Kila kilicho na mwanzo hakikosi kuwa na mwisho. Hivi ndivyo ilivyokuwa Novemba 5, 1985 wakati utawala wa miaka 24 wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere uligota na kuanza enzi mpya ya Ali Hassan Mwinyi.
Lilikua ni tukio lililovuta hisia za wengi waliofika Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru) jijini Dar es Salaam kushuhudia Rais wa tatu barani Afrika kwa wakati huo akiachia madaraka kwa njia ya amani na kwa kufuata mchakato wa kikatiba.
Haikuwa jambo la kawaida kumuona mtu aliyekuwa Ikulu kwa zaidi ya miaka 24, akiondoka Uwanja wa Taifa bila ya ulinzi mkubwa na akiwa na magari machache tofauti na hali ilivyokuwa kipindi kirefu kila alipojitokeza hadharani.
Msafara alioingia nao wa walinzi na magari ya kusindikiza, ulihamia mara moja kwa Ali Hassan Mwinyi baada ya kuapishwa tu. Mwinyi ndiye alikuwa mtu wa kwanza kuondoka uwanjani hapo akiwa na ulinzi mkubwa kabla ya Nyerere kufuatia kuondoka eneo hilo lililotumika kukabidhi uhuru wa Tanganyika mwaka 1961.
Kabla ya Nyerere kukabidhi nchi, viongozi wengine wa Afrika walioweza kuachia madaraka kwa amani ni Leopold Senghor wa Senegal na Ahmadou Ahidjoo wa Cameroon, wengine walikuwa wakiondolewa madarakani kwa mapinduzi.
Siku hiyo, watu mbalimbali wa ndani na nje ya nchi walihudhuria sherehe hizo kushuhudia Mwalimu Nyerere akitimiza nia yake aliyoidokeza mwaka 1975 alipopitishwa kugombea urais na Tanu.
Habari zinazohusiana na hii
Baadhi ya waliohudhuria ni rais wa Zanzibar, Idris Abdul Wakil na katibu mkuu wa CCM, Rashidi Kawawa ambao sasa wote wameshafariki.Wengine ni waziri mkuu wa zamani, Dk Salim Ahmed Salim; Seif Sharif Hamad, Maria Nyerere na mke wa Rais wa Pili, Mama Mwinyi. Walikuwa ni sehemu ya watu zaidi ya 40,000 waliohudhuria sherehe hizo za kuapishwa zilizoanza saa 3:00 asubuhi. Hafla hiyo ilitangazwa moja kwa moja na Radio Tanzania.
“Kama kawaida ya sherehe, kulikuwa na shamrashamra kutoka kwa watu waliofika uwanjani kushuhudia,” alisema mwanasiasa mkongwe nchini, Arcado Ntagazwa.
“Watu wanakwenda uwanjani kuangalia Rais akiapishwa na baada ya hapo tukarudi nyumbani kusubiri shughuli nyingine ziendelee, likiwamo la uteuzi wa baraza la mawaziri.
“Mimi sikuwa na wasiwasi kama nitateuliwa au la kwani nilikuwa nimemaliza nikiwa waziri wa fedha. Sasa kama nateuliwa au vinginevyo nilikuwa sijui.”
Ntagazwa alikuwepo katika baraza la kwanza la Mwinyi.
Wakati Mwinyi akila kiapo, viongozi na wananchi wakiongozwa na Mwalimu Nyerere walisimama kimya na kwa utulivu wakati bendera ya Rais ikiteremshwa taratibu ikiwa ni ishara ya Mwalimu Nyerere kuacha madaraka hayo.
Shughuli za kuapishwa ziliendeshwa na Jaji Mkuu Francis Nyalali ambaye sasa ni marehemu, pamoja na Katibu Mkuu wa Rais, Timothy Apiyo. Mara baada ya kula kiapo huku akiwa ameshikilia kitabu cha Quran, Mwinyi alikabidhiwa na Mwalimu Nyerere Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikiwa na marekebisho ya mwaka 1984 na ilani ya Uchaguzi Mkuu wa 1985.
Muda mfupi baadaye alipigiwa wimbo wa Taifa na mizinga 21 na wakati huohuo bendera ya Rais ikapandishwa ikiwa ni ishara ya kukabidhiwa madaraka kikamilifu ya uongozi wa Taifa la Tanzania na hiyo ilikuwa ndiyo ishara kuwa Mwalimu Nyerere alistaafu rasmi.
Baada ya kuwasili Ikulu, Mwinyi alimteua Joseph Warioba kuwa Mbunge, Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Baadaye aliapishwa na Mwinyi kushika nyadhifa hizo.
