Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mzee Karume niliyemjua, nisiyemsahau

50916 Pic+karume

Mon, 8 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kila mwaka tarehe kama ya leo vyombo vya habari hutawaliwa na taarifa juu ya kuuawa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume siku ya Ijumaa, Aprili 7, 1972.

Sasa ni miaka 47 tangu Mzee Karume alipouawa kwa risasi akicheza bao nje ya jengo la Afro-Shirazi Party (ASP), sasa ofisi ya CCM iliyopo Kisiwandui, mjini Unguja.

Eneo hili zamani lilianikwa ngozi juu ya mapipa na kuitwa Mapipa ya Ngozi.

Unaposoma vitabu au magazeti au ukisikiliza simulizi juu ya kifo chake utajiuliza ukweli ni upi? Zipo simulizi nyingi za hali ilivyokuwa kabla, alipouawa na wapo waliotoa maelezo yenye ajenda iliyojificha ya kisiasa.

Siku ya Aprili 6, 1972 nilifika Zanzibar kama mwandishi wa gazeti la Standard (sasa Daily News) kuandika habari za mashindano ya timu za vijana wa nchi za Afrika Mashariki ambayo alikuwa ayafungue.

Hali ilikuwa ni ya kawaida. Wakati jua likitua Aprili 7 nilikuwa ninacheza dhumna mtaa wa Baraste Kipande, nusu kilomita kutoka Kisiwandui ambapo mzee Karume pia alikuwa akicheza mchezo huohuo.

Ghafla ilisikika milio ya risasi, ikafuatiwa na ving’ora vya polisi huku watu wakikimbilia majumbani.

Maduka yalifungwa na askari wenye silaha waliingia majumbani, walipiga watu na wengine waliwekwa mahabusu.

Wapo wana wa familia yangu waliokamatwa na shemeji yangu Abdulla Ali alikuwa miongoni mwao na akawa mshtakiwa namba moja katika kesi ya uhaini ya kumuua Karume.

Zipo habari kuwa mzee aliambiwa kuhusu tetesi za kutaka kumuua na kushauriwa abaki nyumbani, lakini aliukataa ushauri. Alikwenda kusalimia marafiki na baadaye kufika Kisiwandui alipouawa.

Ingawa Mzee Karume hakuwa na maelewano na baadhi ya wana siasa wa chama cha Umma na baadhi ya mawaziri wake walioshiriki katika mapinduzi, kuuawa kwake kuliacha maswali kibao kuhusu sababu na lengo la hatua hiyo.

Alipigwa risasi na vijana watano, wakiwamo wanajeshi na polisi walioongozwa na Luteni Humoud Mohamed ambaye alipokuwa akisoma Urusi alipata taarifa ya kuuawa baba yake mzazi na kuapa angelilipiza kisasi.

Wazee waliokuwapo kwenye tukio walisema baada ya Humoud na wenzake kuteremka kutoka katika gari ya aina ya Land Rover na bunduki mkononi alimwambia Karume alifika hapo kulipiza kisasi cha kuuawa baba yake.

Nimesoma na kuambiwa kwamba Sheikh Thabit Kombo aliyekuwa katibu mkuu wa ASP alisimama na kumwambia Humoud ‘Msalie Mtume usifanye hivyo’.

Humuod alimjibu: “Mzee ninakuheshimu, nakuomba ukae kitako”.

Baada ya hapo yeye na wenzake walifyatua risasi ambazo nyengine zilimjeruhi Mzee Thabit kiunoni na mguuni huku wengine wakitimua mbio.

Nani alipanga na kutekeleza hayo mauaji ni utata, lakini simulizi zinawalaumu watu 14 walioitwa kikundi cha mauaji, wengi walikuwa wajumbe wa Baraza la Mapinduzi.

Kifo chake kilifuatia kukamatwa zaidi ya watu 500, wakiwemo maofisa wa jeshi waliokuwepo Bara na Visiwani, wanasiasa maarufu akiwamo aliyekuwa Waziri wa nchi za nje, Abdulrahman Babu na waliowahi kuwa mawaziri.

