Kila mwanzo wa mwaka ni wakati wa kutegemea mambo mapya kisiasa, kijamii, kibiashara na uchumi. Watu hata taasisi mbalimbali hutegemea mambo mapya kutokea ndani ya mwaka mpya.
Ni muhimu kukumbuka kuwa hali ya uchumi wa mtu mmoja mmoja, kaya, jamii, taasisi au nchi haitabadilika kwa sababu tu mwaka umebadilika. Kinachofanya uchumi kubadilika ni zaidi ya mabadiliko ya mwaka.
Ukuaji wa uchumi ni ongezeko la thamani ya fedha ya bidhaa na huduma zinazozalishwa katika nchi kwa kipindi fulani. Kwa kawaida kipindi kinachozingatiwa na wataalamu huwa mwaka mmoja.
Kukua kwa uchumi hakutegemei kubadilika kwa mwaka. Kinachotakiwa ni kuongeza thamani ya fedha ya bidhaa na huduma zinazozalishwa. Uchumi unaweza kukua kama bidhaa na huduma zinazozalishwa ndani ya mwaka husika ni nyingi kuliko mwaka uliopita.
Huu ni ukuaji halisi. Ukuaji huu hautegemei mwaka kubadilika bali mambo yanayochangia kuongezeka kwa uzalishaji. Mambo haya hutofautiana kutoka sekta moja hadi nyingine.
Kwenye kilimo kwa mfano, pamoja na mambo mengine ukuaji hutegemea hali ya hewa, upatikanaji wa pembejeo, masoko, miundombinu ya umwagiliaji na usafirishaji pia. Kwa ujumla ukuaji wa kila sekta hutegemea mazingira rafiki, wezeshi na ya kuvutia uzalishaji.
Uchumi unaweza kukua kwa sababu ya ongezeko la bei za bidhaa na huduma zilizozalishwa. Hivyo ni muhimu kutofikiri kuwa uchumi utakua au kutokukua kwa sababu mwaka umebadilika. Ni lazima kuwepo na visababishi vya uchumi kukua kwa wingi na ubora unaotakiwa.
Mfumuko wa bei ni ongezeko la jumla la bei ya huduma na bidhaa. Kama ilivyo kwa ukuaji wa uchumi, mfumuko wa bei haubadiliki kwa sababu mwaka umebadilika.
Kwa nchi kama Tanzania mfumuko wa bei ni suala la kimfumo kuliko fedha. Bado mfumuko wa bei unategemea mwenendo wa mvua. Hii ni kwa sababu mvua zina umuhimu mkubwa katika kilimo huamua kiasi cha mazao ya chakula kitakachopatikana.
Chakula na bei yake vina umuhimu katika kuamua mfumuko wa bei kwa sababu asilimia kubwa ya kipato cha wananchi hutumika kununua vyakula hivyo kuathiri ukokotoaji wa bei kwa ujumla.
Ni bahati nzuri kwamba mfumuko mpaka mwishoni mwa mwaka 2018 ulikuwa wa tarakimu moja ambao ni mzuri (kidogo zaidi ya asilimia nne). Kama ilivyo kwa ukuaji uchumi, mfumuko wa bei kwa mwaka 2019 utategemea visababishi vya kupanda na kushuka kwa bei za bidhaa na huduma muhimu.
Uimara wa sarafu ya nchi hutegemea mambo kadha wa kadha ikiwamo upatikanaji wa fedha za kigeni. Fedha hizi hupatikana kwa kuuza bidhaa na huduma nje ya nchi. Kwa kadiri nchi inavyouza zaidi nje ya nchi ndivyo inavyopata zaidi fedha za kigeni kama vile Dola ya Marekani.
Kadri fedha hizi zinavyokuwa nyingi ndivyo sarafu ya nchi kuwa imara zaidi kwa sababu zitahitajika fedha kidogo za ndani kupata fedha ya nje. Kama nchi ikinunua zaidi kutoka nje ya nchi kuliko inavyouza, husababisha fedha za kigeni kuwa chache hivyo kushusha thamani ya sarafu ya ndani.
Vilevile, fedha za kigeni huifanya sarafu kuwa imara iwapo wananchi wanaoishi ughaibuni watatuma kiasi kikubwa nyumbani, fedha kutoka kwa wawekezaji na misaada na mikopo ya fedha za kigeni kutoka nje ya nchi.
Haya yote hayatokei kwa sababu mwaka umebadilika bali kwa sababu ya mazingira rafiki hivyo kuimarisha sarafu.
Kati ya mambo makuu kiuchumi ni ajira. Hii ni kwa sababu ya umuhimu wake katika maisha ya mtu mmoja mmoja, kaya, jamii na Taifa kwa ujumla. Ajira inaweza kuwa ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja.
Bila kujali aina, hali ya ajira katika nchi yoyote hutegemea mwenendo wa uchumi wa nchi husika siyo kubadilika kwa mwaka. Kadri hali ya uchumi inavyokuwa nzuri ndivyo ajira zinavyoshamiri. Kinyume chake ni kweli pia.
Waajiri huajiri kama kuna haja ya kufanya hivyo ambayo hutokana na hali ya uchumi kama vile uhitaji wa bidhaa na huduma itakayozalishwa. Kwa misingi hii, hali ya ajira haitabadilika kwa sababu mwaka umebadilika bali kutegemeana na mwenendo wa mambo makuu na ya msingi yanayochangia kuwepo au kutokuwepo kwa ajira.