Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mtukudzi kaondoka, ametuachia kina Bitchuka wa ujamaa

38751 Edo+Kumwembe Mtukudzi kaondoka, ametuachia kina Bitchuka wa ujamaa

Tue, 29 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Oliver Mtukudzi alizaliwa Zimbabwe enzi hizo za makaburu wakati huo Zimbabwe ikijulikana kama South Rhodesia. Mzungu alikuwa ameshika hatamu. Ilikuwa nchi ya kibepari kwelikweli. Maisha yalikuwa ya kibepari.

Moja kati ya mazao mazuri ya ubepari wa Zimbabwe ni mtu huyu anayeitwa Mtukudzi. Amefariki wiki iliyopita. Baada ya kugundulika kuwa ana kipaji, watu wenye akili zao walimzunguuka Mtukudzi na kumfanya kuwa jina kubwa barani Afrika.

Aliimba nyimbo ambazo wengine lugha yake hatukuielewa vyema lakini bado zimebakia kuwa maarufu kwetu. Umaarufu wake ukavuka nje ya Zimbambwe. Ukavuka nje ya Afrika. Hii ni kazi ya ubepari, kipaji na pesa.

Tanzania haikuwa hivyo. Wazee wetu kina Hassan Rehani ‘Bitchuka’ na wengineo waliambiwa waimbie nyimbo za kusifu chama kilichopo madarakani na ukombozi wa Afrika. Hawakuufanya muziki kuwa biashara, hakukuwa na watu waliowazunguka ambao walikuwa tayari kuwatafutia pesa na masoko ya nje. Akina Bitchuka waliambiwa tu waimbe kwa sababu za kizalendo.

Sauti za kina Bitchuka ni zaidi ya Mtukudzi. Kipaji cha Bitchuka ni zaidi ya Mtukudzi. Tungo za Bitchuka ni zaidi za Mtukudzi. Kilichowatofautisha ni sera za nchi walizotoka na zama walizokuwapo. Kwa Mtukudzi kipaji ni pesa. Kwa Ujamaa wa Tanzania ile, kipaji chako kinapaswa kutumika kwa ajili ya kujenga uzalendo, basi.

Katika maisha yao ya zamani kina Bitchuka hawakuwa na menejimenti na mpaka leo hauwezi kusikia Mzee Bitchuka ana meneja. Haya ndio maisha ya kijamaa yalivyo. Maisha ya Kibepari ya kina Mtukudzi tayari wazungu walishamzunguuka siku nyingi kwa ajili ya kujipatia pesa na pia kumpatia pesa. Ndivyo ilivyo.

Leo tayari rafiki zake Bitchuka wengi tu wenye vipaji kama yeye wametangulia mbele ya haki wakiwa masikini. Watoto wao pia ni masikini. Nyimbo zao za kusifu chama na ukombozi wa Afrika bado zinapigwa kila mahala.

Nadhani yote haya ndio ambayo Diamond Platinumz anajitahidi kuyafuta. Anajaribu kuzunguka dunia nzima kujitangaza na kujipatia pesa. Hana wimbo hata mmoja ambao unazungumzia ukombozi wa bara la Afrika, lakini kuna asilimia kubwa akafa akiwa tajiri. Maisha bwana!



Columnist: mwananchi.co.tz