Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

NDANI YA BOKSI: Godzilla mwambie Ngwair bado tunammiss kitaa

42114 Pic+box NDANI YA BOKSI: Godzilla mwambie Ngwair bado tunammiss kitaa

Mon, 18 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tabu? Hapana, kila mtu hapendi tabu ila Ngwair alizichukia zaidi. Hata ukisikiliza nyimbo zake nyingi aliongelea bata. Kujirusha huku akisisitiza namna ya kuwatumia vyema warembo. Akiwaita midudu ya kupiga mikasi. Shida na matatizo yetu aliwaachia kina Profesa Jay waongelee.

Si kwamba hakuwahi kuimba nyimbo zenye jumbe mbalimbali. Ila starehe, mitungi, kujirusha na kumiliki viumbe bora sampuli ya kina Irene Uwoya. Ndicho kitu alichopenda kuwaimbia watu na jamii ikamuhusudu. Alisimamia alichopenda na kufanikiwa kuteka watu.

Kwa nini alipendwa na masela, mabrazameni, masister duu na watu wa kawaida? Kwa sababu kama binadamu alikuwa mchanganyiko wa vitu kadhaa. Vitu vilivyolazimisha akubalike na jamii pana. Kipaji halisi ubora wake na kuishi maisha rahisi kuliko urahisi wenyewe.

Muonekano na uhalisia wake Ngwair alikuwa msela kama masela wengine. Pia alipenda maisha mazuri na ndicho alichoabudu katika misele yake. Aliwaimbia madem huku akiwatia hasira wana kitaa kwa kusaka mahela. Na zaidi alikuwa fundi mnoo.

Muulize Ngosha ‘Fid Q’ kilichomtokea kwenye wimbo wa CNN alioshirikishwa na Ngwair. Kwa kujiamini zaidi Ngosha akaamua kuanza yeye kuingiza ‘voko’ kwenye ‘biti’ ya P Funk na Q The Don. Alipomaliza yeye akawasha ‘embasi’ yake akisikilizia zamu ya Ngwair.

Ngwair alipoingia kwenye chumba cha kuingizia sauti. Suruali yake ikikosa ushirikiano na kiuno na kulegea kwenye makalio kama nyaya za TTCL. Akaiweka sawa ‘maiki’ huku akisubiri Majani aachie ‘biti’ kisha apite nayo kikatili. Studio ndo sehemu pekee aliyoihusudu Ngwair.

Bastola cash and, toa code someka, wapi ilipo bata wapi leo kinaeleweka, nna pesa mingi mpaka natamani jiteka... then watu wapo King Stone ka Jamaica... Ni ma model, madodo waku roll na ma Gangsta... Divas and Hustlers, Paper Chasers! Nani anaweza piga ngoma kali ka hii? Me! Nani anaweza gonga beat nzito kama hii? P! Yeah you know that ni Bongo Records... true na Q East Zoo tuko juu au siskii...

Ngosha kufikia hapo akashituka. Akasimama na kumuamuru Mdachi wa watu afute haraka sana ‘vesi’ yake yote ili aanze upya. Maana maneno (mashairi), minato na ukatili wa Ngwair kwenye kuyatafuna na kuyaumba maneno ili yatuame kwenye ‘biti’ vilimtisha Fid na kuona yeye hajafanya lolote.

Balaa la Ngwair kufunika anaposhirikiana na mtu limewatokea wengi. Ila Fid Q akawa mkweli kuwa alilazimika kurudia ‘vesi’ yake yote baada ya Ngwair kufanya matusi mazito. Kuna watu wameondoka dunia ikiwa inawahitaji zaidi kuliko bahari na milima.

Umeshausikia wimbo wake wa Mikasi, ambao ulimpa umaarufu zaidi? Biti ilianza kunyongwa kama utani na Profesa Ludigo. Baada ya kufika kwenye himaya ya ‘Mdachi’ P Funk Majani. Akadata. Sikio la tatu la usikivu wa muziki likagundua kuna kitu kinahitajika zaidi kwenye ‘biti’ ile.

Akapuliza alichovuta. Akacheua alichokunywa. Kwa akili ya sanaa na kichwa chenye nywele za ‘Kidachi’, mwili uliochorwa chorwa kama kitenge. Akajifungia kwenye studio yake pale Bamaga. Akawasha kiyoyozi na kukamata mashine. Acha kabisa.

