Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mwalimu anavyoweza kujijengea heshima kwa wanafunzi

10661 Cristian+Bwaya TanzaniaWeb

Tue, 7 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Shauku ya walimu wengi, kama sio wote, ni kuheshimiwa na wanafunzi. Heshima ya mwalimu ni sauti inayosikika kwa mwanafunzi wake. Hiyo ina maana kuwa mwalimu anahitaji uwezo wa kumwelekeza mwanafunzi jambo na akaelekea. Katika mambo yanayoweza kumnyima amani mwalimu, ni kujikuta kwenye mazingira ambayo kile anachotaka kifanywe na mwanafunzi wake hakifanyiki.

Hali inapoota mizizi hufika mahali mwalimu akaamua kumchukulia mwanafunzi hatua za kinidhamu. Pamoja na hayo nafahamu hakuna mwalimu anayefurahia kutumia mabavu kama namna ya kumrekebisha mwanafunzi wake.

Makala yaliyopita yaligusia mazingira yanayoweza kuwafanya wanafunzi wakakosa nidhamu. Moja wapo ya sababu hizo ni mazingira mabovu ya shule, nyumbani pamoja na tabia za mwalimu mwenyewe.

Katika makala haya tunaangazia maswali matano muhimu unayohitaji kuyajibu, ikiwa unataka kuheshimiwa na wanafunzi bila kutumia nguvu kubwa.

Unawaheshimu wanafunzi wako?

Mwanafunzi ni binadamu anayehitaji heshima kama wewe. Ingawa kweli anaweza kuwa mdogo kiumri, hana elimu kama uliyonayo, lakini bado anastahili heshima.

Heshima ni kuzungumza naye kama unavyozungumza na mtu mwingine unayemheshimu. Sina maana ya kuwaogopa wanafunzi wako bali kuwatendea kama vile ungependa kutendewa wewe mwenyewe. Neno linalobeba uzito wa hiki ninachokisema ni unyenyekevu.

Mtu mnyenyekevu hana sababu ya kuwaonyesha watu kuwa amewazidi. Mtu mnyenyekevu hawatambii watu hata kama anajua fika kuwa anawazidi.

Ukiwa mnyenyekevu unawavutia watu kukuheshimu. Heshimu wanafunzi wako watakupa heshima.

Heshima si zawadi ya mwanafunzi mwenye nidhamu bali tabia ya mtu mstaarabu kwa yeyote bila kujali tabia yake.

Naelewa wapo wanafunzi wakorofi. Hawa ni wanafunzi wanaoweza kukufanya ukapandwa na jazba, ukataka kupambana nao, kuwadhalilisha, kuwatukana kwa sababu ni kweli wamekuudhi.

Lakini nikukumbushe kuwa mwisho wa haya yote, mara nyingi, ni wewe mwenyewe mwalimu kufedheheka.

Ukitaka kupata ushirikiano na wanafunzi hata wale ‘walioshindikana’ anza kwa kuwatendea kwa heshima. Unaposhughulika nao huna haja ya kuwadharau na kuwaonyesha kuwa hawana maana yoyote. Waheshimu hata kama kweli hawastahili heshima. Ukimheshimu binadamu atakulipa heshima kwa wakati wake.

Unafundisha kwa kujituma?

Wanafunzi wanaweza kuonekana hawapendi shule, lakini wana ndoto fulani katika maisha. Hata kama unaona hawaelewi na hawajali kilichowaleta shule, usisahau kuwa ndani yao kuna ndoto fulani.

Heshima yako, pamoja na mambo mengine, inategemea vile unavyowafanya waamini unafanya kila linalowezekana kuwasaidia kufikia ndoto zao.

Jiulize: Je, unajituma kuwasaidia wanafunzi wako kutambua na kufikia malengo yao? Je, unafanya kazi zako kwa weledi? Je, unaingia darasani kwa wakati?

Huwezi kuwa mwalimu anayetegea vipindi, mwalimu usiyejali kazi yako, ukategemea wanafunzi wakuheshimu. Uvivu utakufanya udharaulike.

Pia, epuka kuwafanya wanafunzi wawe na wasiwasi na uwezo wako darasani. Mfanye mwanafunzi aamini wewe ni mtu wa kutegemewa na akiomba msaada ataupata kwa sababu huna ubabaishaji. Ukweli ni kwamba mwalimu mzuri ana nafasi kubwa ya kuheshimiwa kuliko mwalimu mzembe asiyejali kazi yake.

