Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mwalimu Nyerere aliwatoa Watanzania, Mkapa na Kikwete wamewarudisha

84604 Pic+mkappa Mwalimu Nyerere aliwatoa Watanzania, Mkapa na Kikwete wamewarudisha

Mon, 18 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Septemba 20, 2018, katika Chuo Kikuu cha New York (Africa House) New York nchini Marekani, yalifanyika mapitio ya kitabu cha “The Journey of My Life: From A Barefoot Schoolboy to President”.

Tafsiri yangu ni “Safari ya maisha yangu: Kutoka mwanafunzi peku mpaka rais”. Ni kitabu cha Rais wa nne wa Tanzania, Jakaya Kikwete.

Jumanne iliyopita katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, ulifanyika uzinduzi wa kitabu kingine kinachoitwa “My Life, My Purpose (Maisha Yangu, Kusudi Langu)”.

Kitabu kinahusu mapito ya kimaisha ya Rais wa Serikali ya awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.

Wakati wa kongamano la mapitio ya kitabu cha Kikwete huko New York, mjumbe wa bodi ya ushauri ya Chuo Kikuu cha New York (Africa House), Edward Bergman alimshauri Kikwete kukitafsiri kitabu chake kwa Kiswahili.

Bergman alimweleza Kikwete kuwa amepata kutembelea Tanzania na kushuhudia namna Watanzania wanavyompenda hasa kutokana na hulka yake ya kujishusha na unyenyekevu, akamtaka akiweke kitabu hicho kwa Kiswahili kwa ajili ya Watanzania.

Wakati wa kuzindua kitabu cha Mkapa, swali kuhusu toleo la Kiswahili likarejewa tena, hivyo wachapishaji, Mkuki na Nyota wakafafanua kuwa mchakato wa kukitafsiri unaendelea.

Kuhusu ushauri wa Bergman, Kikwete alisema kitabu kimeanza na Kiingereza kwa sababu msukumo mkubwa wa kuandika aliupata kutoka kwa Profesa Yaw Nyarko, mkurugenzi wa chuo Kikuu cha New York (Africa House).

Na kutokana na msukumo huo, ndiyo maana alikaa chuoni New York (Africa House) takriban miezi mitatu, akiandika kitabu kwa msaada au mwongozo wa wanazuoni wa chuo hicho, chini ya usimamizi wa Profesa Nyarko.

Ahadi ya Kikwete mbele ya hadhira iliyokuwapo kwenye kongamano la mapitio ya kitabu chake ni kuwa wakati wa uzinduzi, toleo la Kiswahili pia lingekuwa tayari.

Aliahidi kuwa kitabu kingekuwa tayari Januari mwaka huu, bahati mbaya sasa ni Novemba, kazi hiyo bado. Uzuri ni kuwa wakati wa mapitio, alieleza kuhusu changamoto ya kifedha ya kufanikisha uchapaji. Pengine hicho ndicho kimechelewesha.

Swali ni kuhusu Kiswahili

Kwa nini suala la Kiswahili limeibuka kwenye vitabu vya Mkapa na Kikwete? Jawabu linatolewa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Desemba 9, 1962, Tanganyika ikiwa Jamhuri, vilevile ilikuwa ikiadhimisha mwaka mmoja wa uhuru. Siku hiyo, Mwalimu Nyerere alifanya jambo ambalo alilitangaza kuwa ni zawadi yake kwa Watanganyika.

Alikuwa amekitafsiri kitabu cha “Julius Caesar”, kilichoandikwa na mwandishi mahiri kuwahi kutokea nyakati zake, raia wa Uingereza, William Shakespeare.

Mwalimu alipokitafsiri kitabu hicho, alikipa jina “Julius Kaisari”. Kilihusu simulizi ya mtawala wa zamani wa Roma, Julius Kaisari – mapambano yake, njama za kumpindua na kumuua, ushindi wa mapigano ya Philippi na mengineyo. Shakespeare alikiandika mwishoni kabisa mwa karne ya 16.

Mwalimu Nyerere pamoja na majukumu mengi aliyokuwa nayo, kama kiongozi wa Serikali, alitenga muda kutafsiri kitabu na kutangaza ni zawadi yake kwa Watanganyika. Ni kwa sababu alifahamu Kiswahili ndiyo lugha yao.

Mwalimu hakuishia hapo, nyakati za mapambano ya kujenga Taifa la kijamaa na kuupiga vita ubepari, alitafsiri kitabu kingine cha “The Merchant of Venice”, nacho kiliandikwa na Shakespeare mwishoni mwa karne ya 16 na kutoka mwanzoni mwa karne ya 17.

Mwalimu alipokitafsiri, alikiita “Mabepari wa Venisi”. Alitaka Watanzania wasome na waelewe mkasa wa madhara ya mikopo yenye riba na mikataba ya kipuuzi kati ya mabepari Antonio na Shylock.

Kutoka Julius Caesar mpaka Julius Kaisari, vilevile The Merchant of Venice hadi Mabepari wa Venisi, jawabu ni moja kuwa Nyerere alitambua Kiingereza ni lugha ya mbali kwa Watanzania walio wengi na kuwa iliyo karibu kwao ni Kiswahili.

Kwa kuufahamu umbali huo, ndiyo sababu aliamua kutafsiri kazi za Shakespeare na kuziweka kwa Kiswahili ili ujumbe alioulenga uwe jirani na Watanzania.