Utawala wa Karume

Utawala wa Karume umeangaliwa kwa sura nyingi. Mambo mengine hufichwa na wapo waliomzulia mambo ambayo hakuyasema wala kuyafanya.

Wapo waliompa sifa asizostahiki na wapo waliobuni hadithi za uwongo kumpaka matope.

Ninachoweza kusema kwa kujiamini kwa kumjua tokea mdogo na kuzungumza naye tokea utotoni mwangu na alipokuwa Rais, alipomtembelea baba yangu nyumbani. Mzee huyu alikuwa mtu mzuri.

Alikuwa mtu mwenye imani na huruma, lakini alizungukwa na watu walioshauri vibaya au kufanya mambo machafu nyuma ya mgongo wake.

Baada ya mapinduzi walikuwapo viongozi waliomzungukwa waliokuwa wanamshawishi kufanya mambo ambayo waliomjua kwa undani wasingetegemea kufanywa na serikali aliyoiongoza.

Maisha yake

Simulizi za maisha yake zina utata. Kwa mfano, wapo waliosema alizaliwa Kiongoni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar na mama yake ni Bibi Amina Kadir (Kadudu) na ni mtoto wa kwanza katika familia ya watoto watano ya Bwana Amani Karume. Hapana maelezo ya kina ya wazazi wake.

Wapo waliodai alitokea Malawi na kufika Zanzibar akiwa mdogo na wengine wamedai wazazi wake walitokea ile iliokuwa ikiitwa Rwanda-Urundi (sasa ni nchi za Rwanda na Burundi).

Sijasikia au kuona maelezo yakinifu ya habari za ndugu zake, Asha, Shumbana na Othman. Nilipokuwa mdogo niliwahi kumuona Shumbana akimtembelea Karume nyumbani kwake, lakini hao wengine siwafahamu.

Mke wa mwanzo wa Mzee Karume niliyemjua kwa karibu ni Fatma Gulamhuseein (mama Fatma Karume) tokea nilipoanza kupata fahamu zangu mwanzoni mwa miaka ya 1950.

Nilimuona Mzee Karume kuwa ni rafiki wa kila mtu mtaani licha ya tofauti za kisiasa, lakini zaidi kwa watoto ambao walipenda kuazima baiskeli yake (mimi nikiwa mmoja wao).

Kila mtoto wa kiume alimwita ‘Shabbab’ na wa kike “mchumba wangu”.

Kwa bahati mbaya, licha ya kukaa naye mara nyingi na hata aliponifundisha kucheza karata na dhumna, sikuwahi kumuuliza juu ya habari za wazee na ndugu zake ijapokuwa nilipenda kupata habari na kuwa mwandishi tangu nikiwa shule ya msingi.

Mzee Karume alipendeza kukaa mtaani kwa kuwa mtu wa mikasa. Siku zote jua lilipochomoza alikuwa akipiga soga katika baraza ya kahawa mbele ya nyumba yetu.

Miongoni mwa aliokuwa anazungumza nao alikuwa baba yangu, mjomba wangu Suleiman, Shebe “Madawa”, Rashid Mbarouk, Muhsin na Aboud Maalim,

Abeid (muuza vifuu), Abaa aliyekuwa fundi wa baiskeli na mzee mmoja fundi mwashi, Mwinjuma aliyemchukua Ikulu alipokuwa Rais.

Jambo lisilokuwa na ubishi ni kuwa Mzee Karume alizaliwa 1905 na kupata elimu ya msingi kuanzia katikati ya miaka 1910.

Baada ya masomo alikuwa baharia katika meli za mizigo na kila aliporudi safari aliniletea paketi za peremende, chokoleti na biskuti.

Alijiunga na chama cha mabaharia wa Uingereza kilichokuwa na makao yake makuu Liverpool, Uingereza.

Sikushangaa kumfahamu ni mpenzi wa klabu ya Liverpool wakati wazee wengine mtaani walikuwa mashabiki wa Blackpool, Leeds, Everton, Westham na Shefield United.

