Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Msongore: Siyo kila anayefeli ana uwezo mdogo wa akili

10652 SIYO+PIC TanzaniaWeb

Tue, 3 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Siyo kila mwanafunzi anayefanya vibaya darasani ana uelewa mdogo wa kiakili. Kuna sababu nyingi zinazoweza kuchangia ufaulu mdogo kwa wanafunzi.

Mkurugenzi wa asasa ya kiraia inayojihusisha na kutetea maslahi ya watu wenye matatizo ya kisaikolojia wakiwemo wanafunzi shuleni (Tuspo) Pangarasi Msongore, anasema matatizo ya kisaikolojia yanawakumba wanafunzi wengi hivyo kuchangia kuwa maendeleo duni kitaaluma.

“Katika tafiti zetu za kutathmini uwezo wa wanafunzi wa shule za msingi, tumegundua kuwa wengi wanashindwa kufanya vizuri kutokana tatizo hilo,”

Migogoro baina ya wazazi ni moja ya vitu vinavyomsababishia mwanafunzi tatizo la kisaikolojia, kwani anasema endapo wazazi wakiwa wanagombana mara kwa mara, kuna uwezekano wa mwanafunzi kulifikiria suala hilo awapo shuleni.

“Kwa mfano, kuna mwanafunzi mmoja alikuwa anasoma Shule ya msingi Ilula iliyopo Iringa, unyonge wa mwanafunzi huyo akiwa darasani ulitusukuma kuchunguza na kubaini kuwa wazazi wake hupigana kila siku na hurudi nyumbani wakiwa wamelewa. Kwa hiyo matatizo kama haya yanawatesa sana watoto,”anaeleza.

Msongore anataja sababu nyingine kuwa ni watoto kubeba majukumu ikiwemo kuuguza wagonjwa. Wanafunzi wengi hasa wa vijijini wanaathirika zaidi kielimu kwa kubeba majukumu ya kulea familia.

Anasema mwanafunzi wa aina hii hawezi kufanya vizuri darasani kwa sababu muda wote anawaza familia hasa mgonjwa ambaye anamuuguza.

“Hii ni hatari, kwamba mwanafunzi amekuwa mlezi muuguzi na wakati mwingine huwauguza hata wagonjwa wenye maradhi ya kuambukiza hali ambayo ni hatari kwa afya yake,” anasema na kuongeza:

‘’ Hapa utakuta mtoto anasoma lakini akili yake inawaza hali ya mgonjwa nyumbani. Anawaza kama amekula au la, kwa hiyo mwanafunzi wa aina hii hawezi kuwa sawa kisaikolojia.’’

Mtoto kuishi na mzazi mmoja ni sababu nyingine ambayo inamuathiri kisaikolojia, kwani anasema wakati mwingine mwingine anavyowaona wenzake wakiwa na wazazi wote wawili, naye anatamani maisha kama hayo.

“Mara nyingi watoto wa namna hii wanaishi na bibi na babu. Hata ukichunguza utagundua kuwa wanafunzi wanaoishi na bibi au babu hawafanyi vizuri darasani, kwa sababu muda wote wanawaza kuishi kwa furaha na wazazi wao,” anafafanua.

Tathmini ya kupima uwezo wanafunzi

Hivi karibuni Tuspo ilitoa ripoti ya matokeo ya tathmini ya kupima uwezo wa wanafunzi wa shule za msingi katika wilaya ya Ilala.

Katika tathmini hiyo iliyofanyika kwa ushirikiano na shirika la Twaweza katika wilaya 159 za Tanzania Bara, Wilaya ya Ilala imeshika nafasi ya saba huku nafasi ya kwanza ikishikwa na Wilaya ya Iringa.

Katika tafiti hiyo jumla ya watoto 112, 455 walifanyiwa tathmini katika maeneo mbalimbali ya nchi ambayo hufanyika kwa ngazi ya kaya.

Akitoa taarifa ya ripoti kwa wadau wa elimu, Msongore anasema:

“Tuliangalia ni kiwango gani watoto wa darasa la tatu wanaweza kusoma na kufanya hesabu za darasa la pili, tumebaini kwa Ilala ni asilimia 52 ndiyo wanaojua kufanya hesabu za darasa la pili, wanaoweza kusoma hadithi ya Kiswahili ni asilimia 69 na wanaojua kusoma hadithi ya kiingereza ya darasa ni asilimia 26.

Anaongeza: ‘’ Kwa wanafunzi wa darasa la saba, utafiti umebaini kuwa asilimia 19 hawajui kufanya hesabu za darasa la pili, asilimia 13 hawajui kusoma hadithi ya Kiswahili na asilimia 51 hawajui kusoma hadithi ya Kiingereza ya darasa la pili. Hili ni janga kwani wanafunzi hawa wa darasa la saba wanatarajiwa kuingia kidato cha kwanza lakini hawajui kufanya mtihani wa darasa la pilI.’’

Anasema pamoja na wilaya hiyo kufanya vizuri kwa ngazi ya mkoa na kitaifa, utafiti umebauini kuwa mahudhurio ya walimu na ufundishaji kwa ujumla yapo chini na kuongeza kuwa karibu asilimia 25 ya walimu sawa na mwalimu mmoja kati ya wanne hawakuwepo shuleni wakati wa utafiti.

“Hii inaonyesha kuwa muda wa wanafunzi na walimu kukutana darasani wakati wa muda wa shule ni mdogo na hivyo wanafunzi hawapati muda unaopasawa wa kufundishwa ili waweze kujifunza stadi za msingi,” anaeleza.

Changamoto nyingine inayokwamisha maendeleo ya elimu katika wilaya ya Ilala ni wanafunzi kutopata chakula shuleni. Anasema watoto hawawezi kujifunza kwa umakini ikiwa hawapati angalau mlo mmoja kwa siku wakiwa shuleni.

Uongozi wa wilaya wapongeza

Ofisa Elimu Taaluma wa Manispaa ya Ilala, Anna Petro anasema manispaa imepokea ripoti hiyo na kuahidi kuifanyia kazi ili kuleta matokeo chanya.

“Tunapongeza Tuspo kwa kushiriakiana na Twaweza kwa ripoti hiyo waliyoifanya kwa lengo la kuboresha elimu nchini hasa kuibua changamoto mbalimbali ikiwemo tatizo la chakula kwa wanafunzi wakati wa mchana, uhaba wa vyumba vya madarasa na uwiano duni kati ya walimu na wanafunzi juu ya ujifunzaji na ufundishaji,”anasema.

Kuhusu suala la chakula shuleni anasema, Serikali inatoa elimu bila malipo lakini haiwezi kugharimia kila kitu katika katika sekta ya elimu. Anaitaka jamii ishiriki katika maendeleo ya elimu kwa watoto ikiwamo kuwapatia chakula.

Columnist: mwananchi.co.tz