Wajibu wa Bunge kama chombo cha uwakilishi wa wananchi ni kuisimamia, kuidhibiti na kuishauri Serikali kwa niaba ya wananchi ili ifanye kazi yenye maslahi ya wananchi. Maslahi hayo yanaguswa katika huduma za kiusalama, kijamii na kiuchumi.
Bunge linatakiwa kuelekeza kipaumbele katika suala la usalama kwa sababu ndiyo huduma namba moja kwa nchi iliyo huru. Baada ya mwananchi kuwa huru, kitu cha pili ni usalama wake. Watu wanapoanza kujihisi hawapo salama, ni sawa na kusema kwamba hawapo huru.
Huduma za kijamii, maendeleo na uchumi huwa na mantiki ikiwa wananchi wapo huru na wanajisikia salama. Mahali ambapo usalama wa watu unahatarishwa na kujengewa hofu, kipaumbele cha Bunge kinatakiwa kujikita katika eneo hilo kwanza.
Tatizo lililopo mbele yetu sasa ndilo linapaswa kuwa sehemu ya wajibu wa Bunge letu. Mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo’ alitekwa Oktoba 11. Akashikiliwa kwa siku nane na kuachiwa usiku wa manane, Oktoba 20.
Watu waliomteka na kumshikilia hawajajulikana. Inadaiwa walitaka fedha, lakini hawakufanya lolote ili kupata hizo fedha. Walikaa naye tu kisha wakamwachia.
Wakati sintofahamu hiyo ikiendelea, Oktoba 12, kitengo cha mawasiliano na habari cha Bunge kilitoa taarifa kwa vyombo vya habari yenye kueleza kwamba ratiba ya kamati 14 za kudumu za Bunge zingeanza kukutana Oktoba 21. Dhahiri taarifa hiyo ilitoka siku moja baada ya Mo kutekwa.
Majukumu ya kamati yaliainishwa kuwa ni; Mosi, uchambuzi wa taarifa mbalimbali za Msajili wa Hazina kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma katika mashirika na taasisi mbalimbali nchini. Pili, uchambuzi wa taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu katika mwaka wa fedha 2016-2017.
Tatu, uchambuzi wa taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu hesabu zilizokaguliwa za Serikali za Mitaa katika mwaka wa fedha 2016-2017.
Nne, uchambuzi wa taarifa za utekelezaji wa majukumu ya wizara na taasisi mbalimbali za Serikali.
Tano, uchambuzi wa sheria ndogo zilizowasilishwa bungeni Septemba 10, mwaka huu wakati wa mkutano wa 12.
Kukutana na kamati hizo na kutekeleza majukumu yaliyoainishwa ni mwanzo wa Mkutano wa 13 wa Bunge unaotarajiwa kuanza mwezi huu. Shughuli zote zilizotajwa zina umuhimu mkubwa, lakini kwa vile usalama wa watu ndiyo kitu muhimu cha kutimiza uhuru wao, inatakiwa matukio ya utekaji yalitikise Bunge.
Umuhimu wa usalama wa wananchi unaona na kila mtu. Waziri mkuu mstaafu, John Malecela alisema hivi karibuni kuhusu matukio ya utekaji, akalitaka Jeshi la Polisi lijitathmini.
Alisema Jeshi la Polisi lilipaswa kuwa limejiandaa kukabiliana na matukio ya utekaji watu.
Malecela aliyeihudumia nchi tangu Serikali ya awamu ya kwanza na kustaafu awamu ya nne, neno lake lina ujazo kwamba vitendo vya utekaji havitakiwi kufanywa kuwa mazoea. Mshangao wake unaenda pamoja na shutuma kwa polisi kutofanya maandalizi dhidi ya uhalifu wa utekaji watu.
Hoja ya Malecela ni kuwa kutokana na kasi ya maendeleo ya kiuchumi, Tanzania ilikuwa lazima ingeufikia uhalifu wa utekaji watu kwa lengo la kujipatia fedha, hivyo polisi hawatakiwi kusubiri uhalifu mpya utokee, bali wajifunze unapotokea kwingineko duniani na kujiandaa kuukabili.
Endapo polisi wangekuwa wamejifunza mbinu za kukabiliana na vitendo vya utekaji watu, pengine jeshi hilo lisingehangaika hadi kuonekana halina majibu yenye kutosheleza pindi linapokuwa kwenye operesheni za kukabiliana na watekaji.
Kwa jinsi hali ilivyokuwa, kwa watekaji kutofahamika hadi sasa na kufanikiwa kumrejesha Mo wenyewe, inaonekana jeshi hilo halijazoea mikikimikiki ya vitendo vya utekaji.
Ingawa kabla ya kumwachia Mo, polisi walitoa picha ya gari walilodai ndilo lililotumika kumpakia Mo, baada ya kumteka kwenye Hoteli ya Colosseum, Oysterbay na baadaye kumwachia katika eneo la Gymkana, watekaji walimshikilia mpaka walipoamua kumwachia.
