Fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea kule Russia zimeshuhudia matumizi ya mfumo kisaidizi kwa mwamuzi, VAR katika kuamua masuala mbalimbali yanayokaribia au kufanana na utata.
Kwa mara ya kwanza Fifa wametumia mfumo huo kwa ajili ya kutenda haki na uhalali japokuwa kuna karaha zake katika matumizi.
Waamuzi kadhaa katika fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea kule Russia, wametoa uamuzi wa kila aina kwa kukubali kutengua uamuzi wa awali, lakini pia wapo waliosimamia msimamo wao wa awali baada ya kujiridhishwa kwa kila kitu.
Mwamuzi mkongwe wa EPL, Mark Halsey alipongeza hatua ya Fifa kuanzisha matumizi hayo.
Tayari Fifa imeelezea kuridhishwa na matumizi ya VAR katika fainali zake ambayo ilianza kuonwa mechi ya Kundi C kati ya Australia na Ufaransa na mwamuzi aliipa Ufaransa penalti iliyowafanya waibuke na ushindi wa mabao 2-1.
Rais wa Fifa Gianni Infantino alisema wameridhishwa na VAR na kwamba imeonyesha mafanikio makubwa na hata jamii ya soka.
“Ukweli, ni sawa baadhi ya uamuzi unasababisha maswali mengi. Ni matumaini ya Fifa kwamba kila kinachoamuliwa, Fifa haiwezi kuwa juu yake, ni uamuzi wa mwamuzi kwa muono wake,” ilisema taarifa ya Fifa.
Mapema kabla ya fainali za mwaka huu kuanza, Gianni Infantino alisema kuwa kuanzishwa kwa mfumo wa VAR kutasaidia mwamuzi kuamua kwa haki, japokuwa haitakiwi mwamuzi kuitegemea sana VAR, na asimame kwenye uamuzi wake.
Hayo ya upande huo uko, sasa turudi huku kwetu kwa mfano. Ninajiuliza, hivi waamuzi wetu wakipewa hizi VAR itakuwaje? VAR inatakiwa nidhamu ya hali ya juu.
VAR inatakiwa mwamuzi mwenye weledi hasa kwa kuwa ubabaishaji hautakiwi kwenye hii.
Ukiangalia mazingira ya Tanzania kwa mfano, huwezi kuzitumia kwenye viwanja visivyokuwa na sifa kutokana na teknolojia yenyewe.
Angalia kwa mfano, Uwanja wa Jamhuri Morogoro, Namfua, Singida au Nangwanda Sijaona. Ukweli matumizi yake yatakuwa na changamoto sana.
Ukiachana na hayo, ukija kwa mwamuzi mwenyewe, kwa asiye na weledi, anaweza kuitumia VAR kama bakora kuangamiza timu nyingine.
Kwa maana ipi, kwa kuwa kuna kipengele kinampa nafasi mwamuzi kuamua bila kujali kama kuna VAR na wakati mwingine yeye mwenyewe kuhitaji VAR.
Inaweza kutokea utata kwamba tukio limetokea, lakini mwamuzi akawa ama anataka usaidizi wa mashine au hataki, lakini hata akiona anaweza kuamua vinginevyo kuwa si penalti. Hapa ndipo weledi ule ninaosema unahitajika.
Waamuzi wasio na weledi wanaweza kutumia nafasi hiyo kukandamiza wengine, kuwachapa fimbo badala ya kutumia kama chombo cha kuwasaidia wengine.
Mwamuzi asiye na weledi anaweza kukubali bao ambalo kuthibitisha kuwa anaweza kulikataa kwa kutumia VAR, anaamua kukausha.
Mfano mzuri ni mechi ya Brazil na Uswisi, mwamuzi aliichunia VAR na kulikubali bao la Uswisi ambalo mfungaji alimsukuma beki wa Brazil kabla ya kufunga. Hapa ninachokiona, waamuzi bado hawana elimu juu ya matumizi ya VAR hivyo kuna kila sababu ya Fifa, CAF, hata TFF yetu kama ikianzisha, kuwapa somo kwelikweli waamuzi, kwa kuwa hata hao walioko Russia wakati mwingine wanashindwa kufanya uamuzi sahihi licha ya kujiridhisha na VAR. Kuna kazi kubwa ya utambulisho wa hii VAR.