Akainyonganyonga ‘biti’ ya Mikasi kindava. Vinanda vikaimba kuliko Ferouz. ‘Biti’ ikaunguruma kuliko sauti ya Mchizi Mox. Kikatoka kitu tofauti na Ludigo akasahaulika ghafla. Ni kama Ludigo hakugusa kitu kabla. Hili ‘gemu’ limepita kwenye mikono mingi kufikia hapa. Katika wakati wake, studio na kila kitu kilichokuwemo ndani yake kilimtii. Alipoamua kufanya kazi aliifanya. Ilikuwa rahisi kuingia Ikulu ya Mkapa, lakini si kwenye geti jeusi pale Bamaga kwa Majani. Kuingia ndani ya studio yake ilikuwa ufahari kuliko kurekodi.

Lilikuwa eneo lenye heshima tele ya Bongo Fleva wakati ule. Ni sehemu iliyomfanya Joseph Haule aitwe Profesa Jay. Juma Kassim Kiroboto aitwe Sir Nature. Ndivyo hivyo kwa wengine kama Jaymoe, kusahaulika majina ya asili waliyopewa na wazazi wao.

Ilikuwa nyumba ya ndoto kwa wanamuziki. Kwanini usiheshimu uwepo wako ndani? Baada ya vurugu za Majani kuijaza ‘biti’ uzito wa tani saba. Ngwair. Miongoni mwa viumbe ambao kama ubongo ni ugonjwa ungeomba akuambukize. Akaachiwa uwanja.

Hakufanya makosa, akatambaa nayo. Akaitendea haki akili ya ubinifu ya Ludigo na Majani. Akaongelea maisha halisi ya wanamuziki wa wakati ule. Huku akishirikiana na Ferouz, Mchizi Mox, Mkoloni, P Funk na mwanadada Raha P.

Ukisikiliza walichoimba kwenye ngoma ya Mikasi. Ndo maisha yao yalivyoendeshwa na wanamuziki wakati ule. Walikesha kama popo usiku na kuzurura kama kunguru mchana. Waliishi dunia yao. Asubuhi na mapema wengi wao akili zilivurugwa na vimiminika vinavyoongeza akili mpya.

Pale Graveyard Makumbusho, ilikuwa kama sehemu rasmi ya kukamatwa kwa wanamuziki. Hawakuwahi kuacha kwenda kwa sababu ya kukamatwa kila siku. Waliendelea kupatukuza kana kwamba wamefunga napo pingu ya maisha ya kuvutia bange.

Muda wote mtu ana mchanganyiko wa bange na pombe. Atapata wapi wazo la kuulizia kiwanja cha kununua ajenge? Bei ya mfuko wa saruji? Ili iweje? Wengi walipata umaarufu na pesa wakiwa wadogo. Akili ya kuwaza kesho yake ilikuwa kama kibaka na kituo cha polisi.

Ngwair aliimba alichokiishi yeye na wenzake wa wakati ule. Hata msanii mwenye ‘singo’ moja tu radioni. Bila video wala picha kwenye gazeti. Hakutaka kupanda usafiri wa umma kama daladala au kutembea kwa miguu. Alijiona staa anayestahili kujificha. Kulikuwa na ulimbukeni wa umaarufu. Bajaji au bodaboda hazikuwepo wakati huo. Taksi ikawa usafiri wao. Pesa ziliteketea kwenye pombe na usafiri. Kwa waliokuwa hawana usafiri binafsi wala washikaji wenye ‘ndinga’.

Hawakujali baadaye yao walichoangalia ni kinachowazunguka. Pesa zao zilitoweka kama ambavyo mvuto wao ulivyotoweka kwa mashabiki. Usisumbue kichwa kujua sababu za wasanii wa kipindi kile wengi wao kutoweka kwenye game mpaka katika maisha ya kawaida.

Nenda kasikilize ngoma ya Mikasi ya Ngwair. Ndivyo walivyoishi na ndivyo pesa zao zilivyotoweka. Ziliishia kwenye kaunta za bar maarufu mjini na kumbi za starehe. Hakuimba uongo bali ukweli juu ya maisha laghai ya uongo kwa wasanii wengi. Ambao walijikweza tofauti na kipato.Godzilla naye hatunaye. Ambaye alipita kwenye mifereji ya Ngwair kwa michano huru (freestyle). Kamfuata kaka yake. King Zilla mwambie tunammis kwenye kona ‘spidi’ ileile 120. RIP Godzilla.endo umeumaliza.



Columnist: mwananchi.co.tz