Kwa nini wanakukosea adabu?

Kuna simulizi ya mwalimu mmoja aliyekuwa akimwadhibu mwanafunzi mmoja kwa uchelewaji. Kila siku mwanafunzi yule alikuja baada ya saa nne shuleni.

Ingawa mwanafunzi yule alijitetea kuwa ana matatizo ya kifamilia yanayosababisha achelewe, bado mwalimu hakuelewa na hakumpa nafasi ya kujitetea.

Baada ya miezi kadhaa ya kuchelewa na bakora za kila siku, Joshua hakuonekana kwa siku kadhaa kisha alipokuja alikuwa wa kwanza kushika namba. Kwa kuamini mwanafunzi amebadilika, mwalimu aliwataka wenzake wampongeze: “Darasa tumpongeze leo Joshua amewahi!”

Huku akitiririkwa na machozi Joshua aligugumia: “Mama niliyekuwa ninamhudumia kila siku asubuhi kabla ya kuja shule amefariki dunia wiki iliyopita.”

Kuna vitu mwanafunzi anaweza kuvifanya si kwa sababu anapenda. Mwalimu unayejitambua hupaswi kuwa na haraka ya kuadhibu. Jipe muda wa kufuatilia sababu zilizojificha nyuma ya utovu wa nidhamu unaouona kwa mwanafunzi.

Wakati mwingine anachokifanya huakisi makosa yako mwenyewe. Juzi ulimdhalilisha na kama binadamu mwingine akajawa na kisasi. Kwa nini leo unapomwita hakuitikii unashangaa?

Lakini pia inawezekana na wewe mwalimu hujulikani unataka nini. Mwanafunzi anashindwa kujua afanye nini kukuridhisha kwa sababu unabadilika badilika. Jana ulisema wanafunzi wasikae nje wakati wa masomo na uliwaadhibu.

Leo umewakuta nje wakati wa masomo na hujasema kitu. Kesho ukiwaambia wakaendelea kukutazama utashangaa? Muhimu kusimamia kile unachokisema.

Unawakosoa kupita kiasi?

Moja wapo ya sababu inayoweza kukufanya ukakosa ushawishi kwa wanafunzi wako ni kuwakatia tamaa. Pamoja na kwamba wanafunzi wana upungufu mwingi, huna sababu ya ‘kuwaimbia’ upungufu huo kila siku.

Unapomkatia tamaa mwanafunzi unamfanya awe na ujasiri wa kufanya lolote kwa sababu anakuwa hana cha kupoteza. Kama umemfanya ajione hana thamani, huoni chochote chema kwake, afanye nini kingine zaidi ya kukuthibitishia kuwa kweli hana thamani?

Ukitaka wanafunzi wakuheshimu, wakati mwingine ‘potezea’ matatizo yao. Wanaweza kuwa wavivu kweli, hawana nidhamu kweli, lakini onyesha kuwa kuna kitu chema unakiona ndani yao.

Unaweza kuzungumza na mwanafunzi mvivu kama vile unaongea na mtu mwenye bidii. Najua si jambo jepesi. Mwanzoni mwanafunzi huyu anaweza kudhani unamdhihaki lakini ukisimamia kumwambia unaamini yeye ni mtu mwenye bidii, unaweza kushangaa mwanafunzi akahamasika kukuthibitishia kuwa hujakosea.

Ukiwa mwalimu, jifunze kuona thamani iliyo kwa wanafunzi wako. Watie moyo na waonyeshe kuwa wanaweza. Sema maneno yanayowahamasisha. Waonyeshe thamani iliyo ndani yao, utashangaa namna watakavyokuheshimu kwa sababu umewafanya wajione ni watu wa thamani.

Unashirikiana na walimu na wazazi?

Huwezi kufanya kila kitu mwenyewe. Unahitaji ushirikiano na walimu wengine. Hapa ndipo panapohitajika mkakati na sauti ya pamoja.

Lakini pia kuna wazazi. Mwanafunzi anatoka kwenye mazingira ambayo wakati mwingine ndiyo yamemjenga kuwa hivyo alivyo. Unahitaji kufanya kazi kwa karibu sana na wazazi.

Itaendelea

Blogu: http://sw.globalvoices.org Twitter: @bwaya

Columnist: mwananchi.co.tz