Kutoka miaka ya sitini, Mwalimu Nyerere alipotafsiri kazi za Shakespeare, mpaka sasa nchi haijabadilika sana. Kiswahili kimeendelea kuwa karibu na Watanzania na Kiingereza kimebaki lugha ya kufundishia.

Hakuna wakati wowote katika historia ya nchi, Rais amewahi kuhutubia Taifa kwa Kiingereza. Kufanya hivyo kungekuwa kuwaweka mbali Watanzania na hotuba ya kiongozi wao.

Miaka yote, Mkapa na Kikwete walipokuwa kwenye majukwaa ya kisiasa kuomba kura au kuhustubia, hawakuwahi kutumia Kiingereza. Ni kwa sababu wanafahamu ulimi na sikio la Mtanzania ni Kiswahili.

Ni kwa sababu hiyo, baada ya kuandika vitabu vya Kiingereza, swali la haraka limeulizwa kuhusu toleo la Kiswahili. Mpaka Bergman asiyejua Kiswahili, aliulizia. Si kwa matumizi yake, bali ni haki ya Watanzania.

Hakuna zawadi kubwa ambayo binadamu anaweza kupewa na nchi yake kama kuaminiwa na kuchaguliwa kuwa Rais – mkuu wa nchi, amiri jeshi mkuu na mkuu wa Serikali. Zawadi hiyo Mkapa na Kikwete wamepewa.

Pia hakuna malipo ambayo mtu aliyepewa zawadi hiyo anaweza kulipa zaidi ya kuitumikia nafasi hiyo kwa uadilifu na upendo mkubwa. Baada ya kuondoka madarakani, ni jambo jema kuendelea kulinda uhusiano na kudumisha ushirikiano na mawasiliano. Kiswahili ndiyo lugha ya mawasiliano ya Watanzania.

Na kwa muktadha huo, Kiswahili kikiwa lugha rahisi zaidi ya kuwaweka Watanzania karibu, ni nyenzo ya kujenga uhusiano na kudumisha ushirikiano. Hata kwa wenye kukifahamu Kiingereza, hiyo ni lugha ya tatu kwa walio wengi.

Kwa sehemu kubwa ya Watanzania, kutumia Kiingereza ni kujitenga nao. Si kwa sababu hawaielewi, bali ipo mbali na wao.

Tanzania imejengwa kwa misingi ya kuwa kitovu cha Kiswahili duniani. Mtu ambaye amepata tunu ya kuongoza Taifa, si vema sana kutoa kipaumbele kwa Kiingereza, halafu Kiswahili kinabaki nyuma.

Tafakari; kama kitabu ni cha Rais wa Tanzania na walengwa wakuu ni Watanzania (Waswahili), ni toleo gani lilipaswa kuanza, Kiingereza au Kiswahili?

Vinginevyo ielezwe kuwa kitabu si cha Watanzania, kinahusu watu wengine. Ikielezwa hivyo, litaulizwa Sali jingine, kinatafsiriwa ili iweje? Si kibaki kwenye lugha hiyohiyo ya awali?

Tanzania haiwezi kuwa Taifa lenye kupigania lugha yake ya Taifa kukua na kuzungumzwa duniani, ikiwa viongozi wake wanatoa kipaumbele kwa Kiingereza.

Yapo mambo ya msingi ambayo Watanzania wangependa kuyasoma. Mkapa ameeleza mengi mno. Wizi wa fedha Benki Kuu kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) na majuto ya kisiasa kwa maafa ya Wazanzibari Januari 26 na 27, 2001.

Mkapa ametoa maoni ambayo yanagusa hali ya mkwamo wa kisiasa uliopo. Ni mambo ambayo yalipaswa kuwekwa kwa Kiswahili kwanza kabla ya Kiingereza.

Kikwete naye anayo mengi, baadhi aliyaeleza katika kongamano la kusoma kitabu chake huko Marekani. Aligusia jinsi alivyoshawishiwa kugombea urais na alivyopata uteuzi wa serikali na kadhalika.

Alipokuwa naibu waziri, mwaka 1990, yeye na mawaziri wengine walijikuta wakiranda kwa miguu barabarani kutokea Ikulu, baada ya kuamriwa na Rais Ali Hassan Mwinyi, wajiuzulu ghafla. Hawakuwa hata na usafiri.

Simulizi hizi ni za Watanzania ambao ndio wenyeji wa Kiswahili. Wanatakiwa waipate kwa utamu wake katika lugha yao adhimu, wanayoipenda na kuikumbatia. Kuanza na Kiingereza kisha Kiswahili kifuate ni kuwachelewesha.

Mei 9, mwaka huu, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Fredrick Shoo, alipokuwa anaongoza misa ya kumuombea marehemu Reginald Mengi, alitaka kitabu chake cha “I Can, I Must, I Will: The Spirit of Success” kitafsiriwe kwa Kiswahili ili Watanzania wengi wakisome.

Dk Shoo alifikisha ujumbe kuwa lugha ya Watanzania ni Kiswahili. Mwalimu Nyerere pia alipotafsiri vitabu vya Shakespeare alifikisha maudhui kuwa Watanzania chao ni Kiswahili. Mkapa na Kikwete wanawarudisha kule ambako Mwalimu aliwatoa.

Pamoja na hivyo, pongezi kwao kwa kuandika vitabu. Mwalimu Nyerere aliandika vitabu vingi. Hakuandika cha maisha yake. Rais Mwinyi bado yupo hai. Ana deni la kuandika kitabu. Mungu amwezeshe.

Columnist: mwananchi.co.tz