa ingetumia dakika 90, kutembea umbali wa takriban maili 500 kufika, lakini ikageuka kuwa safari ya juma zima na umbali wa kiasi cha maili 9,500—tena wakati wote abiria na wafanyakazi wa ndege hiyo wakiwa chini ya ‘mtutu wa bunduki’.

Dakika tano tu baada ya ndege hiyo kupaa angani, vijana wanne walisimama ghafla kwa wakati mmoja. Mmoja wao alijipenyeza kwa kasi hadi chumba cha rubani, kisha akaelekeza ‘bastola’ yake kwenye kichwa cha mmoja wa marubani, Kapteni Deo Mazula, na kumuamuru awapeleke Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta, Nairobi.

Baadaye ilikuja kujulikana kuwa majina ya watekaji wale ni Mussa Memba (25), Mohamed Ali Abdallah (26) na nduguye Abdallah Ali Abdallah (22), Mohamed Tahir Ahmed (21) na Yassin Memba (21). Ilikuja kujulikana pia kuwa kiongozi wao alikuwa ni Mussa Memba.

Wakati huohuo, watekaji nyara wengine, huku wakipunga ‘bastola’ bandia zilizotengenezwa kwa vigogo vya miti na ‘mabomu’ ya kutupwa kwa mkono, waliwatangazia abiria kuwa wao ni viongozi wa ‘Vijana wa Harakati za Mapinduzi Tanzania’ na kwamba shabaha yao ni “kuhakikisha kuwa Rais Julius Nyerere anajiuzulu”.

Wakati hayo yakitokea, Mwalimu Nyerere alikuwa Ikulu jijini Dar es Salaam akijiandaa kurejea nyumbani kwake baada ya kupokea risala kutoka kwa chipukizi waliomuahidi kuwa wataendelea “kuwa watiifu, wakakamavu na wenye bidii kwa kuwa tunafahamu mchango wetu unahitajika sana katika ujenzi wa nchi”.

Hadi wakati anaondoka ofisini kurejea nyumbani kwake akiwa amefurahishwa na risala iliyosomwa na mwenyekiti wa Taifa wa chipukizi, Frank Uhahula (15) wa darasa la saba katika Shule ya Msingi ya Tumbi, Kibaha mkoani Pwani, Mwalimu Nyerere hakuwa amejua kile kilichotokea upande mwingine wa nchi.

Mara baada ya watekaji hao kuanza purukushani katika ndege hiyo, waliwaamuru abiria wote wakae kimya kwenye viti vyao na wafumbe macho na kwa sababu ambazo hazikujulikana mara moja lakini za kustaajabisha, waliwalazimisha wafanyakazi wa ndege hiyo kuzima viyoyozi.

Wakati huo ndege ilikuwa ikiambaa angani kuelekea Kenya. Hali ya hewa katika ndege hiyo ilipoanza kuwa nzito na kukaribia kutovumilika tena, ndege ilitua Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi.

Hata hivyo, katika kipindi cha dakika kadhaa baada ya kutua, Mwalimu Nyerere alipewa taarifa kuhusu utekaji huo na kuambiwa kuwa tayari imeshatua Nairobi.

Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, John Samuel Malecela, wakati huo akiwa na miaka 48, aliteuliwa rasmi kushughulikia sakata la utekaji huo na mara moja aliondoka kwenda Kenya.

Mwalimu Nyerere alitaka kuwa na uhakika kwamba Serikali ya Kenya hairuhusu ndege hiyo iondoke katika ardhi yake.

Wakati hayo yakiendelea, polisi wa Kenya waliufunga Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta, pia wanajeshi kusambazwa kuuzingira uwanja.

Itaendelea…



Columnist: mwananchi.co.tz