Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Namna ya kufanya kazi katika mazingira yenye uadui

65771 Kazi+pic

Sat, 6 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Umewahi kupata wazo kuwa kuna mtu kazini kwako hana nia njema na wewe? Je, wakati mwingine unahisi kuna watu fulani unaofanya nao kazi ni wabaya wako?

Inawezekana isiwe uadui wa moja kwa moja lakini kuna ile hali ya kutokuamini wenzako.

Unajisikia hauko salama. Unapomsikiliza mtu lakini hujui ni wakati upi uamini kile anachokisema.

Kwa upande mwingine, inaweza kuwa mazingira ya watu kusemana vibaya, kuchongeana, kutengenezeana fitina za kuchafuliana, kuviziana na majungu yanayolenga kueneza maneno yasiyo kweli dhidi ya wengine.

Haya yote ni mazingira ya uadui kazini. Matokeo yake yanaweza kuwa sonona, chuki, wasiwasi na kutokujiamini.

Huwezi kuwa na amani unapofanya kazi kwenye mazingira ya namna hii. Ufanyeje? Napendekeza mbinu tano.

Pia Soma

Jipambanue unaamini nini

Ofisi unayofanyia kazi inaweza kuwa na utamaduni wa kuzungukana, kufanyiana fitina na kuviziana. Kushiriki fitina hizi kunaweza kukuchimbia kaburi lako mwenyewe. Jipambanue.

Kama mwenzako anakueleza jambo unalohisi ni majungu, usiishie kusikiliza na kuondoka. Mwambie huamini kinachosemwa na ikiwezekana mpe mfano chanya unaobatilisha kile anachotaka ukisikie. Kwa kufanya hivi, siyo rahisi mtu huyu kukurudia tena.

Pia, ni vizuri kuwa wazi kadri inavyowezekana. Unapoombwa kushiriki jambo unaloamini siyo sahihi, sema pale pale. Utajipunguzia matatizo msimamo wako ukifahamika.

Jiwekee mipaka

Unapokuwa kwenye mazingira ambayo hujui umwamini nani, hujui nia ya watu wanaokuzunguka, mipaka ni hatua ya kuanzia. Angalia namna unavyoweza kuishi maisha ya faragha yasiyoingiliana sana na watu bila sababu.

Unaweza, kwa mfano, kutumia muda wako wa ziada kazini kufanya vitu unavyovipenda kama muziki, vitabu, kusoma au kusikiliza hotuba. Fanya kile kinachokukuza.

Ikiwa tatizo ni bosi wako anayeamini anaweza kukuagiza kufanya majukumu ya kazi hata katika muda wako wa mapumziko, unapigiwa simu saa yoyote, unaandikiwa barua pepe inayokutaka kushughulikia jambo ambalo ungeweza kulifanya wakati wa kazi, mipaka ni muhimu.

Kama siyo dharura sana, kwa nini usome na kujibu barua pepe, kupokea simu za kazini unapokuwa nyumbani? Haiwezekani watu kufahamu kuwa unapokuwa nje ya ofisi hupatikani? Jifunze kusema hapana. Kwa mfano; kikao kimepangwa nje ya majukumu yako, hakuna ubaya kusema una udhuru kuliko kuhudhuria huku ukilalamika.

Chagua wachache wa kuwaamini

Unaweza kuwa kwenye mazingira ambayo huna hakika uzungumze nini na nani. Katika mazingira kama haya, tafuta watu wako wa karibu unaowaamini uzungumze nao mambo yanayokusumbua.

Wabaini marafiki zako, mwenzi wako, watu wakomavu kazini, ambao kila unapokuwa na changamoto unaweza kuwafuata na kuzungumza nao kupata mawazo. Kwa upande mwingine, kuna uwezekano wa watu ‘wanaokuamini’ kukufuata wakueleze mambo ambayo usipokuwa makini yanaweza kukufanya ukaonekana unahusika na maneno maneno ya koridoni.

Mbinu hapa ni kumsikiliza mtu anayekueleza mambo yake bila kulazimika kutia neno. Epuka kutoa ushauri kama siyo lazima. Kumsikiliza mtu bila kutia neno inaweza kuwa msaada na itakuepusha na mengi.

Ishi kiungwana, fanya kazi kwa bidii

Wakati mwingine hakuna sababu ya kupambana na wabaya wako. Kama mtu anakufanyia vituko, kumtendea vivyo hivyo hakutatui tatizo. Kwa nini usifikirie kuwa muungwana na ukaendelea na maisha yako?

Ingawa kwa haraka mbaya wako anaweza kuhisi umekuwa dhaifu kwa kushindwa kukabiliana naye, saa nyingine kumtendea mema aliyekutendea ubaya kunaweza kumfundisha vizuri zaidi.

Kadhalika, badala ya kufikiria namna ya kukabiliana na mtu anapenda kuvizia makosa ya wengine, kwa nini usifanye majukumu yako kwa bidii?

Kama kuna kitu kinahitajika kufanyika, kifanye kwa usahihi achana na majibizano yasiyo na msaada. Ukijijengega utamaduni wa kutimiza majukumu yako, hatimaye, watu watakuja kugundua kuwa unaongeza thamani kwenye kampuni na watakuheshimu.

Siyo lazima kuondoka

Siyo mara zote adui hukimbiwa. Kuna nyakati kuishi na adui kunaweza kuwa na faida kubwa kuliko kuzungukwa na marafiki.

Adui anaweza kuwa kichocheo cha kufikiri mambo mara mbili mbili kabla ya kufanya uamuzi.

Katika mazingira kama haya, kuwa na mipango ya muda mrefu ya kujikuza kiujuzi inaweza kuwa ufumbuzi. Kwa nini, kwa mfano, usifikirie kujiendeleza? Kajiandikishe masomo ya masafa kulingana na ratiba yako. Mitandaoni kuna kozi nyingi unazoweza kuzisoma kwa muda wako wa ziada na ukajenga weledi huku ukiendelea na kazi.

Kwa kufanya hivyo, unaweza kujiwekea mazingira mazuri ya kuondoka baadae.

Lakini hata hivyo, kazi unayofanya haipaswi kuzidi umuhimu wa maisha yako na familia yako.

Kuna sababu gani ya kutumia nguvu nyingi kupambana na mazingira mabovu kazini kwa gharama ya kuwa mbali na familia yako? Kuna nyakati unalazimika kuchagua kilichomuhimu zaidi.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU), Moshi. Twitter: @bwaya, 0754 870 815

Columnist: mwananchi.co.tz