Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

NDANI YA BOKSI: Nini Mayele...Kuna King Samatta wa Lubumbashi

Mbwana Samatta Mbwana Samatta

Sun, 10 Jul 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

George Mpole ndiye mfungaji bora wa msimu uliopita. ‘Kesi imeisha’! Lakini tuzo yake imekuwa na mambo mengi nje ya uwanja. Nje ya Mpole na timu yake ya Geita Gold. Siasa za Kariakoo zimeteka kila kitu.

Siyo jambo kubwa! Lakini ukubwa ni kwa sababu ya mitandao na vyombo vya habari. Kulitumia jambo hili ili kuendesha kazi zao za kila siku. Nani atakusikiliza na kusoma bila kugusia hili la Mpole?

Tumekuwa watu wa kutambaa na matukio, kuanzia mtaani, mitandaoni, siasa na michezo. Lakini tatizo kuu ni kwenye soka. Na tuliowategemea watuweke sawa ndo wanatuvuruga zaidi.

Wachambuzi wanaaminika sana siku hizi kuliko hata TFF. Na pengine hata kuliko makocha na viongozi wa timu. Na hili halijaja kwa bahati mbaya, ni jambo lililotengenezwa kutokana na mazingira yetu ya soka.

Mazingira na mambo yanavyoenda kwenye soka. Ndo Chamazi kikuu cha wachambuzi kuwa na nguvu hii, kuliko watendaji wa vilabu na taasisi za soka. Siku zote anayemulika ndiye anayeaminika.

Wachambuzi ni kama unge, lilee la Samuel Sitta (RIP). Kazi yao kukosoa uendeshwaji wa soka letu. Ingawa ni ngumu kusoma au kusikia sehemu wakishauri nini kufanyike. Wanapiga mawe tu.

Kiasili binadamu hupenda kusikia baya kuliko zuri. Na hapa nipo nguvu ya wachambuzi ilipoteka. Kwa kutoa mapungufu ya vilabu na taasisi zake, ikafanya waaminike, wapendwe na kufuatiliwa.

Leo wanafuatiliwa zaidi kuliko soka lenyewe. Wana mashabiki wengi kuliko wachezaji wenyewe. Kila kitu huanzia na kuishia kwao, na baadhi ya viongozi wa soka wametekwa na wao.

Uaminifu na ushabiki wa mashabiki wa soka kwa wachambuzi. Inapaswa uheshimiwe, uogopwe na kulindwa na wachambuzi wenyewe. Bahati mbaya wachambuzi wengi hawajui dhamana waliyonayo.

Kwa tabia na akili za mashabiki wa soka. Wachambuzi wana dhamana kubwa sana na soka letu. Wanaweza kutupeleka motoni ama kwenye pepo ya soka kupitia chambuzi zao. Yes! Tunaimba wanachoimba.Siyo Karia, Senzo, Barbara au Tenga. Waliofanya shabiki wa soka Bongo, ajue kwanini Iniesta au Xiav hakuwa mchezaji bora mbele ya Leo Messi au Ronaldo. Hii kazi kwa asilimia mia ilifanywa na wachambuzi.

Lakini dhamana yao imeanza kuingia doa kwa kuchezewa. Wanaochezea ni wao wenyewe, kwa ujumla wao au kwa walio wengi. Wakiendelea hivi watalipeleka soka sehemu ambayo itachukua miaka mingi kukaa sawa.

Ni wao waliofanya tuamini bila Manji, Yanga itajiendesha na kubwa klabu tajiri. Baada ya Manji kusepa, ni wao pia wakasema ni wakati wa Yanga kuiga kwa Simba, na kumsaka Mo wao pale Jangwani (muwekezaji). Wachambuzi!

Kwa maandishi na sauti zao walitupa sababu za umuhimu wa ‘profesheno plea’ kwenye ligi yetu. Wakidai uwepo wao utainua vipaji vya wazawa na kuongeza chachu na kuitangaza ligi yetu. Walikuwa sahihi sana hapa, leo ni ligi maarufu zaidi ukanda huu.Leo ni wanaotuaminisha kwamba tulinde vipaji vya wachezaji wazawa. Kwa kuwachangia pesa wakifanya vizuri. Lakini nyuma walioponda sana tabia za mabakuri na kutaka timu na wachezaji wawekeze.Ushauri wa wachambuzi mara nyingi ni bora na pia hufuatiliwa sana. Ndo maana kurasa zao mitandaoni zina ufuasi mkubwa. Hili litoshe kukupa picha kuwa wachambuzi wanaenda kuwa wakubwa kuliko soka letu.