Vilevile alikuwa mwanachama wa Yanga ya Dar es Salaam na kwake ukumbini zilikuwepo na picha alizopiga na wazee wa Yanga katika miaka ya 1948 na baadaye.

Alipokuwa Rais alitoa fedha kusaidia ujenzi wa klabu ya Yanga iliyopo Jangwani na mke wake (mama Fatma) mpaka leo hafichi mapenzi yake kwa klabu hii.

Siku moja tulipokuwa uwanjani kuangalia mpira nilimuona akisherehekea goli maridadi lilioizamisha timu yake ya Kisimamajongoo.

Aliipenda klabu ya Liverpool kwa sababu alipokuwa baharia meli yake ilifika sana katika bandari hiyo ambayo mji wake una historia ndefu ya Waafrika kuishi hapo zaidi ya karne nne ziliopita.

Mzee Karume aliiona Liverpool ni timu ya mabaharia wenzake

Mapenzi yake ya mchezo ndio yaliyomfanya mara baada ya mapinduzi kuipatia uwanja wa Amani uliojengwa ukiwa ndio bora zaidi Afrika Mashariki na Kati.

Alisisitiza amani katika michezo wakati wote na kusema hapana haja ya uhasama na labda ndio maana alifurahia hata timu aliyoipenda ilipofungwa bao safi.

Watu wanaomfahamu marehemu hawakushangazwa siku moja katika mwaka 1969 au 1970 alipokuwa jukwaa kuu kuangalia mchezo kati ya Mwadui na Miembeni ya Zanzibar alipoamuru uvunjwe kabla ya muda kwa vile aliona Mwadui walikuwa wanacheza rafu.

Alitoa amri kwa timu ya Mwadui kuchukuliwa uwanjani na polisi kupelekwa moja kwa moja uwanja wa ndege na kuondoka Zanzibar.

Aliipiga marufuku timu hiyo kutembelea Zanzibar na haikufika Visiwani tena wakati wa uhai wake.

Alikuwa akisema “soka ni mchezo wa waungwana na ni watwana ndio wanaocheza rafu”.

Kutokana na kutopenda watu kuumizana katika michezo alipiga marufuku ndondi Zanzibar na sheria hii haijafutwa mpaka leo na ndio maana hapana harakati za mchezo wa masumbwi Zanzibar.

Siku moja, nikiwa na mwandishi mwenzangu maarufu hapo zamani, Mohamed Karim (baba wa mtangazaji Farouk Karim wa ITV), nilimuuliza kwa nini hapendi ndondi. Jibu yake lilikuwa fupi, lakini la kukata na shoka.

“Eboo! Wee Shtobe (jina langu la utani nilipokuwa mdogo kwa vile nilipenda kupigana bila ya sababu) unapigana na mwenzako ili iwe nini. Ukitaka kupigana pigana na tumbo lako na sio na mwenzako”.

Wakati timu ya Zanzibar ilipopiga kambi kwa michuano ya mwisho ya Kombe la Gossage 1966 (sasa Chelenji) ilipofanyika Zanzibar nilimuona Mzee Karume akiitembelea timu hiyo asubuhi na jioni.

Aliangalia hali ya malazi na chakula na kutazama mazoezi na hata kutoa maelekezo kwa wachezaji.

Pia, alikuwa hodari wa kucheza dhumna, bao na karata na tulipokuwa tukirusha kishada, hakupenda kile kilichokuwa na mkia kwa vile hali hiyo ilionyesha kukosekana ustadi katika kukitengeneza.

Mara nyingi alifika kuangalia mpira bila ya taarifa mapema hata timu ndogo zilipocheza uwanja wa Mao Dzedung.

Baadhi ya wakati alikuta jukwaa kuu na kukuta wamekaa watoto. Alichofanya ni kukaa nao kuangalia mchezo kama na yeye ni mtu wa kawaida.



Columnist: mwananchi.co.tz