Mwinyi pia alimwapisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Idris Abdul Wakil, kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Uteuzi wa Warioba ulitangazwa muda mfupi baada ya Rais Mwinyi kuapishwa kuwa Rais kwa muhula wa miaka mitano.
Awali, Warioba alikuwa Waziri wa Sheria na Mwanasheria Mkuu wa Serikali tangu Machi 1983. Aliingia katika utumishi wa Serikali mwaka 1966 akiwa Mwanasheria wa Serikali, katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na mwaka 1968 hadi 1970 alikuwa Mwanasheria wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na mwaka 1971 hadi 1975 alikuwa Mkurugenzi wa Sheria na Mashirika ya Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje. Mwaka 1975 alirudi tena Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na kuwa Msaidizi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali hadi mwaka 1976 alipoteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu.
Mwaka 1983 aliteuliwa kuwa Waziri wa Sheria na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Aunda baraza la mawaziri
Novemba 7, 1985 Mwinyi alitangaza Baraza la Mawaziri. Manaibu waziri waliteuliwa na watatu miongoni mwao walikuwa wapya. Naibu waziri mmoja wa zamani aliachwa. Walioingia katika baraza jipya ni Kawawa, aliyekuwa waziri asiye na wizara maalumu, Dk Salim Ahmed Salim (Waziri wa Ulinzi), na Cleopa Msuya (Fedha na Mipango).
Wengine ni Benjamin Mkapa (Mambo ya Nje), Paul Bomani (Kilimo na Maendeleo ya Mifugo), Kingunge Ngombare Mwiru (Serikali za Mitaa na Ushirika), Mustapha Nyang’anyi (Mawasiliano na Ujenzi), Daudi Mwakawago (Kazi na Maendeleo ya Utumishi), na Muhidin Kimario (Mambo ya Ndani).
Wengine ni Jackson Makweta (Elimu), Al Noor Kassam (Maji na Nishati), Getrude Mongella (Maliasili na Utalii), Basil Mramba (Viwanda na Biashara), Dk Aaron Chiduo (Afya na Ustawi wa Jamii), Damian Lubuva (Sheria na Mwanasheria Mkuu wa Serikali), Dk Pius Ng’wandu (Ardhi, Maji, Nyumba na Maendeleo Mijini), na Fatma Saidi Ali (Maendeleo ya Jamii, Utamaduni, Vijana na Michezo).
Lubuva, ambaye baadaye alifikia wadhifa wa jaji wa Mahakama ya Rufani, anasema nafasi hiyo haikuwa ngeni kwa kuwa alishafanya kazi kama hiyo Zanzibar na alishakuwa naibu mwanasheria mkuu chini ya Jaji Warioba.
“Sikuwa nimewahi kuwa mbunge na nilipofika bungeni nilijifunza kidogokidogo kutoka kwa wabunge na mawaziri mwisho nikazoea,” alisema.
“Lakini upande wa mwanasheria mkuu sikuwa na kazi kubwa kwa kuwa wengi nilikuwa nimefanya nao kazi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu,” anasema Jaji Lubuva aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Katika baraza hilo kulikuwa na mawaziri wengine sita wa nchi na manaibu kumi.
Hao ni Luteni Kanali Abdulrahman Kinana, ambaye aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Amina Salum Ali (Fedha, Uchumi na Mipango), Nicas Guido Mahinda (Viwanda na Biashara). Naibu waziri aliyeachwa alikuwa Eslie Mwakyambiki (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa).
Jina la Mwakyambiki halikupitishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa alipotaka kugombea tena ubunge wa Kyela.
Pia, katika uteuzi wa Novemba 7, manaibu waziri wawili waliendelea kutumikia wizara zao za awali na watatu walibadilishwa. Arcado Ntagazwa aliyekuwa naibu waziri wa fedha, akapelekwa mawasiliano na ujenzi, na Evarist Mwanansao aliyekuwa Wizara ya Viwanda na Biashara, akapelekwa Ardhi, Maji, Nyumba na Maendeleo Mijini, huku Steven Kibona aliyekuwa Wizara ya Fedha, akapelekwa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Naibu Mawaziri walioendelea katika wizara walizokuwamo ni Hamad Rashid Mohammed aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani na Nalaila Kiula ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Elimu.
Kesho tutasoma jinsi wabunge 15 wa kwanza wa viti maalumu walivyopatikana tangu kuanzishwa kwa Bunge la Tanzania na wabunge wa Jumuiya za Wananchi.