Kuna mawili, wachambuzi au soka letu mmoja wao ataneemeka zaidi. Kumbuka wachambuzi wana mvuto kuliko miguu ya Ibrahim Ajibu. Yes! Na hawategemei matukio ya Sokoine na Jamhuri pekee ili wachambue. Wachambuzi waliomponda kinoma Ditram Nchimbi, kwa makosa yake uwanjani. Ndo wanaombembeleza kinomanoma kila siku Ajibu azingatie soka. Na hata mashabiki wanaamua kupita njie zile zile za wachambuzi.

Nenda mitandaoni. Mashabiki wengi husema “Ukimtazama Chama utaona soka kitu chepesi, lakini ukimtazama Nchimbi utajua soka ni kazi ngumu kuliko kilimo.” Hizi lugha zililetwa na wachambuzi wenyewe kwa dhihaka zao..

Wachambuzi wanatueleza kwamba, Mpole anastahili sifa zaidi na zaidi Kwa kuwa kachezea mechi zake nyingi kwenye viwanja vibaya. Tofauti na wale wa Simba na Yanga ambao wao mechi nyingi wanachezea pale Taifa.

Lakini ni hawa hawa jamaa, ambao misimu ya nyuma walituaminisha Chama ni bora zaidi. Kwa pasi zake za magoli ambazo nyingi alizipiga akichezea uwanja mzuri wa Taifa. Lakini akienda mikoani si lolote si chochote.

Hata hili la George Mpole na Mayele, ni kelele za wachambuzi. Wanapiga kelele badala ya kuchambua. Kibaya zaidi wanafanya haya wakiwa katika kelele cha kuaminika sana na watu haswa wale machizi soka. Kama wachambuzi wangesimama katika kona yao. Hizi tabia za watu ‘kubalansi’ Usimba na Uyanga hata kwenye timu ya taifa zingekufa. Hili lipo ndani ya uwezo wa wachambuzi wetu kama wakiamua.

Akili zao sasa zipo kwenye dili, kama followers, umeneja, uwakala, Ubalozi na teuzi. Hizi zinawapa zinawapa kichaa wengi na kujikuta wakifanya vitu nje ya weredi wa kazi zao. Ndiyo! Na hili liko wazi.Wakala au meneja akiwa mchambuzi kwa wakati mmoja unategemea nini?

Anaanzia wapi kukosoa mapungufu ya mtu wake, mteja au anayemuuzia mchezaji? Hizi zote huleta ‘drama’ na kelele kwa wachambuzi.

Bahati mbaya wao huona sifa sana kutojulikana ushabiki wao. Wakati Wazungu tunaowaiga. Wachambuzi wao wako wazi kishabiki, lakini likija suala la kazi ushabiki kukaa kando. Sasa njoo kwa hawa wanaofanya siri ushabiki wao.

Wanafanya siri, lakini wanafanya yale yale ya mashabiki. Hii inaharibu sana na kuondoa uzito wa kazi yao. Ajabu Ally Mayai na Amri Kiemba, wao huaminika na dunia nzima inajua ni wanazi wa timu gani Bongo.

Wanaoficha ushabiki wao ni wanafki. Kimsingi wapo kwa maslahi yao na siyo soka. Ndo hao ambao hufanya mambo ya sirini ili kufaidika kwenye pande zote. Wakati watu wakijua unakuwa safi zaidi.

Ni wakati wa wachambuzi kuanza kuchambuana. Wajitenganishe ili kuwe na ‘daraja’ kabla ya kubatizana majina ya ‘uchambuzi’. Hii ikiachwa kama ilivyo itapelekea akili za hawa mashabiki wa soka kuingia shimoni na zisirudi.

Leo hii unaweza kumsikia shabiki anamtusi mchezaji. Ukimuuliza kosa lake hajui ila alimsikia mchambuzi flani akiponda uwezo wake. Ni kama watoto ambao huongea au kutenda wanachoona kwa wakubwa. Mpole ndiye mfungaji bora. Kwisha! Tumpongeze kama mchezaji tu. Hizi kauli za uzalendo zinatokea wapi? Tunataka nini? Kulikuwa na sababu gani sasa ya kupigania ‘profesheno’ wawepo kwa kauli hizi?

Sipingi matumizi ya neno uzalendo. Ni jambo zuri kuwatia morali vijana wetu. Lakini tukumbuke wakati tuna Mpole na Mayele Bongo, miaka ya nyuma kulikuwa na Mputu na ‘King’ Samatta pale Lubumbashi, bila neno ‘Uzalendo’.

Columnist: www.mwananchi.co.tz