Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

NYUMA YA PAZIA: Iwe Anfield au Etihad, lakini anayeumia yupo Old Trafford

Pep Na Klopp Klopp na Pep Guardiola

Sun, 22 May 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Upo Melbourne Australia au Praia Cape Verde ama Njombe Tanzania. Umekaa sebuleni, rimoti mkononi. Korosho kando yako. Pambano ni kati ya Manchester City dhidi ya Aston Villa. Wewe ni shabiki wa Manchester United. Unataka timu gani ishinde?

Unatamani bao la majeruhi la Aston Villa ambalo litaipa sare? Kule Merseyside unatamani Liverpool ampige Wolves na kutwaa ubingwa? Au unatamani Kelvin De Bruyne apige hat trick nyingine dhidi ya Villa na kuipa Manchester City ubingwa wa pili mfululizo. Ni swali gumu kwa shabiki wa United anayejielewa.

Shabiki wa United aliyekulia nchi za Kiingereza atapata wakati mgumu na swali hili. Miujiza ikitokea Liverpool anaweza kushinda dhidi ya Wolves pale Anfield, halafu City akatoka sare dhidi ya Aston Villa na hivyo Liverpool kutawazwa kuwa mabingwa. Unadhani shabiki wa United atakenua meno yake kwa furaha?

Endapo hilo likitokea basi Liverpool watakuwa wameifikia Manchester United kileleni mwa orodha ya timu iliyotwaa mataji mengi zaidi England. Mpaka sasa United wana mataji 20 wakati Liverpool wana mataji 19. Linasubiriwa taji moja tu kwa Liverpool kuifikia Manchester United.

Kwa miaka mingi Liverpool walikuwa na mataji 18 huku Manchester United wakiwa na mataji saba tu. Aliyechafua hali ya hewa alikuwa ni Sir Alex Ferguson wakati alipoingia Old Trafford.

Alitwaa mataji 13 ya Ligi Kuu ya England huku Liverpool ikiwa imesimama pale pale. Na aliwaambia wazi waandishi wa habari wakati akitambulishwa Carrington 1986 kwamba lengo lake lilikuwa kuing’oa Liverpool kileleni.

Hatimaye zama zikapishana. Liverpool wakaganda walipo na United wakachukua kila kukicha. Kuja kushtuka United kawa na mataji 20.

Taji lao la mwisho walichukua 2013 ukiwa ni msimu wa mwisho wa Sir Alex Old Trafford. Tangu hapo

hawajachukua tena. Lakini msimu uliopita Liverpool wakachukua taji la 19. Ni baada ya miaka 30 tangu wagande na taji la mwisho la 18 mwaka 1991.

Endapo maajabu yakitokea kesho Pale Etihad halafu City ikafungwa au ikadroo basi Liverpool wataifikia United. Hiki kitu kinaumiza kwa mashabiki wa United hasa wale waliozaliwa na kukulia England huku wakiona ushindani wa mataji wa mahasimu hawa.

Kumbuka kinachowafanya wawe mahasimu sio jiografia ya miji yao, hapana. Ni historia za mafanikio hayo.

Mbaya zaidi kwa mashabiki wa United ni kwamba nje ya mafanikio ya England, Liverpool bado wapo juu yao.

Liverpool wana mataji sita wakati Manchester United wana mataji matatu tu. Ina maana kama Liverpool wakitwaa taji wikiendi hii basi watakuwa timu yenye mafanikio zaidi katika soka la England

Kama shabiki wa Manchester United amekaa sebuleni Tokyo - Japan kwanini ashangilie Liverpool kuchukua ubingwa mbele ya City? Haiwezekani. Hakuna asiyetaka kuwa namba moja daima.

Lakini hapohapo tugeukie upande wa pili. Kuna hawa watani wa United. Manchester City. Hawa ndio ambao wanatoka nao mji mmoja. Wanachangia pamoja sebule za familia, mabomba ya maji, baa, vyoo na kila kitu.

Sidhani kama United wanatamani City wachukue ubingwa. City wanapochukua ubingwa kelele zote zinawaangukia wao. Masimango yote yanawaangukia wao.

Zamani Sir Alex alipenda kuwaita noisy neighbours yaani majirani wenye kelele. Wao furaha yao ilikuwa kuifunga Manchester United tu. Katika mataji hawakuwahi kufanana. Ilikuwa mbingu na ardhi. Lakini walikuwa wanawasumbua zaidi katika mechi za watani. Derby.

Lakini sasa kibao kimebadilika. Tangu City wanunuliwe na Waarabu 2008 wametwaa mataji matano ya England wakati United wametwaa mataji matatu. Na hapana shaka kuna asilimia kubwa wakatwaa taji la sita kesho jioni. Kibao kimebadilika na zile kelele ambazo Sir Alex alikuwa anazilalamikia zimezidi mara mbili. United ya leo inadhalilishwa uwanjani na City, kisha hapo hapo inadhalilishwa katika mataji.

Najua mashabiki wa United waliopo Tanzania hawana shida na City kuchukua ubingwa lakini wale waliopo Uingereza ambao wanaamini upinzani wa timu hizi mbili wanajua karaha ambayo italetwa na mashabiki wa City ambao wanaishi nao kila siku. Wiki moja iliyopita nilikuwa Hispania kushuhudia pambano la watani kati ya Atletico Madrid na Real Madrid ambayo ilishachukua taji. Ungeweza kuona huzuni iliyotanda kwa mashabiki wa Atletico.

Lakini kinachokera zaidi vilevile ni kwamba licha ya kwamba ni ndoto kwa City kufikia mataji ya United, lakini pengo lililopo baina yao ni kubwa kwa sasa. Nazungumzia pengo la kiuwezo baina ya wawili hawa. Ni kubwa na wakati mwingine linatia aibu. Ukiitazama Manchester United hii ya Harry Maguire kisha ukaitazama Manchester City ya Kelvin De Bruyne unajiuliza, nyakati zimekwenda wapi?

Ukitazama kile ambacho United wamefanywa mwaka huu na City nyumbani na ugenini ungejiuliza namna gani United wameruhusu pengo hili likue kila siku. Ilianzia pale ambapo Sir Alex mwenyewe alidhibiwa mabao 6-1 nyumbani kwake Old Trafford kabla hajastaafu. Sasa hivi pengo hilo limekuwa kubwa kiasi kwamba ni kitu cha kawaida City kucheza pambano la fainali Ligi ya mabingwa huku United wakicheza Europa.

Shabiki halisi wa United kwa sasa nafsi yake haijielewi. Hataki ubingwa uende Liverpool kwa sababu ya ugomvi wa mataji baina yao. Lakini hataki ubingwa uende kwa City kwa sababu ya zile kelele ambazo Sir Alex alikuwa akizungumzia. Sasa hivi zile kelele zimezidi maradufu.

Nadhani kwao kwa sasa ni bora achukue Arsenal au Chelsea. Watapumua. Lakini kwa hawa wawili nadhani shabiki wa United atasikia maumivu ya kichwa taratibu. Unapozingatia kwamba wanacheza pambano lao la mwisho wakiwa hawawezi kuingia hata Top Five basi hapo ndipo roho zinapouma zaidi.

Columnist: www.mwananchi.co.tz