Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mpendwa Rais, “Kilio huanza na mfiwa”, Watumishi wa serikali wana arijojo

28608 Rais+pic TanzaniaWeb

Sun, 25 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

FMwandishi ni mhadhiri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ameandika waraka kwa Rais John Magufuli akieleza kilio cha watumishi wa Serikali. Waraka huo ni huu ufuatao:

Meshimiwa Rais, Novemba Mosi nilifurahi sana kukuona mubashara ndani ya Ukumbi wa Nkrumah wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Nilikaa kule juu, nisingeweza kuonekana hata kama ningenyoosha mkono sana, pale chini nilikosa nafasi; walikaa waalikwa maalumu ambao wanajua kuzungumzia kwa ufasaha masuala ya kitaifa.

Siku ile ya Julai 2015 ulipopata asimilia 87 ya kura za wajumbe wengi wa CCM kuwa mgombea wa urais, nilipata matumaini mapya kuwa hatimaye tumempata Rais mpambanaji na mwenye uchungu na nchi. Vijana wa kijiweni wana msemo wao kuwa wewe ni jembe la Watanzania.

Naomba nikuhakikishie kuwa wananchi tulio wengi tunaridhika kabisa na mapenzi yako makubwa kwa Watanzania na taifa zima kwa ujumla. Jitihada zako zinaonekana. Wewe ni jemedari wetu katika vita hii ya kujiletea maendeleo. Sifa walizokupatia siku ile pale Nkrumah ulistahili bila mashaka yoyote.

Hata hivyo, wahenga walisema kuwa, “Kilio huanza na mfiwa ndipo wa mbali wakaingia”. Siku ile ningepata nafasi kuna jambo moja nilitamani nikuambie kwa niaba ya Watanzania wenye nia njema na kuona unapata mafanikio zaidi katika vita yako dhidi ya rushwa na umaskini. Profesa Rwekaza Mukandala alijaribu kufikisha ujumbe ingawa sijui kama alieleweka.

Naomba nitumie lugha ya picha kujenga hoja yangu

Katika kijiji fulani, kulitokea baba mmoja alikuwa amesafiri kwenda nchi ya mbali alichelewa kurejea nyumbani. Aliporejea nyumbani akagundua kuwa wanakijiji wenzake wameshalima na kupanda mashamba yao. Akaingiwa na hofu kuwa watoto wake watakufa njaa asipochukua hatua kwa haraka.

Mzee yule aliamua kuwafunga punda wake wawili siku iliyofuata na kuwaweka shambani ili walime shamba lake lote la ekari 50 kwa kutumia jembe la kukokotwa (plau). Alilenga kuwa kesho yake punda wale watumike pia kupanda. Ilikuwa ni kazi iliyotakiwa kufanyika kwa wiki mbili lakini yeye alitaka ifanyike kwa siku mbili.

Aliwatumikisha wale punda kwa siku nzima lakini waliweza kulima ekari kumi tu kinyume cha malengo yake ya siku ile. Baadaye akaamua kuwalaza punda wale shambani waendelee kulima lakini waliishia kugoma na kulala chini. Hata alipowapiga fimbo nyingi mgongoni punda wale hawakuamka. Waliishia kugoma.

Si kwamba wale punda hawajui kufanya kazi, la hasha, lilikuwa tatizo la mkulima yule hakukubali kuwa uwezo wa punda haukuwa kulima lile shamba kwa siku moja. Pia, alipaswa kujua kuwa si matakwa yake peke yake bali hata ya punda wanaomfanyia kazi alipaswa kuwajali. Yeye hakuwapumzisha wala kuwapa chakula ili wawe na nguvu za kufanya kazi. Alichopaswa kufanya ni kutafuta msaada wa punda wengine wamlimie mashamba mengine na hivyo siku zingepungua na siyo kuwatesa waliopo.

Hawa punda wako bahati mbaya wana maumivu mengi kuliko unavyoweza kufikiria. Nimeamua kukudokeza hivi kwa nia njema kabisa kwa sababu mimi ni mtu ninayekutakia mafanikio; sitamani kabisa kuona watumishi hawa wakukwamishe katika jitihada zako za ujenzi wa uchumi wa kati.

