Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Muhimu ni ujuzi, sio kujua Kiingereza

11804 Pic+ujizi TanzaniaWeb

Tue, 14 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Imekuwa kama ada kwa kila anayetaka kuwakosoa wahitimu wa vyuo vya elimu ya juu nchini, kudai kuwa wahitimu hao hawaajiriki kwa sababu ya kutojua vilivyo lugha ya Kiingereza.

Mwaka 2015, Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) lilizindua ripoti yake ya mwaka kuhusu nchi zinazoendelea na kudai kuwa mfumo wa elimu nchini hautoi wahitimu wanaoweza kushindana katika soko la ajira.

‘’ Kuna suala la wahitimu wa Tanzania kutojiamni na kukosa stadi zinazowawezesha kushindana katika soko la ajira, huku wengi wao wakishindwa kuwasiliana vilivyo kwa kutumia Kiingereza,’’ilisema sehemu ya ripoti hiyo.

Mshiriki mmoja, raia wa Sychelles, hakuficha hisia zake aliposema Kiingereza kinawaangusha Watanzania. Akinukuliwa na gazeti la The Citizen, alisema:

“ Wahitimu wengi hawajiamini, hawana stadi za kazi na hata Kiingereza ni tatizo kwao. Unaweza kuwa na watu lakini ni tatizo kama hawajui Kiingereza.’’

Kiingereza kipimo cha elimu, ajira

Haishangazi kuwa kauli hii ya kuwaponda wahitimu wa Kitanzania kutojua lugha ya Kiingereza imetoka kwa mtu wa nje.

Huu ndio mtazamo wa waajiri wengi kutoka nje, mtazamo ambao sasa umekuwa kasumba iliyowakumba pia baadhi ya Watanzania.

Kwa walio wengi, lugha ya Kiingereza imekuwa kipimo cha maarifa na elimu aliyo nayo mtu. Ndiyo maana maeneo mengi ya kazi, usaili umekuwa ukifanywa kwa lugha hiyo hata kwa kazi zisizokuwa na uhusiano wowote na ujuzi wa Kiingereza.

Mchambuzi wa sera na masuala ya elimu nchini, Gervas Zombwe anasema kujua Kiingereza kumegeuzwa kuwa sehemu muhimu ya ajira.

“ Hali ilivyo sasa, kupata ajira hapa nchini hakuhitaji maarifa wala ujuzi. Kunahitaji uwezo wa kubwabwaja Kiingereza na jina la mzazi wao tu. Hata kama hujui kusoma na kuandika, ukipiga Kiingereza utapata ajira kiurahisi.”

Ninaungana naye anaposema kuwa Kingereza sio tu ni lugha ya mawasiliano bali ni lugha ya ajira, ambayo hutumika kama kama kikwazo cha wanyonge kupata ajira. Kikwazo hiki anasema kimewekwa na mabepari ili waendelee kuwanyonya wanyonge.

Ni kweli kuwa Kiingereza ndiyo lugha ya mawasilaino ya dunia, na ni lugha muhimu kila mtu kuijua. Lakini hatuna budi kuelewa kuwa ipo tofauti kati ya mtu kusoma kwa minajili ya kupata maarifa ya fani husika na kujua Kiingereza.

Ukweli ni kuwa sio kila mhitimu wa elimu ya juu nchini amesomea upokeaji simu ofisini au utoaji huduma kwa wateja, kiasi kwamba alazimike kukijua Kiingereza hasa anapohudumia wageni.

Kwa mfano, hivi sasa Tanzania imo katika harakati za uchimbaji wa mafuta, gesi na madini mengine kama urani. Kuendesha mtambo wa kuchimba mafuta hakuhitaji mhusika kujua ‘is’ na ‘was’ pekee.

Kunahitaji maarifa ambayo kimsingi yanaweza kupatikana kupitia lugha yoyote.

Ni kasumba tu iliyojaa katika vichwa vya waajiri wageni na hata wazawa, kukiona Kiingereza kama kigezo pekee cha maarifa ya mtu na kisha kumpa mtu huyo ajira.

Tembelea viwandani, wageni ndio wanaoongoza vitengo, sababu kubwa ni kasumba tu kuwa wageni ndio wanaoweza kuendesha mambo hata kama hawana maarifa ya kutosha. Wanahusudiwa kwa kuwa wanakijua Kiingereza.

Kibaya zaidi katika baadhi ya maeneo, wataalamu wazawa wenye maarifa yaliyotukuka wanaongozwa na wageni ambao wengine hata hicho Kiingereza wanazungumza kwa kuokoteza maneno.

Ugeni na kutojua Kiingereza ni ghiliba tu zinazotumiwa na wawekezaji kutothamini wazawa.

Kiingereza kinatumika kuwavunja moyo wataalamu wa ndani, hata wanapoajiriwa wajione kuwa walipendelewa kupewa nafasi.

Tatizo lililopo

Kutojua Kiingereza katu hakuwezi kuwa sababu pekee ya kuwahukumu wahitimu wetu kuwa hawana uwezo hivyo hawawezi kuajirika.

Kinachoweza kukubalika kwa walio wengi na ndiyo mtazamo wa mwandishi wa makala haya ni kuwa mfumo wetu wa elimu una dosari za kushindwa kuwaandaa wahitimu wake kujiamini, kufikiri, kutatua matatizo kazini na katika jamii na hata kukosa stadi za kushindana na wengine.

Haya yote ni kwa sababu wahitimu hawa wanafundishwa katika mfumo ambao maarifa yamejaa nadharia zaidi kuliko vitendo. Ni jambo la haki zaidi kwa wanaowaponda wahitimu wetu kulisemea hili, lakini sio kudai kila siku kuwa Kiingereza ndicho kinachowaangusha katika soko.

Wajapan, Wajerumani Wafaransa na mataifa mengine kadhaa leo yameendelea, yanashindana na hata kuyazidi mataifa yanayotumia Kiingereza, Kwa nini wamefikia hapo?

Hawa hawakutumia Kiingereza kupata mafanikio ya kielimu, sayansi, teknolojia na uvumbuzi wanavyotamba navyo sasa.

Wachina sasa wanaongoza duniani. Tanzania sasa imekuwa kimbilio lao, kila kona wako wao na kampuni zao.

Haya ni matunda ya maarifa waliyotoa kwa wahitimu wao kupitia lugha yao ya Kichina.

Tukune vichwa Watanzania, tupambane na ghiliba za wageni kuwa wahitimu wetu ni bomu kwa kuwa hawajui Kiingereza.

Kujenga daraja, kuendesha gari hakuhitaji kujua Kiingereza. Kwa nini mzawa atoswe katika ajira kwa kigezo rahisi cha kutojua Kiingereza?

Kutojua Kiingereza ni ghiliba na hoja nyepesi inayotolewa na waajiri wasiowatakia mema wahitimu wazawa.

Columnist: mwananchi.co.tz