Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mtoto Anthony sasa si yule wa Kabanga

28866 MTOTO+PIC TanzaniaWeb

Mon, 26 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katikati mwa mwaka huu mtoto Anthony Petro mkazi wa Kijiji cha Ngundusi, Kata ya Kabanga mkoani Kagera picha na video zake zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii pale alipotishia kumfikisha polisi baba yake.

Alifikia hatua hiyo baada ya kutilia shaka kwamba mzee wake huyo Petro Magogwa (67), alikuwa na mpango wa kuuza shamba lao, jambo aliloona linaweza kumweka pabaya yeye na ndugu zake wawili Editha Petro (13) na Eliza Petro (8) ambao hawana rasilimali nyingine yoyote zaidi ya shamba hilo.

Kutokana na hali halisi ya familia yake, licha ya udogo wake Anthony alikuwa akilazimika kwenda kutafuta chakula na anapopata hurudi nyumbani kuja kula na ndugu zake.

Kusambaa kwa video na picha hizo kukawa neema kwa Anthony (10) baada ya kujitokeza Isihaka Msuya, aliyejitolea kumfadhili kimasomo na kumhamisha kutoka Shule ya Msingi Ndungusi kwenda shule ya Amani Vumwe English Medium iliyoko Mwanga, Kilimanjaro.

Mbali na Msuya pia baadhi ya wasamaria wema walianzisha Umoja wa Wana Ngara Kumsaidia Anthony, ambao huichangia familia hiyo chakula na mavazi kila mwezi.

Mhasibu wa umoja huo, Stela Rutaguza na mhamasishaji wa kundi hilo, Gubas Vyagusa, wanasema mpaka sasa wameshatoa vitu vyenye thamani ya Sh365,000 kati ya Sh3.8 milioni zilizotolewa na walioguswa na maisha ya Anthony na familia yake.

Baada ya kuwasili katika shule hiyo, Anthony amekuwa na maendeleo mazuri yanayowavutia walimu na wale wanaojitolea kumsaidia yeye na familia yake.

Vyagusa alimtembelea mtoto huyo Mwanga anakoendelea na masomo ambapo anasema akiwa huko alielezwa na walimu wake kuwa Anthony anaendelea kufanya vizuri darasani akijifunza lugha ya kiingereza, kiswahili, hesabu, kusoma na kuandika.

“Nilifarijika kumuona Anthony anajiamini akionyesha ushirikiano na upendo kwa wanafunzi wenzake na kuwapa matumaini walimu na mlezi wake,” anasema Vyagusa.

Vyagusa anasema mtoto huyo amebadilika kimazingira kwa kujifunza lakini mapenzi yake makubwa bado yapo kwa familia hasa baba na ndugu zake Editha ambaye ni dada yake na Eliza mdogo wake.

“Walimu waliniambia wakati mwingine Anthony huomba atafutiwe baba yake kwa simu ili aongee naye.

“Wakati mwingine huonekana mnyonge na anapotafutiwa baba yake kwa simu na kuzungumza naye hufurahi na kurudi katika hali ya uchangamfu,” anasema Vyagusa.

Kwa upande wake Msuya ambaye pia ni mmiliki wa shule ya Amani Vumwe English Medium, anasema licha ya kuchelewa kujiunga na wenzake lakini katika mtihani wa kufunga muhula, Juni mwaka huu, alishika nafasi ya 10 kati ya watoto 16 walioko darasa la pili.

“Mara kwa mara nimekuwa nikizungumza na walimu na mlezi wake wa karibu ambaye ni meneja mstaafu wa shule yetu, Paulina Mndeme wananiambia Anthony ni kijana mwema.

“Ni mtiifu, msikivu ana upendo na mwenye kupenda kujifunza kila siku,” anasema.

Matumaini ya kupata nyumba

Wakati anapatikana mfadhili wa kumsomesha Anthony katika Shule ya Amani Vumwe English Medium huko Mwanga, pia alijitokeza mfadhili mwingine (Millard Ayo) aliyeahidi kujenga nyumba ya familia hiyo ambayo ujenzi wake tayari umeanza.

Millard mtangazaji wa kituo cha redio cha Clouds aliongoza uchangishaji uliofanikisha kupatikana kwa fedha zilizotumika kununua kiwanja katika Kijiji cha Ngundusi, Kata ya Kabanga, vifaa vya ujenzi na kuanza ujenzi ambao sasa umefikia hatua ya linta.

Hata hivyo, inafika miezi mitano sasa ujenzi huo umesimama tangu ulipofikia hatua hiyo huku kukiwa hakuna maelezo ya kitu gani kinakwamisha.

Msimamizi wa ujenzi anayemwakilisha Millard kutoka Manispaa ya Bukoba, Lameck Leonard hajaeleza chochote juu ya kusimama kwa ujenzi huo.

Alipotafutwa Millard kueleza kilichokwamisha, simu yake ya kiganjani kwa siku nne mfululizo iliita bila kupokelewa mara ya mwisho kumpigia ikiwa ni jana saa 9.30 alasiri.

Ahadi ya kuisaidia familia ya Mzee Petro Magogwa ambaye ndiye baba mzazi wa Anthony ilianza kutolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, Aidan Bahama aliyeahidi kununua eneo lililo karibu na makazi ya watu na kilimo ili kumhamisha mzee huyo ambaye kwa sasa anakoishi ni mbali na makazi ya watu na huduma za kijamii ikiwamo hospitali.

Mkurugenzi huyo alitoa ahadi hiyo baada ya kuitembelea familia hiyo akiambatana na Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Ngara, Musa Balagondoza na waandishi wa habari ambapo hakuridhishwa na mazingira aliyokuta akiishi mzee huyo na familia yake akiwamo Anthony na wadogo zake wanaosoma darasa la pili katika Shule ya Msingi Ngundusi.

Pia, alirudia ahadi hiyo wakati akimkabidhi Anthony katika Shule ya Amani Vumwe English Medium ambapo aliwahakikishia walimu na mfadhili wake kwamba wadogo zake nao watasomeshwa na familia yao kujengewa nyumba.

Madiwani waweka ngumu

Bahama alipoulizwa umefikia wapi mchakato wa ununuzi wa shamba na kujenga nyumba ya Anthony kisha kuwasomesha wadogo zake, alisema hakupata ridhaa ya baraza la madiwani kutumia fedha za halmashauri kuisaidia familia moja.

Pia, alisema baada ya Millard kununua kiwanja na kujenga nyumba halmashauri ilibaki na jukumu la kuhakikisha inawasomesha wadogo zake katika shule waliyopo sasa kijijini kwao Ngundusi.

“Nitatuma maafisa wa ustawi wa jamii wakawanunulie vifaa na sare za shule ndugu zake Anthony ili waendelee na masomo shuleni hapo,” anasema Bahama.



Columnist: mwananchi.co.tz