Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mkaa, nishati muhimu inayoharibu mazingira

39309 MKAA+PIC Mkaa, nishati muhimu inayoharibu mazingira

Mon, 4 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Unapozungumzia nishati ya uhakika kwa ajili ya kupikia, huwezi kuacha kuutaja mkaa.

Watu wengi hutumia nishati hiyo kwa sababu ni rahisi kupatikana na wanaweza kumudu gharama yake tofauti na nishati nyingine kama umeme na gesi.

Licha ya sifa yake ya kupatikana kwa urahisi na watu kumudu gharama zake, mkaa na kuni vinatajwa kuwa hatari kwa mazingira.

Moshi, vumbi na moto mkali ni miongoni mwa vitu wanavyokutana navyo waandaaji wa chakula wanaotumia mkaa na kuni jambo linaloweka rehani afya zao.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, inakadiriwa kuwa asilimia 61 ya ardhi imeharibika na inakabiliwa na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame kutokana na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na shughuli kama ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.

Naibu katibu mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Balozi Joseph Sokoine anasema ukataji wa miti kwa ajili ya mkaa umesababisha mmonyoko na upotevu wa rutuba kwenye udongo.

Balozi Sokoine anasema pamoja na kuwepo kwa athari za kimazingira matumizi ya kuni na mkaa yanaathiri afya.

“Biashara ya kuni na mkaa inatokana na ukataji wa miti katika misitu ya asili. Kwa sehemu kubwa ukataji huu unaenda kinyume na sheria na taratibu zilizowekwa za kuendesha biashara hii,” anasema Balozi Sokoine.

“Ripoti ya pili ya hali ya mazingira nchini ya mwaka 2014, inaonyesha kasi ya uharibifu wa misitu ni kubwa na kila mwaka zaidi ya hekta 46,942 huharibiwa.”

Anasema matumizi ya kuni na mkaa yanaathiri afya kwa watumiaji kama magonjwa yatokanayo na kuvuta hewa chafu na kuathiri mapafu, moyo na pia magonjwa ya kupumua kwa watoto.

Balozi Sokoine anasema utumiaji wa muda mrefu wa nishati hiyo pia husababisha magonjwa ya macho, kwa kuwa kuni na mkaa hutoa hewa na uchafu unaozidi kiasi kinachoruhusiwa kwa mujibu wa viwango vya kimataifa.

“Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) inakadiriwa kuwa takriban watu milioni 4.3 hufa kila mwaka kutokana na uchafuzi wa hewa itokanayo na nishati ya kuni na mkaa ndani ya nyumba,” anasema balozi huyo.

Anasema pamoja na kuwepo kwa  fikra kuwa kuni na mkaa hupatikana kwa urahisi na kwa bei ni  nafuu,  madhara yake kwenye mazingira na afya za binadamu yana gharama kubwa hasa kurejesha hali ya uoto wa asili na miti iliyokatwa pamoja na kutibu magonjwa  yatokanayo nishati hiyo.

Balozi Sokoine anasema mikoa ya Dodoma, Singida, Shinyanga, Manyara, Simiyu, Geita na Kilimanjaro ni miongoni mwa maeneo yalioathirika zaidi na ukataji wa miti kwa ajili ya matumizi ya mkaa.

“Hali hii imesababisha mikoa hiyo kuwa na upungufu mkubwa wa maji na uwezo mdogo wa kuzalisha mazao kwa sababu maeneo haya yameachwa wazi na hayana uoto na baadhi ya mito iliyokuwa ikitiririka mwaka mzima, hivi sasa haitiririshi kwa ufanisi,” anasema.

Hata hivyo, Balozi Sokoine anasema wizara hiyo imekuwa na ushirikiano wa karibu na wasambazaji wa gesi ya mitungi (LPG) na mwaka jana ilifanya majadiliano kuona uwezekano wa kuanzisha mchakato wa kupunguza bei ya gesi hiyo ili wananchi wengi wamudu.

“Maongezi hayo yalijadili pia kufungua vituo vingi vya usambazaji wa gesi katika mikoa yote nchini ili wananchi wengi waweze kuipata kwa urahisi na kwa bei nafuu,” anasema Balozi.

Balozi Sokoine anashauri watu binafsi, vikundi, taasisi, vyuo vya ufundi na wawekezaji mbalimbali kuendelea kubuni na kuanzisha viwanda vya uzalishaji wa mkaa mbadala.

Anasema kipaumbele cha Serikali ni kujenga uchumi wa viwanda. Matumizi ya mkaa mbadala yanatoa mchango wake mkubwa kwa kuwa na viwanda vya kutengeneza mkaa huo sanjari na  kuzalisha majiko sanifu na banifu kwa ajili ya  matumizi fanisi ya nishati hiyo.

Mmoja wa watumiaji wa mkaa, Pili Hamad anakubaliana na hoja ya madhara ya nishati hiyo, lakini anasema ni vigumu kuacha kuutumia kwa sababu ya unafuu wa bei na urahisi kupatikana.

“Naomba Serikali ifanye utaratibu wa kuwezesha wamiliki wa gesi kupunguza bei ili tuweze kuzidumu,” anashauri.

