Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mwenyekiti UVCCM amepotoka, akemewe

9515 PIC+UVCCM TanzaniaWeb

Thu, 2 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nimemsikiliza mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Kheri James akitaka wananchi waliochagua upinzani wasipelekewe maendeleo nikashangaa na kujiuliza maswali mengi.

Pia, nimemsikiliza akiomba radhi kuhusu kauli zake hizo.

Huyu ndio kiongozi wa jumuiya muhimu na yenye nguvu ndani ya CCM ambaye hajui kuwa maendeleo hayana chama na Katiba ya mwaka 1977 imekataza kabisa ubaguzi wa aina hii, au anajua baadaye baada ya kushutumiwa na watu wengi.

Bahati mbaya sana, hata viongozi wa CCM hawajamchukulia hatua hadi sasa licha ya kauli yake kupingana na ya mwenyekiti wake, Rais John Magufuli anayeimba kila mara kuwa maendeleo hayana chama.

Akiwa huko mkoani Manyara katika moja ya mikutano ya kampeni za uchaguzi mdogo, kiongozi huyo wa vijana alitoa matamshi hayo ambayo bila kukanushwa, yataendelea kubaki kuwa msimamo wa CCM.

Nikimnukuu alisema “Mbowe (Freeman) na wachekeshaji wenzie wanajua. Nchi hii hakuna maendeleo bila CCM kuamua. Sisi tukiamua yanakuja na tukiamua hayaji na cha kutufanya hakuna.”

“Kwani wewe diwani (aliyehama Chadema na kuingia CCM) ulivyokuwa Chadema tulileta kitu hapa. Waambie tulileta? Hatuwezi kuleta. Tunaletaje? Yaani tukuletee tu kienyeji enyeji? Hatuleti”

“Sisi tuliahidi shule, ukakataa shule; tuliahidi zahanati, ukakataa sasa tunaleta za nini. Kitendo cha kumchagua diwani wa Chadema maana yake umekataa mipango ya CCM.”.

Ibara ya 3(1) ya katiba ya nchi na marekebisho yake, inasema wazi Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Asichokijua James ni kuwa katiba ambayo ndio sheria mama, imekataza kabisa matendo ya ubaguzi hasa katika nchi kama Tanzania ambayo mfumo wa vyama vingi vya siasa ni wa kisheria.

Ibara ya 12 inasema lengo la katiba ni kuhakikisha inazuia na kuondoa dhuluma, vitisho, ubaguzi, unyanyasaji, rushwa, uonevu na upendeleo miongoni mwa wananchi kwa misingi ya itikadi.

Lakini ibara ya 34 (5) ya Katiba hiyo imetafsiri neno “kubagua” kuwa ni kutimiza utashi, haki au mahitaji mengineyo kwa watu mbalimbali kwa kuzingatia utaifa wao, kabila au maoni yao ya kisiasa.

Sasa kama Katiba ambayo ndio sheria mama inakataza ubaguzi wa aina yoyote na Rais Magufuli amelisisitiza hili katika hotuba zake nyingi tu, Kheri James anapata wapi ujasiri wa kubagua watu?.

Leo Kheri James anataka kutuambia na kuwaaminisha Watanzania kuwa Serikali ya CCM inaadhibu wana CCM na wasio wana CCM kwa sababu tu eneo fulani wananchi wamechagua upinzani?

Mathalani, katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, jimbo la Siha mkoani Kilimanjaro, Rais John Magufuli alipata kura 18,252 na Edward Lowassa 22,572 basi Serikali isipeleke maendeleo Siha?

Hivi Kheri James hajui kuwa vyama vya siasa ni daraja tu la kupata uongozi wa kisiasa na baada ya uchaguzi, anayekuwa amechaguliwa ni kiongozi wa wote, waliomchagua na wasiomchagua?

Sisi kama Watanzania tunapaswa kukemea kwa nguvu zetu zote pepo hili la ubaguzi ambalo limeanza kulinyemelea taifa letu na njia pekee ya kufanya hivi ni kusimama katika utawala wa sheria.

Sote tunafahamu vyombo vinavyohusika katika kupanga na kuidhinisha bajeti ya maendeleo kwa wananchi ni Bunge na mabaraza ya madiwani na sio kwa utashi wa chama kilichopo madarakani.

Maendeleo yanafanywa kutokana na kodi za Watanzania, ambao ni wana CCM na wasio wana CCM na katika kodi hizo zikiwekwa kwenye kapu huwezi kujua ipi ni ya mwana CCM na ipi sio.

Vivyo hivyo katika upigaji kura, huwezi kujua ipi ni kura uliyopigiwa na mwanachama wa chama chako na ipi umepigiwa na mfuasi wa chama cha upinzani au Mtanzania asiye na chama.

Natamani mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli na vyombo vyake vya maamuzi ndani ya chama, pamoja na kuomba radhi, vimuite na kumuonya ili asirudie kauli kama hizo.

Columnist: mwananchi.co.tz