Hawa watumishi wana njaa, tena hawana motisha. Wengi wao tangu 2015 hawajaonja mshahara mpya, wengine wana madai yaliyolundikana kiasi cha kukatisha tamaa wakiwa wanaishi kwa matumaini ya kuwa labda ipo siku moja watalipwa.

Ni hatari kwa jemedari kuwaagiza askari wako waende vitani ili hali wana njaa na hawana morali. Askari hao wanaweza kukugeuka au wakatumika na adui. Hapa kwetu adui ni rushwa, mafisadi na wahujumu wa maendeleo.

Katika vita hii ya ujenzi wa uchumi, wafanyakazi wa umma ni askari wako wa kukusaidia kutekeleza yale unayotaka wananchi wapate. Zipo baadhi ya sekta zimeelemewa kwa kuwa na watumishi wachache ambao hawawezi kufanya kwa ufanisi. Tunaomba ofisi yako ifikirie kuwapeleka watumishi zaidi maeneo mbalimbali wakawasaidie wenzao wachache kuliko kuwafanyisha kazi nyingi hao wachache waliopo na ufanisi ukapungua.

Tufanyeje?

Tukifanya mambo kadhaa tutaweza kuimarisha utendaji wa watumishi wa umma nchini. Kwanza kabisa ni kuboresha huduma za afya na elimu nchini. Elimu ikiwa bora na huduma za afya zikiimarika naamini watumishi wengi wataridhika na mishahara yao na kutokuwa na wasiwasi kuhusu elimu ya watoto wao na watakuwa hawana hofu ya afya za familia zao na hivyo hata tamaa za kuiba na kuhujumu kazini zitapungua.

Sasa hebu pata picha kidogo. Nesi ambaye maisha yake ni magumu huko Ludewa, Tandahimba, Namtumbo, Ngara, Ikungi, Kasulu nk anampeleka mtoto wake kwa mwalimu ambaye naye ana hali ngumu; hasira zake anazihamishia kwa mtoto wa nesi. Nesi naye hasira zake anazihamishia kwa mtoto wa mwalimu. Kumbe endapo kila mmoja ataridhika kuwa Serikali inamjali basi atafanya kazi kwa moyo kabisa.

Pia, watumishi wanahitaji mafunzo ya mara kwa mara ili waweze kuboresha utumishi wao serikalini. Baadhi ya watumishi ufanisi wao wa kazi unashuka sana kwa sababu hawana maarifa mapya na wengine wanafanya kwa mazoea.

Hili la wateule wako huko wilayani na mikoani. Kusema ukweli baadhi ya wateule wako uliowatuma huko mikoani wananyanyasa watendaji wa chini.

Labda hawajui kuwa cheo ni dhamana; kwa lugha nyepesi ni kuwa mwenye cheo anapaswa kuwa kimbilio kwa walio chini yake. Bahati mbaya baadhi ya viongozi ukisikia wanakuja huoni tena kama wao ni kimbilio. Viongozi unaowateua wanapaswa kuwa mamlaka za rufaa, lakini wanakuwa kinyume chake.

Madi mbalimbali

Nakuomba utatue hili la wafanyakazi wa umma kukopea ahadi za kulipwa malimbikizo ya mishahara wakiamini “labda mwezi huu tutapata”. Baadhi yetu hata tukitembea kwenye sehemu zetu tumenunua kofia ndefu kuficha nyuso zetu wanaotudai wasituone. Hili la maslahi ya wafanyakazi hasa mishahara, malimbikizo, pensheni na mengine ni vilio vikubwa na vya muda mrefu.

Bahati nzuri wewe unaelewa kuwa mgomba haushindwi na mkunguwe. Mimi ni mfiwa ninayeanza kulia. Sisi ni kama punda wako shambani, huwezi kufikia malengo yako ya kuitengeneza Tanzania kama hutajali maslahi ya watumishi wako, ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakiishi kwa matumaini.

Faraja Kristomus ni mhadhiri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.



Columnist: mwananchi.co.tz