Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mnangagwa wa Zimbabwe hajabadilika

12071 PIC+MNANANGWA TanzaniaWeb

Wed, 15 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani uliofanyika hivi karibuni nchini Zimbabwe ulitegemewa kuwa ungeleta mabadiliko ya kidemokrasia na kupunguza ukiukwaji wa haki za binadamu ambao umekuwa ukifanywa na vikosi vya ulinzi na usalama kwa amri za wanasiasa kwa muda mrefu, lakini inavyoonekana hali si hivyo.

Matokeo ya uchaguzi huo yalitangazwa na Tume ya Uchaguzi wa nchi hiyo (ZEC) baada ya kucheleweshwa kwa muda na kusababisha maandamano kutoka kambi ya upinzani kupinga ushindi wa Emmerson Mnangagwa.

Kuchaguliwa kwa Mnangagwa kwa asilimia 50.8 kumeleta maswali mengi miongoni mwa wafuatiliaji wa mambo nchini humo kwa sababu kura za urais zilikuwa za mwanzo kuhesabiwa na kutumwa makao makuu ya Tume mjini Harare, lakini katika mshangao yakawa ya mwisho kutoka na hata yalipotangazwa kiongozi wa chama cha MDC, Nelson Chamisa aliyakataa na kusema kumekuwa na uchakachuaji wa tarakimu. Alisema yeye ndiye alikuwa mshindi.

Wakati wafuasi wa MDC walipoandamana katika ofisi za ZEC kushinikiza matokeo hayo kutangazwa, vikosi vya jeshi havikuchelewa kufika hapo na kuwasambaratisha na taarifa za kuuawa kwa watu watatu zikatolewa na hata siku ya pili vikosi vya jeshi viliendelea kuwaandama wafuasi hao na watu wengine watatu wakauawa na kufikisha idadi ya waliokufa kuwa sita.

Licha ya kuwa chaguzi nyingi barani Afrika zinapofanyika hakuna aliye tayari kukubali matokeo yaliyo hasi kwake, lakini kitendo cha jeshi kuingia mitaani na kuanza kufanya kazi za Jeshi la Polisi lazima kizushe maswali kwa sababu jeshi kazi yake ni kulinda mipaka ili kukabiliana na adui wa nje na siyo raia wa Zimbabwe.

Imekuwa ni kawaida kwa jeshi la Zimbabwe kutoa matamshi ya kutokubali kupokea amri kutoka kwa Rais ambaye hakushiriki vita vya kumwondoa Ian Smith na wazungu wenzake katika utawala wa nchi hiyo mwaka 1980 vilivyojulikana kama vita vya Chimurenga.

Majigambo ya Zanu-PF

Hata wakati wa kampeni kuna baadhi ya maofisa wa Zanu-PF walikuwa wakijigamba kuwa wana uhakika wa kushinda kwa sababu wangepata usaidizi kutoka kwa Jeshi la Zimbabwe ambalo hakika halijawahi kujitenga na chama hicho kikongwe barani Afrika.

Hata jeshi hilo lilipomwondoa madarakani, Rais Robert Mugabe kwa kisingizio kuwa linapambana na kikundi cha watu 40 walio kuwa karibu na Mugabe na kwa hakika walikuwa wanamuunga mkono mke wake Grace, haikuwa kweli kwa sababu inajulikana wazi kuwa maofisa wa ngazi za juu wa jeshi hilo ndiyo wabobezi wa ulaji rushwa na hata mashirika ya kimataifa ya kupigania haki za binadamu yametoa lawama zao mara nyingi kuwa wamekuwa wakifanya biashara ya madini kama almasi na dhahabu wakiwatumikisha Wazimbabwe masikini kwa ujira mdogo. Biashara hiyo ni ya magendo kwa sababu wao wamekewa vikwazo vya kiuchumi na kutosafiri katika nchi za Ulaya na Marekani.

Nia ya maofisa wa jeshi hilo ilikuwa ni kumzuia Bibi Mugabe asiingie kwa sababu walijua fika kuwa ataondoa utukufu waliokuwa nao wa kujifanya kuwa wao ndiyo Zimbabwe na Zimbabwe ni wao. Kwa lugha rahisi ilikuwa kulinda maslahi binafsi ambayo wamekuwa wakijinufaisha nayo kutoka walipoingia katika kutawala nchi hiyo mwaka 1980.

Wakati Rais Mugabe alipomwondoa Joyce Mujuru kutoka makamu wake kwa visingizio vya kichawi na kutaka kumpindua na kumwingiza Mnangagwa, maofisa wa jeshi hilo hawakuwa na wasiwasi kwa sababu alitoka mwenzao na kuingia mwenzao lakini ilipoonekana kuwa baada ya Mnangagwa kuondoka atakayeingia hapo ni Grace Mugabe ikawa ni hapana.

Kwa kuwa Mnangagwa alikuwa ameishajiwekea akiba ya uaminifu kwa maofisa wa jeshi, ilikuwa jambo la ama wao au Mugabe na kwa kuwa wao walikuwa na zana za kijeshi walimshinda Mugabe aliyekubali kuachia madaraka na ndoto ya mkewe Grace kuwa Rais ikayeyuka.

Ukandamizaji wa upinzani

Ukandamizaji wa wapinzani nchini Zimbabwe haukuanza jana wala juzi, baada tu ya kupata uhuru miaka ya mwanzo ya 80, Rais Mugabe akishirikiana kwa karibu na Mnangagwa wakati huo akiwa Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa walianzisha kikosi cha jeshi maalumu na kukipa jina la Kikosi cha tano ambacho kiliwajibika moja kwa moja kwa waziri mkuu wakati huo Robert Mugabe.

