Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mwalimu hapaswi kuachana na teknolojia

29130 Mwalimu+pic TanzaniaWeb

Wed, 28 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Maendeleo ya teknolojia yanafanya sekta zote zisonge mbele kwa kasi kubwa. Tunaona teknolojia mpya zinaibuliwa kwenye kilimo, viwanda, biashara, uhandisi, ujenzi na fani nyingi hali inayowafanya wahusika wa fani hizo kila kukicha kujifunza vitu vipya.

Hilo pia linapaswa kuwa kwenye elimu hususani kwa walimu. Kasi hii ya ukuaji wa teknolojia inashuka hadi kwa wanafunzi hivyo ni muhimu kwa mwalimu wa kisasa kuzingatia yafuatayo ili kwenda na kasi hiyo.

Jichanganye na walimu wengine

Ni muhimu kwa mwalimu kujitathmini uwezo wake na kujifunza kutoka kwa wengine. Hili litawezekana endapo mwalimu atakuwa anapata wasaa wa kukutana na walimu na wadau wengine katika masomo aliyojikita ili kupeana uzoefu.

Inashauriwa kuhudhuria mikutano, semina, warsha na makongamano ya kitaaluma. Kukutana na walimu wengine ni njia mojawapo ya kubadilishana mawazo na kupeana njia tofauti za kufundisha kwa ufanisi ili kuwa na darasa bora.

Kujifunza hakuna mwisho

Ukiwa mwalimu haina maana ndiyo umemaliza kusoma, kama ilivyo kwenye fani nyingine kuna mambo mengi ya kujifunza. Usijibane wala kujizuia kujifunza vitu vipya na ukipata nafasi ya kuongeza ujuzi usisite kufanya hivyo.

Jiwekee utaratibu wa kusoma vitabu, majarida na ikiwezekana peruzi mitandaoni kujifunza vitu mbalimbali. Unaweza pia kujiunga na kozi zinazotolewa mitandaoni ili kukuongezea stadi kwenye fani yako ambayo ndio msingi wa maisha ya wengi.

Fahamu teknolojia

Walimu wa kisasa wanatakiwa kufahamu kuhusu teknolojia na kuwa tayari kuvumbua teknolojia mpya ambazo zitaleta maboresho kwenye ufundishaji wao.

Kama inavyofahamika kuwa teknolojia inakuja na kubadilika hivyo walimu muda wote wanatakiwa kuwa tayari kwenda sawa na mabadiliko ya teknolojia yanayotokea.

Hii itasaidia kwenda sambamba na mabadiliko hayo na kuyatumia kwenye suala zima la utaoji elimu. Mwalimu akiwa mtundu kwenye masuala ya teknolojia hata darasa lake wanafunzi watakuwa wadadisi na watashirikiana katika kujifunza.

Shiriki kwenye mitandao ya kijamii

Kuwa mwalimu haina maana umejitenga na dunia. Kwa teknolojia iliyopo sasa hakuna sababu ya kupenda kuhadithiwa vitu ni muhimu kujionea na njia rahisi ya kuona mengi ni mitandao ya kijamii.

Mwalimu anayetumia mitandao ya kijamii anaweza kujifunza vitu vingi ikiwemo kulifanya darasa lake liwe la mjadala.

Pia mwalimu anaweza kukutana na walimu wengine na wakaweza kutengeneza mtandao wa kubadilishana uzoefu katika masomo wanayofundisha.

Pata muda wa mapumziko

Hii ni muhimu zaidi kwa mwalimu ili awe na uwezo mzuri wa kufikiria na kufundisha ni lazima apate muda wa kutosha wa kupumzika na kujiweka kando na msongo wa mawazo unaotokana na kazi.

Mwalimu wa kisasa anajua ni wakati gani apumzike yeye hata wanafunzi wake. Mtu akiwa amechoka hawezi kufundisha wala kujifunza kwa ufanisi.



Columnist: mwananchi.co.tz