Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Mipango ya nchi huanzia darasani kwa wanafunzi

11604 Joseph+Chikaka TanzaniaWeb

Tue, 17 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tuanze makala haya kwa kufanya tafakuri tunduizi kuhusu maarifa, ujuzi na umahiri unaojengwa kwa wanafunzi kwa kutazama siku yao moja ya masomo.

Turejeshe mawazo yetu huko madarasani katika shule za awali, msingi, sekondari, vyuo na hata katika mfumo wa madarasa yasiyokuwa rasmi.

Tutazame namna ambavyo siku moja tu ya masomo inavyotumika nchi nzima. Je, ni kweli tunawaona wanafunzi wetu ambao ndiyo rasilimali watu watarajiwa; wakipata maarifa thabiti, ujuzi na umahiri wa kukabiliana na changamoto za maisha halisi ya Kitanzania?

Je, wanajengeka katika umahiri na kujitambua kuwa wao ni Watanzania na Waafrika, kimtazamo, kuishi na kuthamini maisha yao halisi? Je, wawezeshaji wao, wanajiamini kiasi cha kuweza kuwavusha kwa kuwapa silaha za ujuzi wa kushinda changamoto za kiuchumi, mabadiliko ya hali ya hewa na mabadiliko ya sayansi na teknolojia?

Tunaweza kujihoji maswali mengi kuhusu tafakari hiyo ya siku moja tu ya masomo nchi nzima. Mathalani, kujihoji pia kuhusu kile wanachojifunza kama huakisi vilivyo mipango yetu ya dira ya maendeleo ya taifa ya muda mfupi na muda mrefu.

Muhamo wa ruwaza katika mitaala ya elimu na maendeleo

Miaka ya 2004 mpaka 2007 kulikuwa na mchakato wa katika sekta ya elimu wa maboresho makubwa ya mitalaa nchini.

Maboresho hayo yalilenga masuala kadhaa yakiwamo kuhama kutoka katika mitalaa iliyojikita katika maarifa zaidi na kumfanya mwalimu kuwa kitovu cha ujifunzaji kwenda kwenye mitalaa inayokuza ujuzi na umahiri na yenye kumlenga mwanafunzi kuwa kitovu cha ujifunzaji.

Katika maboresho hayo mwalimu hupaswa kuwa msimamizi na mratibu wa mchakato wa ujifunzaji. Hivyo, njia na mbinu za ufundishaji na ujifunzaji zilizo shirikishi zilisisitizwa zaidi.

Miaka kadhaa imepita tangu maboresho hayo yafanyike. Jamii inategemea kuona wanafunzi walioivishwa katika mfumo huo wa kujenga ujuzi na umahiri wakibadilika na kutumia ujuzi huo katika shughuli mbalimbali za ujenzi wa Taifa.

Endapo wahitimu hao watashindwa kuthibitishia umahiri walioupata kwa vitendo; basi hiyo itakuwa ni changamoto kubwa kwa walimu, waandaaji wa mitalaa, wasimamizi wa elimu na wadau wote wa elimu.

Kwa upande wa walimu, wao hujihoji kupitia maandalio yao ya masomo kama kweli wanafunzi wanajifunza. Na kama malengo yao ya somo yamefikiwa ama walichopanga wanafunzi wapate wamekipata. Hayo yote wanapaswa kuyatenda huku yakishabihiana na matakwa ya maono mapana ya taifa ya maendeleo kupitia falsafa ya elimu.

Jamii ndiyo kipimo cha elimu bora

Ubora wa elimu hupimwa kutokana na vigezo vingi vya wataalamu na wadau wa elimu. Kipimo cha mwisho huwa ni jamii, ambayo hutazama matumizi lengwa ya elimu hiyo ambayo wameitafuta na kuigharamia kwa thamani kubwa. Jamii inatazama namna wahitimu wanavyotafsiri kwa vitendo elimu waliyopata.

Kwa mfano, jamii inawatazama wasomi wanatumiaje ujuzi wa kanuni za biashara, afya, demokrasia, kusoma, kuandika na kuhesabu katika kuboresha maisha. Kwa mfano, ni wangapi, wana uwezo wa kuandika barua za aina mbalimbali kwa usahihi au kuandika mihutasari ya vikao vya vikundi vyao wanavyosisitizwa kuviunda?

Ni wasomi wangapi huthubutu kuandika malalamiko yao katika mamlaka husika badala ya kunung’unika mitaani ama kufikiri kuwa kila suluhu itapatikana kwa njia ya maandamano? Pia, ni kwa kiwango gani wanatambua kuwa haki huambatana na wajibu?

Masuala yote hayo, hupaswa kutafsiriwa katika ngazi zetu mbalimbali za elimu. Jambo la kuzingatia ni kwamba kama kinachotendeka darasani nchi nzima kwa siku moja tu ya masomo, kitakuwa ni nadharia pekee isiyogusa ujuzi na umahiri wa kutekeleza mipango yetu ya sekta mbalimbali, tuna kazi nzito ya kufikia maendeleo endelevu.

Tofali la maendeleo huanza darasani

Ni dhahiri kwamba kama shabaha yetu kama taifa ni kurusha roketi angani, kutokomeza ujinga, umaskini na maradhi baada ya miaka kadhaa, hatuna budi malengo hayo yaanze kutekelezwa katika hatua mbalimbali katika madarasa yetu.

Kama shabaha yetu ni kuendelea kuwa taifa lenye amani, umoja na uzalendo, masuala hayo hayana budi kutekelezwa kupitia maandalio ya masomo ya walimu shuleni.

Darasa ni tanuru la kuoka wajasiriamali, wafanyabiashara na wataalamu wa sekta mbalimbali, hivyo mageuzi ya kiuchumi, kisiasa, kitaumaduni na kiteknolojia huanza darasani.

Darasa lina nguvu kubwa ya kubadili mitazamo na fikra za jamii kwa jumla na baadaye kuweza kuvunja nguvu ya uchumi hodhi na kufanya kuwa uchumi shirikishi. Aidha, lina kazi ya kuvunja mifumo kandamizi na kufanya kuwa mifumo huru ya kidemokrasia.

Kwa kutafakari kwa kiasi umuhimu wa yanayofanyika darasani katika mustakabali wa nchi, kila mmoja wetu ana wajibu wa kuona ni kwa kiasi gani tunaweza kuchangia kutoa mazingira wezeshi kwa wanafunzi au wahitimu wetu, ili watumie ujuzi wanaoupata kwa ajili ya ujenzi wa taifa.

Hivyo basi shughuli zote zinazofanyika darasani kila siku kuanzia ngazi ya elimu ya awali mpaka elimu ya juu, hutuamulia ni taifa la namna gani tunajenga. Kwa kuwa mipango ya nchi hutafsiriwa pia katika ngazi ya darasani, hatuna budi kama taifa kuendelea kufanya uwekezaji zaidi katika elimu yetu.

Columnist: mwananchi.co.tz