Yapo maelezo ambayo polisi waliyatoa, ambayo kiukweli badala ya kujibu maswali ya wananchi kuhusu watekaji na vitendo vya utekaji, ndiyo kwanza yaliongeza maswali. Hata sasa Mo akiwa ameshapatikana, kurejea kwake kumekuwa na simulizi yenye vituo vingi na alama nyingi za mkato hadi kupoteza maudhui.
Kutokueleweka kwa taarifa za polisi kunasababisha wananchi watafute majibu yao wenyewe. Simulizi zinakuwa nyingi na inakuwa vigumu kutofautisha uongo na ukweli. Zipo simulizi za mitaani zinazowaogopesha raia kuhusu nchi yao, dola yao na vyombo vyao vya usalama. Na hiyo ndiyo hasara ya jumla.
Wananchi lazima wajiulize. Ni haki yao maana yanatokea kwenye nchi yao. Lazima waendelee kusikiliza kila hadithi yenye kupita kwenye masikio yao, kwani mamlaka zenye kupaswa kuusema ukweli na kumaliza utata hazitimizi wajibu ipasavyo. Katika hali kama hiyo, ni wajibu wa Bunge kikatiba kumsaidia mwananchi.
Sasa basi, Bunge la 11 katika mkutano wake wa 13, halina budi kutenga muda ili kushughulikia hali ya usalama wa nchi. Lilibane Jeshi la Polisi litoe maelezo ya namna ambavyo liliendesha upelelezi wake. Wananchi wanaamini kuna siri haijatolewa nyuma ya kutekwa na kuachiwa Mo. Wanaamini polisi wanaifahamu.
Aprili mwaka jana, wabunge Zitto Kabwe (Kigoma Mjini, ACT-Wazalendo) na Hussein Bashe (Nzega Mjini, CCM) walijitahidi kulishawishi Bunge lisitishe shughuli zake nyingine ili kujadili kadhia ya watu kutekwa na kupotea.
Jitihada hizo ziligonga ukuta, Bunge liliendelea na shughuli zake kama zilivyokuwa zimepangwa. Vitendo vya utekaji havikujadiliwa, vikaendelea.
Wakati huo mjadala ulikuwa unawagusa Ben Saanane ambaye alikuwa kada wa Chadema na msaidizi binafsi wa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.
Vilevile ulimgusa mwanamuziki wa Hip Hop nchini, Ibrahim Mshana ‘Roma Mkatoliki’, aliyetekwa akiwa na wenzake watatu. Roma na wenzake waliachiwa, Saanane mpaka leo hajulikani alipo, kama yupo hai au la!
Matokeo ya Bunge kutotoa umuhimu wa kujadili kadhia ya watu kupotea au kutekwa, imesababisha vitendo hivyo kuendelea. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Kigoma, Simon Kanguye na mwandishi wa habari wa kujitegemea, gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda nao walitoweka na mpaka leo haijulikani watarudi au ndiyo kimoja.
Mwendelezo wa kuonekana usalama wa watu ni mdogo, ulichagizwa na matukio ya idadi kubwa ya watu kufa na miili yao kuokotwa kwenye fukwe za Bahari ya Hindi pamoja na Mto Ruvu.
Haya ni mambo yenye kuwafanya wananchi watafute majibu. Na katika kuyatafuta, wanajikuta wanaamini fununu nyingi ambazo pengine haziukaribii ukweli.
Inaonekana vitendo vitaendelea. Dalili zinaonyesha watekaji ama wana nguvu na mbinu nyingi au wana kiburi. Namna walivyomteka na kumwachia Mo Dewji, mazingira waliyomteka na waliyomwachia, lazima Bunge kama chombo chenye kubeba sauti za wananchi, lisimame kidete, lihoji; mambo haya ni mpaka lini? Suluhu ni nini?
Bashe aliutangazia umma kwamba alikuwa kwenye maandalizi ya kuwasilisha bungeni hoja binafsi, yenye kuhusu vitendo vya utekaji na ukiukwaji wa haki za binadamu. Hoja hiyo ilikwenda na maji. Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema Bashe alikuwa anababaisha tu, hakuwa na hoja.
Bunge halipaswi kuthubutu kukimbia wajibu wake. Kama kuna dhambi kubwa litafanya ni kukwepa hoja ya usalama wa nchi dhidi ya utekaji, vifo tata na maiti zilizookotwa katika fukwe za Bahari ya Hindi. Bunge la Novemba tulione likibeba wajibu wake wa kikatiba. Vinginevyo lijipambanue kuwa siyo Bunge la wananchi, na lina maslahi mengine.
Kutekwa Mo Dewji kulivyobadili upepo nchini
Mo azungumza