Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mtoto aliyezaliwa kwenye nyasi ni tukio tata kwa Jeshi la Polisi

9822 Liquman TZWeb

Sun, 24 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwalimu darasani aliamua kuwadadisi wanafunzi wake wa darasa la tatu ili kupima uwezo wao wa kufikiri. Aliwauliza darasa zima lenye watoto 40, kila mmoja kwa utashi wake ni kazi gani angependa aifanye ukubwani na ipi asiyoitamani kabisa.

Yalitoka majibu ya kila aina, lakini mwalimu aliamua kuwaita mbele watoto wawili ambao mmoja alisema anapenda akiwa mkubwa awe polisi na mwingine alijieleza kwamba kamwe asingetokea kufanya kazi ya upolisi hata ikiwa na masilahi makubwa kiasi gani.

Kilichomfanya mwalimu awaite mbele watoto hao wawili ni kutaka kujua sababu nyuma ya kila mmoja kuipenda au kuichukia kazi ya upolisi. Aliamini kuwa angeweza kutoa somo zuri kwa wanafunzi wengine wote kutambua kwamba kila mmoja ana uchaguzi wake, unachoweza kukipenda wewe, mwingine anakichukia.

Mtoto aliyesema akiwa mkubwa anatamani awe polisi alisema kuwa alivutiwa na upolisi kwa sababu wakati fulani kwenye nyumba waliyokuwa wakiishi, walivamiwa na majambazi. Wale majambazi walikuwa na taarifa kwamba ndani ya nyumba hiyo kulikuwa na mtu mwenye fedha nyingi.

Kulikuwa na familia tatu zilizokuwa zikiishi kwenye nyumba hiyo. Ikatokea wale majambazi wakawa hawana uhakika ni baba wa familia ipi alikuwa na fedha. Walichokifanya, waliamua kuziteka familia zote tatu, wakawa wanawatesa na kuwatisha kuwaua, lengo likiwa kumfanya mwenye fedha ajitokeze na aseme zilipo.

Wakiwa wanaendelea kuwatisha na kuwatesa, miongoni mwa wale majambazi, kulikuwa na waliokuwa wakipita vyumbani kutafuta mahali fedha zilipo. Walipokosa, ilibidi watumie njia ya mwisho ambayo ilikuwa kuua watoto. Waliamini wangemshika mtoto kumuua, baba mwenye fedha asingekubali mwanaye auawe, angetaja.

Yule mtoto alisimulia kuwa jambazi mmoja alimkamata na kumwekea bastola kichwani na kutishia kumuua endapo asingetokea mwenye fedha kusema alipoziweka. Mtoto alikuwa akilia akiwaita wazazi wake waende kumsaidia, lakini ghafla alisikia mlio mkali wenye kishindo na yule jambazi akawa ameanguka, akapoteza nguvu ya kumshika, hivyo mtoto naye akaanguka.

Pia, alisema alishuhudia jambazi mwingine aliyekuwa silaha akianguka chini. Baadaye alikuja kutambua kuwa jirani yao ambaye alikuwa askari polisi, baada ya kutambua kulikuwa na uvamizi, aliamua kutumia vema mafunzo yake ili kuwaokoa.

Yule polisi alivunja dirisha na kuingia ndani, akitembea kwa kuchukua tahadhari zote za kiaskari, alifanikiwa kuwaona majambazi wakiwa wamewaweka chini mateka. Alibaini majambazi wawili ndiyo walikuwa na silaha. Wakati akipiga hesabu namna ya kuwakabili, alishuhudia mtoto akishikwa na kuwekewa bastola kichwani.

Alipiga hesabu zake kisha akafanya shambulizi la kushtukiza kwa kumpiga risasi moja ya kichwa yule aliyekuwa amemshika mtoto na kumwekea bastola, bila kuchelewa alimpiga na yule mwingine aliyekuwa na bunduki. Baada ya hapo aliziokoa zile familia zote tatu.

Alipofanikisha uokoaji, yule askari aliwaweka chini ya ulinzi wale majambazi wengine na kuwafikisha kituo cha polisi, baadaye walipelekwa mahakamani kisha wakafungwa. Mtoto alisema kwa tukio hilo, aliona umuhimu wa polisi. Kuanzia siku hiyo huwachukulia polisi kuwa ni watu jasiri na mashujaa.

Mtoto anayechukia polisi

Alisema waliishi na jirani yao mkorofi aliyekuwa na jeuri kubwa ya fedha. Ilitokea siku katika michezo ya watoto, yeye aligombana na mtoto wa yule jirani. Jioni wakiwa nyumbani yule jirani alifika kwao na kufoka sana, aliwatuhumu wazazi wake kuwa ndiyo walimtuma akampige mtoto wake. Mwisho aliahidi kuwaonyesha cha mtema kuni.

