Mvutano unaoendelea kati ya Spika wa Bunge, Job Ndugai na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hisabu za serikali (CAG), Profesa Mussa Assad si tu unatishia kuibuka kwa mgogoro wa kikatiba bali pia unauweka rehani uhuru wa taasisi zinazopaswa kusimamia uwajibikaji ndani ya serikali na taasisi zake.
Kufuatia hatua yake ya kumtaka CAG kesho atokee mbele ya kamati ya Maadili, kinga na madaraka ya Bunge kufuatia kauli yake kuwa Bunge ni dhaifu, Spika Ndugai ameibua mjadala unaoendelea kurindima kutoka kila kona ya nchi huku wananchi wakihoji agizo hilo la Spika wakisema kwamba si tu linaenda kinyume na katiba bali pia sheria zingine za nchi.
Baadhi ya wadadisi wa mambo wana hofu ya uwepo wa shinikizo nyuma ya suala hilo zaidi ya tunaloambiwa. Lakini madai hayo yamekanushwa na Ndugai akisema hakuna mtu yeyote mwenye nia mbaya dhidi ya mwingine kwenye mzozo huo
Azungumza na waandishi wa habari baada ya kikao cha Kamati ya Uongozi ya Chama cha mabunge ya Jumuiya ya Madola Kanda ya Afrika (CPA) kilichokutana katika ofisi za Bunge, Dar es Salaam, Ndugai alisisitiza kuwa Profesa Assad akiwa ofisa wa Bunge amelidhalilisha Bunge na lazima aitikie wito uliotolewa.
Akifafanua hoja hiyo, Ndugai anasema kwa mujibu wa taratibu wa mabunge ya Jumuiya ya Madola, CAG ni ofisa wa Bunge.
Hata hivyo, katiba ambayo inaipa ofisi ya CAG kiwango kikubwa cha uhuru chini ya ibara ya 143, uhuru ambao pia unahakikishwa na Sheria ya Ukaguzi ya mwaka 2008 haielezi kwamba ni ofisa wa Bunge.
Hata hivyo, katika chapisho lenye kichwa cha habari ‘Usimamizi wa Bunge kwa CAG’ lililochapishwa katika mtandao wa Academia, mtafiti kutoka Taasisi ya Utawala wa Umma nchini India, Govind Bhattacharjee anasema taratibu kuhusu nafasi ya CAG hutofautiana kati ya nchi na nchi zinazofuata mfumo wa Jumuiya ya Madola.
“Kwa baadhi ya nchi, CAG anakuwa ni afisa wa Bunge ambalo humuhakikishia uhuru wake dhidi ya mhimili wa serikali, kama Uingereza na Australia, wakati kwenye nchi zingine, kama vile India, CAG yuko huru dhidi ya serikali na Bunge lenyewe.” Dk Bhattacharjee anasema kwamba hata pale inapotokea kuwa CAG ni ofisa wa Bunge, “kanuni zinazoanzishwa na taratibu zingine za kimaadili kwa kiasi kikubwa zinalinda uhuru wa CAG.”
Katika mazungumzo yake ya kwanza tangu mzozo huo uibuke, Profesa Assad mbali na kuweka wazi kwamba yuko tayari kuitikia wito wa Bunge ili kudumisha uhusiano uliopo kati ya vyombo hivyo viwili, alisema maneno yake yaliyozua mjadala hayakuwa na nia ya kulidhalilisha Bunge hata kidogo.
“Maneno kama ‘udhaifu’ na ‘mapungufu’ ni lugha ya kawaida sana kwa wakaguzi katika kutoa maoni ya utendaji wa mifumo ya taasisi mbalimbali,” alisema Profesa Assad.
Akijaribu kutoa ufafanuzi wake katika mvutano unaoendelea, wakili Jebra Kambole anasema ofisi ya CAG, kama ilivyo kwa Bunge, imeanzishwa na Katiba ambayo pia inatoa nguvu na mamlaka yake. Katika msingi huo , wakili Kambole anaiita kauli ya Spika ya kusitisha kufanya kazi na CAG kama uvunjifu wa katiba.
Kambole anasema kwamba kwa mujibu wa ibara ya 29(I) ya katiba inasema kila mtu, haijalishi nafasi yake, ana wajibu wa kuitii katiba. “Kama hivyo ndivyo, uamuzi wa Spika unaashiria utayari wake kukiuka ibara hii na kwamba majukumu yake hayataendelea tena kuongozwa na katiba.”
Kuna wasiwasi kwamba madai yanayooendelea kutolewa na Spika kwa CAG yanafanya iwe ngumu uwezekano wa kuwa na taasisi imara, jumuishi na zinazowajibika. Kambole anadhani kuwa katika mazingira ya uvunjifu wa wazi wa katiba, lengo la kuwa na taasisi madhubuti litabaki kuwa ni ndoto.
“CAG punde anatarajiwa kwenda kukagua matumizi ya Bunge, sasa unajiuliza hiyo inawezekanaje katika mazingira ambayo Spika amesema ofisi yake haitofanya kazi tena na CAG? Si tu kwamba jambo hili halikubaliki bali pia ni kichekesho,” anabainisha Kambole.
Wakati mvutano ukiwa unaendelea, wahanga wakubwa wa jambo lenyewe wametajwa kuwa ni wananchi wa kawaida na walipa kodi wa taifa hili.
Mhadhiri wa sayansi ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk Paul Luisulie ameuita mvutano huu wa bahati mbaya sana na kwamba haukupaswa hata kuibuliwa.
“Tafsiri ya vurugu zote hizi ni kwamba mwananchi wa kawaida, ambaye anapambana kila siku ili kuiwezesha serikali yake kutekeleza majukumu yake kwa kuhakikisha kwamba analipa kodi inayotakiwa, ataachwa gizani kwa kutojua jinsi kodi yake inavyotumiwa,” anasema Dk Luisulie.
Anasema kwa kukataa kufanya kazi na CAG, Spika Ndugai amezipa uhuru taasisi za serikali kufanya zinavyojisikia na pesa za umma kwani wanajua kuwa hata kama CAG atawakagua hakuna kitakachotokea kwani Bunge litaacha kufanyia kazi ripoti za CAG.
Ni katika mazingira haya basi ambapo baadhi ya wadau wameshauri busara ichukue mkondo wake ili kurejesha hali katika utulivu. Hata CAG mwenyewe amesema ameona ni busara kuitikia wito wa Spika pengine akidhani kwamba kwa kufanya hivyo jambo lenyewe litaisha.
Ni busara hiyohiyo ambayo mratibu wa mtandao wa watetezi wa haki za binadamu (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa amewaomba wazee wastaafu wa taifa hili kuingilia kati.
Ole Ngurumwa anadhani kwamba Spika Ndugai amedhamiria kulidhoofisha Bunge na ni vyema wazee hawa wakasema hapana na kuingilia kati.
Anashauri: “Wazee wetu hawa wameishi sana na kushuhudia mambo mengi sana, ni wazi kwamba hawaridhishwi na kinachoendelea, basi wasikae kimya, waone jinsi wanaweza kuingilia katika na kutatua huu mtanzuko uliopo sasa.”