Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Miradi ya kimkakati ijumuishe inayoibuliwa na wananchi

Thu, 20 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Miradi ya kimkakati ni ile inayohusisha ujenzi wa miundombinu tofauti itakayochochea kukuza uchumi kwa kipindi kirefu.

Baadhi ya miradi ya kimkakati kwa sasa nchini ni ujenzi wa reli ya ya kiwango cha kisasa (SGR), ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme katika Bonde la Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge) na ujenzi wa bomba la gesi kutoka Tanzania hadi Uganda.

Miradi mingine ya kimkakati ni ununuzi wa ndege kwa ajili ya kulifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), upanuzi wa bandari, usambazaji umeme vijijini na ujenzi wa hospitali za mikoa na rufaa.

Miradi ya kimkakati inatajwa kugharimu kiasi kikubwa cha fedha za Serikali kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato vikiwamo vya ndani, mikopo na misaada. Ujenzi wa reli ya kati unakisiwa kuhitaji kiasi cha Sh7 trilioni hadi kukamilika kwake.

Mradi wa kufua umeme huko Mto Rufiji unatarajiwa kuzalisha megawati 2,100 utakaoiongezea Tanzania nishati na kuiweka miongoni kwa nchi zinazozalisha umeme kwa gharama ya chini barani Afrika.

Hadi sasa, ununuzi wa ndege tatu aina ya Bombardier Q400 dash 8 na Boeing 787-8 Dremliner umeshafanyika zikitajwa kugharimu kiasi cha Sh739.6 bilioni. Hii yote ni miradi ya kimkakati ambayo ina lengo la kutengeneza miundombinu ya uchumi itakayolinufaisha Taifa miaka mingi ijayo.

Miradi hii ya kimkakati pamoja na sababu nyingine ina lengo la kuhakikisha Tanzania inafikia dira ya maendeleo ya Taifa 2025 mapema na kwa ufanisi. Kwa mfano ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha SGR utaongeza usafirishaji wa mizigo na abiria kote itakakofika, ndani na nje ya mipaka.

Ununuzi wa ndege nao utasisimua uchumi na kuongeza idadi ya watalii wanaoitembelea Tanzania. Kwa ujumla miradi yote ya kimkakati ina manufaa makubwa kwa wananchi kujiletea maendeleo endelevu na kuianza safari ya Serikali kujitegemea kibajeti.

Pamoja na dhamira njema ya Serikali kutekeleza miradi ya mikubwa ya kitaifa ambayo huridhiwa na Bunge, ipo haja ya kuipa kipaumbele pia miradi inayoibuliwa na wananchi katika ngazi ya kitongoji, kijiji au mtaa, kata na halmashauri.

Miradi hii ni ile inayopendekezwa na wananchi kwa ajili ya kutatua changamoto zilizopo katika maeneo yao ilhali ile mikubwa mingi imo kwenye ilani ya chama tawala.

Baada ya sera ya ugatuaji madaraka, wananchi kupitia mamlaka za Serikali za Mitaa, pamoja na mambo mengine, wamepewa uwezo wa kuibua miradi kwa kutathmini fursa na kuitekeleza kwa mapato ya halmashauri au ruzuku kutoka Serikali Kuu.

Takwimu zinaonyesha zaidi ya asilimia 90 ya halmashauri zinategemea zuruku kutoka Serikali Kuu ili kujiendesha. Ruzuku inayotegemewa ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Mfumo unaotumiwa kuibua miradi ya maendeleo umefafanuliwa vizuri katika muongozo ulioboreshwa wa ruzuku ya maendeleo ya Serikali za Mitaa. Kijiji au mtaa huibua miradi yao ya kipaumbele kwa utaratibu ulioanishwa na kuwasilisha ngazi ya kata. Utaratibu huendelea hivyo mpaka wilayani.

Kata hupokea miradi yote iliyopendekezwa kutoka kijijini au mtaani na kuiwasilisha katika kikao cha maendeleo ya kata kinachoongozwa na diwani husika katibu akiwa ofisa mtendaji wa kata hiyo.

Kikao hicho huwa na uwakilishi mpana wa wananchi kwani hujumuisha wenyeviti wa kijiji au mtaa na kitongoji. Pia hujumuisha maofisa watendaji na wataalam wa kata pamoja na maofisa maendeleo ya jamii, waratibu wa elimu, bwana au bibi shamba na wataalamu wengine ambao hualikwa kwa ajili ya ushauri elekezi.

Kikao cha maendeleo ya kata hupitisha miradi ya kipaumbele na kuiwasilisha ngazi ya halmashauri kwa uchambuzi kisha kuunganishwa kwenye miradi ya halmashauri.

Wananchi wamekuwa wakishiriki kuendeleza miradi wanayoibua na kazi ya Serikali huwa ni ukamilishaji. Takwimu zinaonyesha halmashauri nyingi kuwa na maboma ya madarasa, nyumba za walimu, zahanati na viporo vingine vya miradi ya maendeleo ambavyo walianzisha kwa matumaini ya Serikali kuikamilisha.

Pamoja na miradi ya kimakakati, Serikali ina jukumu la kukamilisha miradi inayoanzishwa kwa nguvu za wananchi pia hivyo maofisa wenye dhamana waipe kipaumbele ili nguvu za wananchi zisipotee bure.

Maeneo mengi, miradi iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi imekuwa ikichelewa kukamilika kutokana na kutopata fedha za kuimalizia kwa wakati. nSi tu jambo hilo huchelewesha manufaa ambayo wananchi husika waliyakusudia, huiweka kwenye hatari ya kuharibika hivyo kupoteza rasilimali zilizotumika mpaka kwenye hatua ilipofika.

Viongozi wa Serikali za Mitaa, kuanzia mwenyekiti mpaka diwani wanapaswa kuwasilisha taarifa za miradi iliyopo kwenye maeneo yao halmashauri ili fedha zitakapopatikana zitolewe na kutumika kulingana na vipaumbele hivyo.

Wataalamu wa halmashauri nao wanapaswa kushauri na kukumbusha juu ya ukamilishaji wa miradi ya aina hii ambayo manufaa yake yatawagusa wengi mara tu itakapokamilika. Ni vyema kufahamu kuwa Serikali inapopanga wananchi hao hupanga.

Columnist: mwananchi.co.tz