Yule jirani alipoondoka, kilipita kitambo kidogo kisha nyumba yao ilivamiwa na polisi ambao waliwapiga baba na mama yake pamoja na yeye. Baada ya hapo waliwakamata na kwenda kuwalaza mahabusu ambako walikaa siku tatu mpaka yule jirani yao mkorofi alipokwenda kituo cha polisi kuwaagiza polisi wawaachie huru.

Mtoto yule alisema kuwa walipokuwa wanaachiwa pale kituoni, polisi mmoja aliwaambia wana bahati jirani yao aliamua kuwasamehe, vinginevyo wangewapa kesi wafungwe hata miaka 10. Kutokana na tukio hilo, yule mtoto alichukulia kazi ya kipolisi kuwa ni ya kikatili na uonevu.

Aliwaona polisi ni watu ambao wanaweza kutumiwa na wenye fedha ili kuwaonea wanyonge. Ushuhuda wake pamoja na wazazi wake kupigwa na kulazwa mahabusu siku tatu bila kosa lolote, ulimfanya ajenge chuki. Ndiyo maana alimwambia mwalimu wake kwamba upolisi ni alama ya kumuasi Mungu.

Wakati mtoto akimaliza kusimulia, alikuwa akilia. Baadhi ya wanafunzi wenzake pia walilia kwa tukio hilo alilosimulia. Mwalimu alimbembeleza na kumwongoza kurejea kwenye dawati lake. Hata mwanafunzi aliyesema anapenda upolisi alikuwa mnyonge.

Mwalimu aliwaambia wanafunzi wote wampe pole mwenzao ambaye alikuwa akiendelea kulia. Ni dhahiri simulizi ya matukio mawili ya polisi yalikuwa yameyeyusha mpangilio wa somo alilotaka kuwapa wanafunzi wake.

Hata hivyo, mwisho alimudu kuwaambia kuwa upolisi ni kazi nzuri, ila kuna watu wachache ambao ni wabaya hufanya kazi ya upolisi.

Wote walikuwa sahihi

Mtoto aliyesema anataka kuwa polisi alikuwa sahihi. Wapo askari waaminifu na waadilifu mno kwenye viapo vyao. Mfano mmojawapo ni huyo aliyesaidia familia ya huyo mtoto pamoja ni majirani zao.

Lipo tukio la askari wa usalama barabarani aliyefanikiwa kuwadhibiti majambazi katika eneo la Ubungo Mataa, Dar es Salaam, waliokuwa wakijaribu kupora fedha za Benki ya NMB miaka michache iliyopita.

Askari wa mfano huo kwa nini asishawishi watoto kupenda upolisi? Ni watu ambao hutambua kua kiapo chao cha kulitumikia jeshi kimejengwa kwenye utoaji wa huduma. Watoto huitwa malaika, kwa hivyo hupenda matendo mema. Hiyo ni sababu askari wema huwavuta kutamani kuwa kama wao.

Tafsiri hiyohiyo kuwa watoto ni malaika, basi huchukia matendo mabaya. Wanapoona askari wanatenda uovu kwa raia hujenga chuki. Kwa hivyo, mtoto asiyependa upolisi ni kiwakilishi kizuri cha hisia za watoto pale wanaposhuhudia mambo mabaya yenye kutendwa na polisi.

Wanasaikolojia wanashauri kumlinda mtoto na mambo mabaya. Hata kitendo cha baba kumpiga mama hutosha kumharibu mtoto, sembuse polisi wenye sare na bunduki kuwapiga wazazi wake wote wawili, kisha kuwaweka mahabusu. Mtoto yule ana haki ya kuchukia upolisi.

Ukatili wa kipolisi na matukio yote ya uhalifu unaohusisha polisi hujenga jamii mbaya mno. Nadharia ya hisia hasi juu ya sheria kwa sehemu kubwa husababishwa na polisi kutotimiza wajibu ulio ndani ya viapo vyao.

Wanyonge wanaona sheria hazina msaada, wababe wanaamua kusigina sheria na mifumo yake kwa jeuri kubwa.

Sikitiko la juu kabisa ni nchi kuwa na askari ambao hawajui dhima ya kuitwa polisi. Matokeo yake wanatengeneza chuki na raia mpaka na watoto. Polisi linakuwa jeshi lenye kuvamiwa na watafuta kazi na mshahara kuliko wito wa kuhudumia jamii na Taifa.

Columnist: mwananchi.co.tz