Kuhusu matumizi ya mkaa mbadala,  Pili anasema wanaoutengeneza bado hawajasambaa maeneo mengi, jambo linalosababisha baadhi ya watu kushindwa kuupata.

Leonard Kushoka, mkurugenzi wa kampuni ya Kuja na Kushoka, inayojikita katika kutengeneza mashine za mkaa mbadala, Lanasema madhara yanayotokana na mkaa wa kuni ni makubwa tofauti na mkaa mbadala.

Anmsema madhara huyo hudhibitiwa wakati wa uandaji wa mkaa mbadala na hivyo kuwa nafuu kwa watumiaji.

Anakubaliana na hoja kuwa mkaa mbadala bado haujasambaa, lakini hawajakata tamaa katika kuelimisha umma matumizi yake.

“Mapambano haya yanahitaji nguvu sana kwa sababu unawatoa wananchi kwenye utamaduni wa kutumia mkaa wa asili kuwapeleka wa kwenye mkaa mbadala, jambo ambalo ni gumu kwa mazingira ya Tanzania,” anasema Kushoka.

Mkaa sawa na mazao mengine

Mkurugenzi wa Idara ya Misitu kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Arjanson Mloge anasema biashara ya mkaa ni sawa na ya mazao mengine na imeruhusiwa kisheria na kuwekewa utaratibu.

Ananukuu Mwongozo wa Uvunaji Mazao ya Misitu wa mwaka 2017 kipengele 2(2.2)

Anasema uvunaji wa mazao yote kama mkaa unasimamiwa na sheria ya misitu Na 14 ya mwaka 2002, Kanuni za misitu za mwaka 2004, matangazo mbalimbali ya Serikali na mwongozo wa uvunaji endelevu na biashara ya mazao ya misitu.

Anasema anayetaka kuvuna mazao haya hutakiwa kupeleka maombi kwa kamati ya uvunaji.

Anasema baada ya maombi hayo kupitishwa, wavunaji hao wanatakiwa kusajiliwa kama wafanyabiashara wa mazao ya misitu na usajili hutolewa na ofisi ya meneja misitu wilaya na baadaye hupewa leseni ya uchomaji mkaa ambayo hutolewa na afisa misitu wa wilaya. Kwa mujibu wa Mloge, baada ya kuandaa tanuru na uchomaji wa mkaa kukamilika, magunia hayo yatasafirishwa kwa kutumia Hati ya Usafirishaji Mazao ya Misitu (T.P) inayoonyesha jina la mfanyabiashara, mahali na tarehe iliyotolewa.

Anasema hati hiyo itaonyesha idadi ya gunia zilizopakiwa kwenye chombo cha usafiri, namba ya usajili wa chombo hicho, njia na vituo vya ukaguzi, tarehe ya mwisho ya kutumika hati hiyo na mahali mkaa utakaposhushwa na lazima eneo hilo liwe limesajiliwa.

“Idadi ya wafanyabiashara walioruhusiwa na kamati za uvunaji wa mazao ya misitu kuvuna mkaa kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2018/2019 ni 613 na magunia 1,100,606 yameruhusiwa na kamati hizo kuvunwa kwa kipindi cha 2018/2019,”anasema Mloge.

Hata hivyo, idadi hiyo hubadilika kila mwaka kufuatana na Mipango ya Usimamizi ya misitu na mipango ya uvunaji miti. Na takwimu hizo ni kwa wafanyabiashara wale waliosajiliwa na TFS, haihusishi wavunaji wasiofuata taratibu.

Kwa mujibu wa Mloge, kiwango cha fedha kinachopatikana kutokana na ushuru hubadilika kulingana na uvunaji kwa kuzingatia mipango ya usimamizi wa misitu na mwaka  2017/2018  walifanikiwa kukusanya zaidi ya Sh6 bilioni kama  maduhuli ya Serikali  yanayotokana na mkaa.

Anasema biashara ya mkaa inategemewa zaidi na wananchi wenye kipato cha chini katika maeneo mbalimbali ikiwemo mijini huku zaidi ya asilimia 90.

Mloge anasema licha ya biashara hiyo kuwa halali, katika siku za karibuni imeonekana kuwa na uvunaji usio endelevu.

“Kuwepo kwa pikipiki zinazosafirisha bidhaa imefanya watengenezaji mkaa kuuweka mahali popote nje ya maeneo yaliyosajiliwa au kutengwa kwa ajili ya bishara ya mkaa,” anasema.

Hata hivyo, Mloge anasema TFS imeweka mikakati ya udhibiti wa biashara hiyo na ukataji ovyo wa miti na kuendelea kutoa elimu kwa njia mbalimbali.

Pia TFS inaimarisha doria za mara kwa mara katika maeneo ya uvunaji na barabara kuu ikiwa ni pamoja na kuanzisha kikosi maalum cha kufuatilia na kuzuia uharibifu wa misitu ambacho hutafafuta taarifa za uharibifu katika vyanzo na kuzuia mapema.



Columnist: mwananchi.co.tz