Kikosi hicho ambacho kilipata mafunzo yake kutoka kwa wataalamu wa kijeshi kutoka Korea ya Kaskazini, kilikuwa na kazi moja ya kuangamiza watu wa kabila la Wandebele ambao nao kama wapigania uhuru wa Zimbabwe walikuwa na jeshi lao la ukombozi la Zapu.

Mateso na mauaji ambayo yalifanywa na kikosi hicho mpaka leo yamebaki kama kovu kwa Wazimbabwe na wapigania haki za binadamu kote ulimwenguni. Raia wa kabila la Wandebele wanaokadiriwa kuwa 20,000 waliuawa huku wakati mwingine waathirika wakitakiwa kuchimba makaburi yao wenyewe kabla hawajapigwa risasi na kuuawa.

Mauaji hayo ambayo baadaye yalikuja kujulikana kwa jina Guruhukundi kwa lugha ya kishona yenye maana ya kusafisha uchafu yanamtwika lawama za moja kwa moja Mnangagwa kama ambavyo Mugabe mwenyewe alivyosema kuwa ED Emmerson Dambuzo Mnangagwa, alifanya vitendo kinyume na amri yake siku ya maadhimisho ya kifo cha aliyekuwa kiongozi wa Zapu na Makamu wa Rais, Joshua Nkomo mwaka 2000.

Mwishoni mwa mwaka jana alipohudhuria mkutano wa jukwaa la wachumi huko Davos nchini Uswisi alipoulizwa na waandishi wa habari juu ya Guruhukundi, Mnangagwa alipiga chenga kujibu swali hilo na kusema kuwa yeye anajishughulisha na Zimbabwe mpya yenye mafanikio kwa wote kwa kuwa kabla ya hapo alishapiga hesabu zake vizuri kwa kutangaza kuwa wazungu walioporwa mashamba yao watalipwa fidia na hakuna uporaji wa ardhi tena Zimbabwe.

Vilevile aliahidi kuwa serikali yake ingeandaa uchaguzi ulio huru na wa haki kwa kufanya hivyo kabla ya safari ilikuwa ni rahisi kwake kuonekana kuwa ni mtu tofauti na Mugabe ambaye wazungu walimwona kama asiyetakiwa duniani.

Wafuasi wa upinzani nchini humo wanasema kuwa hali ya sasa kiusalama kwao ni mbaya kuliko wakati wa Mugabe. Mmoja wa Viongozi waandamizi wa upinzani kutoka chama cha MDC Alliance, Tendai Biti alikimbilia nchini Zambia akihofia usalama wake lakini nchi hiyo imemkatalia na kumrejesha kwao ambako ameshtakiwa, japo ameachiliwa kwa amri ya Mnangagwa lakini hali si shwari kwa wapinzani.

Jambo lililo wazi ni kuwa endapo vikosi vya jeshi visingeingia mjini Harare na maeneo mengine ambayo wafuasi wa upinzani wana nguvu bila amri kutoka kwa Rais ambaye ndiye mkuu wa majeshi, Emmerson Mnangagwa.

Uchaguzi wa 2008

Mwaka 2008 ulipofanyika uchaguzi Mkuu na Mugabe kushindwa kwa kura chache na Morgan Tsivangrai, matokeo ya urais yalicheleweshwa kwa mwezi mzima ili kupika tarakimu zilizofanya kuwepo kwa duru ya pili ya uchaguzi kati ya Mugabe na Tsivangrai ambaye alikuwa kiongozi wa MDC.

Imekuwa ikielezwa kuwa Rais Robert Mugabe wakati huo alikuwa amekubari kuwa ameshindwa kwa sababu kabla matokeo hajatangazwa Tsivangrai alimhakikishia kuwa hatashitakiwa kwa makosa aliyotenda akiwa uongozini na Mugabe aliwaita wasaidizi wake wa karibu 12 wakiwemo maofisa wa vyombo vya ulinzi na usalama na kuwaambia kuwa yuko tayari kumwachia Tsivangrai atawale lakini maofisa hao wakiongozwa na Mnangagwa walimkataria kuondoka.

Wakati maandalizi ya duru ya pili ya uchaguzi yakifanyika Vikosi vya usalama vikiongozwa na Mnangagwa viliendesha kampeni ya mateso, mauaji na vitisho katika maeneo ambayo yalikuwa ngome ya upinzani na hata kiongozi wao Tsivangrai alipigwa na kuumizwa vibaya huku akiwekwa rumande na kupelekwa mahakamani kwa makosa ya kuongoza vurugu.

Mnangagwa ni mtu ambaye amepitia katika idara ya usalama anajua kuwa ukitaka watu wakuamini usiwatishe na kwa kufanya hivyo utapata kile unachohitaji, anaendelea na maneno ya kujifanya anapenda amani na mshikamano miongoni mwa Wazimbabwe huku chini kwa chini vikosi vya ulinzi na usalama vikiendesha kampeni ya kunyanyasa wafuasi wa upinzani.

Wazimbabwe wataendelea kupiga kura wakidhani kuwa kuna demokrasia lakini jeshi la nchi hiyo ambalo kuna wakati halieleweki kama ndiyo serikari au chama tawala cha ZANU PF litaendelea kukataa matakwa yao kwa kisingizo kuwa hawakushiriki vita vya Chimurenga ambavyo vilileta uhuru wan chi hiyo.

Jumuiya za Kimataifa kama Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Kiuchumi na Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika ni lazima zianzishe juhudi za kuondoa utukufu na ufalme wa jeshi la Zimbabwe ambao ndiyo kikwazo katika maendeleo ya demokrasia na haki za binadamu.

[email protected], 0783 165 487

Columnist: mwananchi.co.tz