Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mzee Cheyo, Lipumba wanavyomsaidia refa aendelee na mechi

40527 Edo+Kumwembe Mzee Cheyo, Lipumba wanavyomsaidia refa aendelee na mechi

Thu, 7 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katika shughuli za Kitaifa macho yangu huwa yanaganda kwa wazee wangu. Mzee Professa, mwenye elimu nyingi, Ibrahim Lipumba wa CUF na Mzee wangu mapesa, John Cheyo wa UDP. Huwa wananiacha hoi. Nawakubali sana.

Kule kwenye mpira wachezaji wa timu moja wakibaki sita mwamuzi haruhusiwi kuanzisha mpira. Huku katika siasa ili itifaki itimizwe kuna wakati mtu mzito mtoa hotuba analazimika kusema ‘na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa’.

Ukisikia hii sentensi imesemwa basi kamera huwafuata Mzee Lipumba na Mzee Cheyo. Huwa nacheka sana. ni nadra sana katika shughuli ya Serikali au ile ya juzi ya mhimili mwingine ukasikia sentensi hiyo nzito halafu kamera ikamuonyesha Zitto Kabwe au John Heche. Huwa hawaendi. Sijui kwa nini.

Wazee wangu Lipumba na Cheyo hawakosi. Wanatimiza namba ili mechi iendelee. Nafurahi sana. Miaka ya karibuni huwezi kusikia eti wazee wangu hawa wanafungua matawi ya vyama vyao lakini ukweli ni kwamba vyama vyao vipo na msajili amevisajili kihalali.

Hawajawahi kupinga kuzuiwa kwa mikutano ya vyama vya siasa. Nadhani wao wanaendesha mikutano yao kisasa zaidi. Labda wanatumia ‘magroup’ ya Whatsapp kuhutubia au hutumia zaidi njia ya ‘Bluetooth’ kufikia wanachama wao. Dunia imekuwa kijiji siku hizi. Hauwezi kujua.

Hauwezi kusikia nia yao ya kwenda Ikulu kuchukua nafasi ya urais. Huwezi kusikia mipango yao ya kuongeza wabunge katika vyama vyao, lakini bado wanabakia kuwa wapinzani na msajili wa vyama vya siasa anatambua hilo. Nilisahau, kumbe Mzee Cheyo hana jimbo!

Nadhani kwa sasa mpango mkubwa zaidi kwao kwenda Ikulu ni kwa kutumia hafla zaidi na sio boksi la kura. Kumbe wakati mwingine hatupaswi kuyafanya maisha kuwa kitu kigumu sana, kumbe kuna njia nyingi za kufika Ikulu kuliko kugombea urais. Hata Mzee wangu Lyatonga aligundua hilo wakati wa utawala wa Mzee JK.

Wazee wangu kwa sasa hawataki shida. Nadhani wanaufanya upinzani katika njia za kisasa zaidi. Njia ambazo wapinzani wengine duniani wameshindwa kuzitumia. Nadhani wapo katika Serikali ya mseto ya kufikirika zaidi. Binafsi nawakubali sana wazee wangu hawa, nami nimeamua kufayanya maisha yasiwe magumu. Nadhani nimeeleweka.



Columnist: mwananchi.co.tz