Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mjue koala, mnyama anayelala saa 22 kwa siku

Mnyama Koala.png Mjue koala, mnyama anayelala saa 22 kwa siku

Fri, 3 May 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati dunia ikiadhimisha siku ya mnyama wa porini aitwaye koala leo Mei 3, jamii imesisitizwa kuhusu umuhimu wa kulala na utunzaji wa mazingira.

Koala ni mnyama wa familia ya wombat ambaye kwa kawaida hupatikana nchini Australia.

Wanajulikana kwa vichwa vyao vikubwa, masikio mafupi yenye manyoya na miili isiyo na mkia na wanachukuliwa kuwa ndiyo alama ya Australia, kama ambavyo twiga huchukuliwa hapa nchini.

Sifa yao kubwa ni kulala sana. Wakati twiga hulala kwa wastani wa saa 1:09 kwa siku, koala hulala kwa kati ya saa 18 hadi 22 kwa siku. Kwa maana nyingine, hupata muda wa kujitafutia chakula kwa saa mbili hadi sita pekee kwa siku.

Siku ya Kimataifa ya Koala

Siku ya Koala huwaleta pamoja wana mazingira na wanaharakati wa wanyamapori katika kulinda na kuhifadhi mazingira ya koala.

Wanyama hao ni miongoni mwa aina 10 za wanyama zilizo hatarini kupotea duniani kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa muhimu wa mtandao wa National Today, Australia wanasherehekea siku hiyo kwa kupanda miti, kutekeleza njia za kupambana na ongezeko la joto ulimwenguni na huvaa fulana zenye majani ya mti wa mkalatusi na kushiriki sifa za kipekee za koala.

Inaelezwa kuwa ongezeko la joto la dunia ni miongoni mwa hatari zinazowakabili koala. Moto uliowashwa misituni mwaka 2020 uliwaathiri mamilioni ya koala na kuongeza umuhimu wa kuanzisha hatua za kuwalinda.

Siku ya Kimataifa ya Koala inalenga kuongeza uelewa kuhusu masuala yanayotishia maisha wanyama hao. Koala wanaweza kuishi tu katika misitu mizito ya mikatatusi.

Licha ya kuishi msituni, koala ni wanyama rafiki kwa binadamu. Wanakadiriwa kuwepo duniani kwa miaka zaidi ya milioni 25.

Tatizo la usingizi

Wakati koala akilala kwa saa 22, binadamu anatakiwa alale kwa wastani wa saa nane kwa siku ili kuendeleza afya na ustawi bora.

Hata hivyo, kumekuwa na tatizo la watu kukosa usingizi na kufikia kutumia dawa na wengine wamepona kwa kufuata ushauri.

Daktari wa upasuaji wa taasisi ya Falmouth Primary Care nchini Marekani, Dk Christopher L. Wathier anasema, "ikiwa hupati usingizi wa kutosha mara kwa mara, uko kwenye hatari ya kupata magonjwa ya muda mrefu kama vile ugonjwa wa moyo, shinikizo la juu la damu, unene wa kupindukia, kisukari na msongo wa mawazo.

"Ninaona wagonjwa wengi wenye matatizo ya usingizi, hasa wazee na moja ya mambo mabaya zaidi ambayo mtu yeyote anaweza kufanya ni kuwa tegemezi kwa dawa ili zimsaidie kulala," anasema.

Anapendekeza mtu ajaribu kufanya chochote ilia pate usingizi mzuri wa usiku badala ya kutumia vidonge vya usingizi.

"Kutokuwa na uwezo wa kulala ni suala la tabia, si suala la kemikali, hivyo kuongeza dawa kwenye utaratibu wako, inapaswa kuwa hatua ya mwisho. Vidonge vingi vya kulala vina athari hasi. Urithi na kuongezeka kwa kuanguka, hasa kwa wazee, ni athari za kawaida za vidonge vya kulala."

Mwanasaikolojia Isaac Lema wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, anasema tabia za watu kunywa pombe kupitiliza, kunywa kahawa kwa wingi na kutozingatia kanuni bora za kulala, zimewasababishia kukosa usingizi na matokeo yake kuhatarisha afya zao za akili.

“Wengine wana maumivu ya mwili na wengine wana magonjwa kama sonona na msongo wa mawazo, wengine wanaota ndoto za kutisha na wengine wanatembea wakiwa wamelala, mpaka anafungua mlango na kutoka nje.

“Wote hao tunawasaidia kwa kutibu kwanza magonjwa yanayosababisha hali hizo,” amesema.

Amewataka pia watu kuacha tabia zinazosababisha kukosa usingizi.

Mwanasaikolojia mwingine, Saldin Kimangale amesema kukosa usingizi au kupata usingizi wa mang'amung'amu ni ishara kuwa kuna changamoto nyingine ya kiafya.

“Inaweza kuwa afya ya akili au afya ya mwili na kuna wakati kukosa usingizi ndio ugonjwa wenyewe,” amesema.

Amesema tatizo hilo kwa kitaalamu huitwa ‘insomnia’ ambalo husababishwa na matumizi ya bidhaa zenye kafeini, magonjwa ya wasiwasi, sonona, msongo wa mawazo na mfadhaiko, kuchoka kupita kiasi, kuhamahama miji inayopelekea kukosa mtiririko wa saa na kuwa na maumivu.

“Ni vyema kumuona mtoa huduma ya afya ili akusaidie kutambua chanzo cha tatizo hilo na ukubwa wake badala ya kukimbilia kutumia dawa zinazodhaniwa zitakupa usingizi,” amesema.

Ametaja matibabu yake kuwa ni pamoja na dawa iwapo kuna sababu za kiafya na pia zipo tiba za kisaikolojia.

“Mara nyingi dawa ni mazoezi ya kutuliza au kuupumbaisha mwili (relaxation) na kuzingatia adabu za kulala kwa kutojishughulisha na mambo yanayohitaji umakini wakati wa kulala, kujiepusha na matumizi ya simu na runinga, kutolala na njaa au ukiwa umeshiba sana.

“Unapaswa kulala kwenye chumba tulivu na chenye giza, kutolala kwenye chumba chenye joto au baridi kali, kutolala ukiwa na haja; kubwa au ndogo, kuepuka kulala na jambo zito moyoni ambalo unaweza kulizungumza ukalimaliza na kuchelewa kulala,” amesema.

Akifafanua zaidi kuhusu kanuni bora za kulala, Kimangale amesema kuna muda unaitwa ‘sleep window’, ambao ukiuvuka bila kulala, utapata shida ya kupata usingizi na mzunguko wa usingizi haukamiliki.

Columnist: www.tanzaniaweb.live